Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Kuepuka janga la tabianchi kunahitaji kuchukua hatua sasa

Mwanamke aliyevaa kofia ya majani na kubeba mfuko wa begani amesimama akiwa ameshika nguzo ndefu kwenye uwanja mkubwa wa udongo uliopasuka na kukauka, huku mashua ya zamani ya uvuvi ikiwa imepumzika kwenye ardhi kavu nyuma yake chini ya anga la kijivu na mawingu.
© Adobe Stock/Johnstocker Mwanamke akiwa amesimama kwenye udongo mkavu na vifaa vya uvuvi, ongezeko la joto duniani na mgogoro wa maji vinaathiri watu wengi.

UN: Kuepuka janga la tabianchi kunahitaji kuchukua hatua sasa

Tabianchi na mazingira

Mawimbi makubwa ya joto, mafuriko yenye kusababisha vifo na hali mbaya ya hewa vinaonesha dunia inayozidi kuchemka kwa joto na ambalo hivi karibuni liko katika hatari ya kuvuka viwango salama vya ongezeko la joto.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne. Hata hivyo, kuongeza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sasa kunaweza kusaidia kuzuia janga kubwa la tabianchi imesema ripoti hiyo.

Mambo muhimu

  • Hatua za haraka, za pamoja na za kimataifa ni muhimu ili kudhibiti ongezeko la joto lisivuke nyuzi joto 1.5°C
  • Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kubadili mwenendo wa sasa kwa kupunguza uchafuzi wa methane, kulinda ardhi, misitu na bahari, na kuharakisha kuondokana na matumizi ya nishati za visukuku
  • Kila sehemu ya ziada ya ongezeko la joto itagharimu maisha, kuharibu maisha na vyanzo vya kipato, kuongeza ukosefu wa usawa na kusukuma mifumo ya ikolojia karibu zaidi na uharibifu usioweza kurekebishwa
Joto kali lililokumba maeneo ya kaskazini mwa dunia katika miezi ya hivi karibuni, moto mkubwa wa nyika na mafuriko yenye kusababisha vifo, ni onyo kuhusu hali inayoweza kuikabili dunia siku zijazo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.
Amekumbusha kuwa Mkataba wa kihistoria wa Paris wa mwaka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliwashuhudia viongozi wa dunia wakiahidi kudhibiti ongezeko la joto hadi kufikia kiwango cha nyuzi joto 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Wanasayansi wanasema kiwango hicho ni muhimu ili kuepusha madhara makubwa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, dunia inashindwa kutimiza ahadi hiyo, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP).
“Mapambano ya kusalia na nyuzi joto 1.5 ni mapambano kwa ajili ya ubinadamu,” amesema Guterres. “Tuko katika mwelekeo wa kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5°C ndani ya miaka michache ijayo.”
Gari la umeme la rangi nyeupe limeunganishwa na kituo cha kuchaji cha rangi nyeusi katika eneo la maegesho lililozungukwa na miti na mimea ya kijani.
© Unsplash/Ratio EV Charging Kituo cha kuchaji magari ya umeme

Kila ziada ya ongezeko la joto itagharimu maisha

Hakuna matokeo mazuri endapo dunia itaendelea kuwa na viwango vya joto vinavyozidi nyuzi joto 1.5°C kwa muda mrefu, ameonya Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen.
“Kote duniani, mawimbi makali ya joto tayari yanaonesha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zitajitokeza kwa kasi zaidi, zitakuwa kali zaidi na kudumu kwa muda mrefu zaidi, na kusababisha vifo zaidi na kuvuruga maisha kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa “Ni wakati wa kuongeza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Tunaweza na lazima turudi kwenye njia sahihi. Kwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuimarisha mnepo na hatua za kukabiliana na athari, na kuhakikisha kuwa kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5°C kunakuwa kwa kiwango kidogo na kwa muda mfupi iwezekanavyo.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekubaliana na kauli hiyo.
“Kila sehemu ya ziada ya ongezeko la joto itagharimu maisha, kuharibu maisha na vyanzo vya kipato, kuongeza ukosefu wa usawa na kusukuma mifumo ya ikolojia karibu zaidi na uharibifu usioweza kurekebishwa, amesema Guterres. “Ubinadamu unakimbia kwa kasi kupita kiwango kinachohitajika ili kuepusha janga la tabianchi.”

