Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinsi mradi wa JP-RWEE unavyosaida kubadilisha maisha ya wanawake wa vijijini nchini Rwanda

Mwanamke aliyevaa blauzi yenye madoa mengi na sketi yenye rangi nyingi ameketi kwenye tarp nyeusi, akichambua mbegu za mahindi. Wafanyakazi wengine wanaonekana nyuma, pia wakichakata nafaka.
IFAD/Edward Echwalu Mwanamke anachambua mbegu za mahindi kwa ajili ya kuzihifadhi kaskazini mashariki mwa Rwanda.

Jinsi mradi wa JP-RWEE unavyosaida kubadilisha maisha ya wanawake wa vijijini nchini Rwanda

Wanawake

Kwa wanawake wengi wa vijijini nchini Rwanda, kupata ardhi na aina nyingine za mali ni muhimu katika kujihakikishia maisha, kusaidia familia zao na kujenga maisha yenye utulivu kwa siku zijazo.

Rwanda imepiga hatua kubwa katika kuweka mfumo wa kisheria unaohakikisha wanawake na wanaume wana haki sawa za kurithi. Hata hivyo, katika baadhi ya jamii, imani za kitamaduni, mitazamo ya jadi kuhusu majukumu ya wanawake na wanaume, pamoja na uelewa mdogo kuhusu sheria, bado vinaweza kuwazuia wanawake kutumia kikamilifu haki hizo.

Mpango wa pamoja unaoungwa mkono kifedha na Wakfu wa Gates unasaidia kukabiliana na baadhi ya vikwazo hivyo kwa kuunganisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na juhudi za kubadili mitazamo na kuimarisha ushirikiano ndani ya familia.

Mpango wa Pamoja wa Kuharakisha Maendeleo kuelekea Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake wa Vijijini, unaojulikana kama JP-RWEE, unatekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN Women, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) pamoja na wadau wengine.

Mpango huo unafanya kazi na wanawake na wanaume wa vijijini kuimarisha fursa za kiuchumi, kuboresha ujuzi wa kifedha na kuhamasisha ufanyaji wa maamuzi wenye usawa zaidi ndani ya familia.

Na kwa baadhi ya washiriki, mabadiliko hayo tayari yanaonekana katika maisha ya kila siku kuanzia ushirikiano mkubwa kati ya wanandoa hadi kuongezeka kwa uwezo wa wanawake kushiriki katika maamuzi kuhusu mali, akiba na rasilimali za uzalishaji.

Kwa Iragena Betty na mume wake, Jean Claude Iyakalyeme, mabadiliko yalianza na kubadilika kwa namna walivyozitazama nafasi zao ndani ya familia.

Kwa miaka mingi, nyumba yao ilikuwa imejaa mvutano na kutokubaliana.

“Tulikuwa na migogoro ambayo wakati mwingine ilifikia hatua ya kupigana kimwili,” anakumbuka Jean Claude.

Kiini cha migogoro hiyo kilikuwa mitazamo ya jadi kuhusu majukumu ya wanawake na wanaume.

Jean Claude aliamini kwamba, kwa kuwa yeye ndiye mwanaume wa familia, alipaswa kuwa na kauli ya mwisho kuhusu mali na mifugo ya familia.

“Hapo awali, niliamini kwamba mifugo yangu ilikuwa mali yangu pekee kwa sababu mimi ndiye mwanaume wa familia, na kwamba mke wangu hakuwa na haki ya kutoa maoni kuhusu jinsi nilivyoisimamia,” anasema.

“Kwa mfano, ikiwa ningeamua kuuza ng’ombe wangu, nilifikiri hakuwa na haki ya kupinga.”

Kubadilika kwa mitazamo, kubadilika kwa familia

Hali hiyo ilianza kubadilika baada ya wanandoa hao kushiriki katika mafunzo ya JP-RWEE kuhusu usawa wa kijinsia, uanaume chanya, majukumu ya pamoja na mawasiliano.

Jean Claude anasema mafunzo hayo yalianza taratibu kupinga na kubadilisha imani ambazo alikuwa amekulia nazo.

“Baada ya kumaliza mafunzo yetu, maisha yetu yalibadilika na kuwa mazuri,” anasema.

Mabadiliko hayo yalionekana pia katika uamuzi muhimu kuhusu maisha yao ya baadaye.

“Hata tuliamua kujenga nyumba.”

Wanandoa hao walikuwa wameishi pamoja kwa miaka 12 bila kuwa na nyumba yao wenyewe. Jean Claude anasema miezi mitatu tu baada ya mafunzo, waliamua kuanza ujenzi.

Kwa Betty, msaada huo umeleta hali mpya ya ushirikiano ndani ya familia.

“Ninashukuru kwa msaada, mafunzo na usaidizi kutoka katika mradi wa JP-RWEE. Ninathamini sana juhudi zao,” anasema.

Jean Claude anasema kinachomfurahisha zaidi ni kwamba sasa yeye na mke wake wanaweza kufanya maamuzi kwa pamoja.

“Kinachonifurahisha zaidi sasa ni kushirikiana na mke wangu; tunazungumza na kukubaliana kuhusu mambo yanayosaidia kuendeleza familia yetu,” anasema.

Uzoefu wao unaonyesha mojawapo ya misingi ya mpango huo: uwezeshaji wa wanawake kiuchumi unahusiana kwa karibu na uwezo wao wa kushiriki katika maamuzi kuhusu rasilimali zinazosaidia familia zao.

Kutoka kuishi katika nyumba hadi kuwa na haki juu yake

Kwa Uwitije Anastasie, suala la haki ya mali lilikuwa la moja kwa moja zaidi.

