WFP: Shambulio la anga lateketeza chakula cha msaada Kordofan Sudan
Msaada wa Kibinadamu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelaani vikali shambulio la anga lililolenga malori mawili yaliyokuwa yamebeba chakula cha msaada kwa familia katika eneo la Dilling, jimbo la Kordofan Kusini nchini Sudan, tarehe 30 Agosti 2026.
Malori hayo yalikuwa yakielekea Kadugli na yalikuwa yametambulishwa wazi kwa mabango na bendera za WFP.
WFP imesema shambulio hilo limeteketeza zaidi ya tani 50 za chakula, ikiwemo nafaka, mbaazi za njano zilizogawanyika, mafuta ya mboga na chumvi.
Chakula hicho kingeweza kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu 5,800 kwa mwezi mmoja.
Karibu watu 58,000 wanahitaji msaada Kadugli
Katika eneo la Kadugli, WFP inatoa msaada kwa karibu watu 58,000 wanaokabiliwa na viwango vya dharura vya ukosefu wa chakula au hali mbaya zaidi, kupitia mgao wa chakula.
Shirika hilo limesema shambulio hili ni mfano wa hivi karibuni wa mazingira magumu ambayo WFP na mashirika mengine ya kibinadamu yanakabiliana nayo nchini Sudan.
Mashambulizi kwa huduma zakibinadamu yaongezeka
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, WFP imerekodi mashambulio manane ya anga ambayo yameharibu majengo yake na kuvuruga shughuli za utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Shirika hilo limesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi na operesheni za misaada ya kibinadamu hayawezi kukubalika.
WFP imewataka wote wanaohusika katika mapigano kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kuwalinda raia, wahudumu wa misaada na mali za kibinadamu.
“Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada na shughuli za kibinadamu hayakubaliki na lazima yakome,” imesisitiza WFP.