Zambia: Mtaalamu wa UN ataka ukandamizaji baada ya uchaguzi ukomeshwe na wafungwa wa kisiasa waachiliwe
Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujumuika, Gina Romero, leo tarehe 2 Septemba 2026 ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa hali ya demokrasia na haki za kibinadamu nchini Zambia baada ya uchaguzi, akitaka serikali kulinda misingi ya demokrasia na nafasi ya kiraia, pamoja na kukomesha mara moja hatua za kuwashtaki watu kwa sababu ya kutoa maoni ya kisiasa yanayopinga serikali.
Wito huo umetolewa kufuatia ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu baada ya uchaguzi, sambamba na madai mazito kuhusu dosari katika mchakato wa uchaguzi.
Romero pia ameeleza wasiwasi kuhusu viongozi waandamizi wa muungano wa upinzani kufunguliwa mashtaka ya uhaini ambayo anadai yametungwa, akionya kuwa hatua hiyo inaweka mfano hatari, hasa kwa kuwa uhaini ni kosa linaloweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo nchini Zambia.
Mbali na hayo, matukio ya vitisho dhidi ya wapiga kura, mashambulizi na utekaji nyara yameripotiwa, huku kuongezeka kwa ghasia na vifo, vikiwemo vya waziri wa zamani na wakala wa kituo cha kupigia kura, kukihitaji uchunguzi wa haraka wa kimataifa.
Nafasi ya kiraia yazidi kubanwa
Wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya wapinzani wa kisiasa ulikuwa tayari umeibuliwa na Romero katika mawasiliano rasmi na serikali. Mtaalamu huyo pia amewasiliana na mamlaka za Zambia kuhusu dalili za matatizo yaliyojitokeza katika miezi iliyotangulia uchaguzi mkuu.
Aidha, mwaka 2025, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki ya uhuru wa maoni na kujieleza aliibua wasiwasi kama huo katika matokeo muhimu ya ripoti yake kuhusu hali nchini Zambia.
Romero amesema mgogoro wa sasa unaakisi mwenendo mpana wa kuzidi kubanwa kwa nafasi ya kiraia, unaojumuisha kukamatwa kiholela kwa viongozi wa upinzani, wabunge na wanaharakati wa mashirika ya kiraia kwa mashtaka ambayo mara nyingi hayalingani na makosa yanayodaiwa au hayako wazi kisheria.
Hali hiyo imejitokeza pia katika kufutwa kwa mkutano wa RightsCon, unaotajwa kuwa mkutano mkubwa zaidi duniani kuhusu teknolojia na haki za kibinadamu, siku chache kabla ya kuanza kwake mjini Lusaka, baada ya taratibu za kiutawala kusitishwa na kukiwa na madai ya shinikizo la kisiasa kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Romero, kukamatwa kiholela, kufunguliwa kwa mashtaka yasiyolingana na makosa yanayodaiwa, yakiwemo ya uchochezi dhidi ya serikali na ujasusi, pamoja na kuwekwa kwa vikwazo dhidi ya mikusanyiko ya amani, kunakiuka viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR)
Wafungwa wa kisiasa waachiliwe
Romero amesema demokrasia yenye afya inahitaji sauti zote, zikiwemo za wapinzani wa kisiasa, viongozi wa kidini, mashirika ya kiraia na waandishi wa habari, ziweze kusikika kwa uhuru bila hofu, huku akizitaka mamlaka za Zambia kuwaachilia watu wote wanaoshikiliwa kwa sababu za kisiasa, kuheshimu uhuru wa msingi na kurejesha uwajibikaji wa kidemokrasia.
Mtaalamu huyo anaendelea kuwasiliana na mamlaka za Zambia kuhusu masuala hayo.