Aliishi katika nyumba kubwa na yenye thamani, lakini anasema kwa muda mrefu hakuhisi kuwa alikuwa na haki yoyote juu ya nyumba hiyo.

“Kwa mfano, mnaweza kuona jinsi nyumba hii ilivyo kubwa na nzuri; ina thamani kubwa,” anasema.

“Lakini kuishi ndani yake bila kuwa na haki yoyote juu yake kulikuwa kunakatisha tamaa sana na kunaweza kusababisha migogoro ndani ya familia.”

Mafunzo kupitia JP-RWEE yalimsaidia Anastasie na mume wake kuzungumzia suala hilo na kufikia makubaliano.

“Baada ya kupata mafunzo, mimi na mume wangu tulifikia makubaliano. Sasa nina haki kamili juu ya mali yetu,” anasema.

“Hakuna tena matatizo, na familia yetu ina furaha.”

Uwezeshaji wa kifedha

Madhara chanya ya mpango huo hayaishii katika haki za mali na mahusiano ndani ya familia.

Mshiriki mwingine, Jean Claude Munyabugingo, anasema kabla ya kuoa aliamini kuwa wanawake hawakuwa na haki ya kusimamia mali ya familia.

“Kabla ya kuoa, niliamini kwamba mwanamke hakuwa na haki ya kusimamia mali ya familia,” anasema.

Mke wake, Delphine Mujawimana, anasema mafunzo kuhusu usimamizi wa fedha za familia kwa wanandoa yaliwasaidia kubadilisha namna walivyokuwa wakisimamia fedha zao.

“Baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyotolewa na mradi wa JP-RWEE kuhusu usimamizi wa fedha za familia kwa wanandoa, hali yetu iliboreka kwa kiasi kikubwa,” anasema.

“Sasa tunaishi kwa amani na tunakua pamoja.”

Katika Wilaya ya Gisagara, Martine Niyinsenga anasema mpango huo pia uliwahamasisha washiriki kuunda vikundi vya kuweka na kukopa.

“Mradi wa JP-RWEE ulitupatia mafunzo na kutuhamasisha kuunda vikundi vya kuweka na kukopa, jambo ambalo lilitusaidia kusimamia fedha zetu kwa ufanisi zaidi,” anasema.

Mpango huo pia uliwahamasisha washiriki kutumia taasisi rasmi za kifedha.

“Sasa tunaweka hata fedha benki,” anaongeza Martine.

Kwa Nzabanyinshi Jacqueline, uwezeshaji wa kiuchumi unaonekana moja kwa moja katika mali alizofanikiwa kupata.

“Sasa ninamiliki ng’ombe, kuku, nguruwe na mbuzi,” anasema. “Nilipata vitu hivi vyote kupitia mradi wa JP-RWEE.”

Kujenga maisha ya baadaye kupitia akiba

Kwa Rachel Nyirankurikiyineza, ambaye pia anatoka Gisagara, uwezo wa kuweka akiba na kuwekeza tena umekuwa sehemu muhimu ya maisha yake ya kiuchumi.

“Tangu mradi wa JP-RWEE uanze, nimejifunza kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa,” anasema.

“Sasa ninaweza kupata fedha na kuzisimamia kwa ufanisi.”

Rachel anasema anawekeza tena sehemu ya mapato yake na kutumia sehemu ya fedha hizo kulipia bima ya afya.

“JP-RWEE imenisaidia sana kwa kunipatia mfuko wa akiba na aina nyingine za msaada,” anasema.

“Mungu awabariki, na natumaini wataendelea kuwasaidia wengine pia.”

Mabadiliko yanayovuka mipaka ya wanawake

Ingawa mpango huo unalenga uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake wa vijijini, mbinu yake inawahusisha kwa makusudi wanawake na wanaume.

Lengo si kuwapatia wanawake fursa za kiuchumi pekee, bali pia kushughulikia mitazamo ya kijamii na ya kifamilia inayoweza kuwazuia kunufaika kikamilifu na fursa hizo.

Kwa Betty na Jean Claude, mabadiliko yalianza kwa kujifunza kuonana kama washirika katika kufanya maamuzi.

Kwa Anastasie, ilimaanisha kutambuliwa kwa haki yake katika nyumba anayoishi.

Kwa Martine na Rachel, uwezeshaji unamaanisha kuwa na ujuzi na fursa zaidi za kuweka akiba, kusimamia na kuwekeza mapato yao.

Na kwa Jacqueline, mabadiliko hayo yanaonekana katika ng’ombe, kuku, nguruwe na mbuzi anaomiliki sasa.

Hadithi zao zinaonyesha namna uwezeshaji wa kiuchumi unavyoweza kwenda zaidi ya kuongeza kipato pekee.

Unaweza kumaanisha kuwa na sauti katika maamuzi ya familia, kuwa na udhibiti wa mali, kujenga usalama wa kifedha na kuimarisha mahusiano ndani ya familia.

Uzoefu wa JP-RWEE nchini Rwanda pia unaonyesha umuhimu wa kuwahusisha wanaume katika juhudi za kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Wanawake wanapopata fursa kubwa zaidi ya kupata na kumiliki mali, huduma za kifedha na maarifa — na wanaume wanapokuwa washirika katika kupinga mitazamo ya kijinsia inayowazuia wanawake — manufaa yanaweza kwenda mbali zaidi ya wanawake binafsi na kufikia familia na jamii zao.

Kwa familia hizi za vijijini nchini Rwanda, mabadiliko hayaanzi tu katika shughuli za kiuchumi, bali pia ndani ya nyumba.