Suluhisho tayari tunalo

Hata hivyo, hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuurudisha ulimwengu kutoka ukingoni mwa janga, amesema Guterres.
“Bado tunaweza kurejesha ongezeko la joto hadi chini ya nyuzi joto 1.5°C ifikapo mwishoni mwa karne hii,” amesema. “Lazima tufanye kipindi cha kuvuka kiwango hicho kiwe kifupi na kidogo iwezekanavyo,” huku tukidhibiti kiwango cha juu ambacho joto linaweza kufikia na muda litakaokaa juu ya nyuzi joto 1.5°C.
Hilo linahitaji ongezeko la azma” kupitia kuharakisha kuondokana na matumizi ya nishati za visukuku na kuendeleza mapinduzi ya nishati jadidifu, kupunguza uchafuzi wa methane na kulinda ardhi, misitu na bahari, amesema.
Pia, serikali zinapaswa kutekeleza kwa kiwango kikubwa zaidi mipango ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ahadi za kufikia uzalishaji sifuri wa gesi chafuzi na hatua nyingine zaidi. Nchi zilizoendelea zinapaswa kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari za tabianchi na kuhakikisha zinafika kwa watu walio katika hatari kubwa zaidi.
“Sayansi iko wazi,” amesema Guterres. “Suluhisho tunalo, na dunia haijawahi kuwa na uwezo mkubwa kama ilivyo sasa wa kuyatekeleza. Sasa ni wakati wa kuongeza azma na kuharakisha hatua.”
Wazima moto wawili waliovaa mavazi ya kujikinga wanaonekana kutoka nyuma, wakitembea kupitia moshi mzito kuelekea moto mkali wa msituni.
Unsplash/Mikhail Serdyukov Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika

Mambo muhimu katika ripoti mpya

  • Joto likizidi nyuzi joto 1.5°C, hatari na madhara yataongezeka kwa kila sehemu ya ziada ya ongezeko la joto na kila mwaka unaopita. Hii ni pamoja na hali mbaya zaidi ya hewa, kupotea kwa mifumo ya ikolojia na kuzamishwa kwa visiwa vidogo vinavyoendelea na miji ya pwani iliyo kwenye maeneo ya chini, pamoja na madhara makubwa kwa afya ya binadamu, uhakika wa chakula, maji, mazingira, miji, miundombinu na uchumi.
  • Uwezekano wa kuvuka mipaka ya mabadiliko yasiyoweza kurekebishwa unaongezeka kadiri kiwango na muda wa joto la juu unavyoongezeka, ikiwemo kuyumba kwa mabonge makubwa ya barafu na kuharibika kwa msitu wa Amazon.
  • Hatua za kupunguza uzalishaji na kukabiliana na athari za tabianchi lazima zitekelezwe kwa pamoja, huku kipaumbele kikitolewa kwa hatua zinazotumia nguvu ya mazingira, kama vile kupunguza joto kwa njia za asili.
  • Kufikia kiwango cha kutozalisha kabisa gesi chafuzi ni hatua muhimu kuelekea kupunguza uzalishaji huo hadi kufikia viwango hasi kwa muda mrefu.
  • Mafanikio yanahitaji utashi mkubwa wa kisiasa na ushirikiano wa kimataifa, sera madhubuti, utawala shirikishi na fedha.
  • Nchi zenye mchango mkubwa zaidi katika kusababisha mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kuchukua hatua kwa kasi zaidi na kwa azma kubwa zaidi