UNAIDS, SADC na China washirikiana kuimarisha uzalishaji wa dawa Kusini mwa Afrika
UNAIDS, SADC na China washirikiana kuimarisha uzalishaji wa dawa Kusini mwa Afrika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Ukimwi, UNAIDS, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Taasisi ya Kimataifa ya Ubunifu wa Afya, GHII, wamewaleta pamoja serikali za Afrika Kusini na China, kampuni za dawa za China pamoja na washirika wa kikanda na kimataifa katika ushirikiano mpya unaolenga kuimarisha uzalishaji wa dawa Kusini mwa Afrika na kuongeza usalama wa afya katika ukanda huo.
Ushirikiano huo, ulioendelezwa kupitia juhudi zinazoongozwa na UNAIDS, unasukumwa mbele wiki hii kupitia majadiliano kati ya SADC na China yanayofanyika kuanzia tarehe 31 Agosti hadi 4 Septemba 2026 katika miji ya Johannesburg, Durban na Cape Town nchini Afrika Kusini.
Kwa kutumia mafunzo yaliyopatikana katika mwitikio dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), majadiliano hayo yanawakutanisha serikali, wazalishaji wa dawa, taasisi za utafiti, washirika wa kifedha na maendeleo pamoja na wataalamu wa afya ili kutathmini jinsi ushirikiano imara unavyoweza kuharakisha uzalishaji wa dawa, vifaa vya uchunguzi wa magonjwa na teknolojia za afya ndani ya ukanda huo.
Mkurugenzi wa UNAIDS Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Anne Githuku-Shongwe, amesema kuimarisha uzalishaji wa dawa ni zaidi ya kutengeneza dawa pekee, kwani kunahusu kuzipa nchi za Afrika udhibiti mkubwa zaidi wa bidhaa za afya ambazo wananchi wake wanazitegemea, zikiwemo zinazohusiana na VVU, huku pia kukijengwa ujuzi, uwekezaji, teknolojia na mifumo inayohitajika kuhakikisha usalama wa afya kwa muda mrefu.
Ushirikiano huo unakuja wakati ambapo uhakika wa afya, uimara wa mifumo ya ugavi na upatikanaji endelevu wa dawa muhimu ni miongoni mwa vipaumbele barani Afrika.
Kwa nchi za Kusini mwa Afrika, kuimarisha uwezo wa kuzalisha dawa ndani ya ukanda huo kunatoa fursa ya kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na athari zinazoweza kujitokeza pale mifumo ya kimataifa ya ugavi inapovurugika. Hatua hiyo pia inaweza kuchochea ubunifu, maendeleo ya ujuzi, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Dkt. Lamboly Kumboneki kutoka Sekretarieti ya SADC amesema uhakika wa afya unahitaji uwezo wa kuzalisha bidhaa muhimu za afya, huku ushirikiano na China ukiweza kusaidia kuunganisha uwezo wa uzalishaji barani Afrika na uwekezaji, teknolojia na ujuzi unaohitajika kuimarisha uzalishaji wa dawa katika ukanda huo.
Kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa dawa kikanda
Sehemu muhimu ya majadiliano hayo ni kutathmini jinsi ushirikiano kati ya China na Afrika unavyoweza kuwezesha uhamishaji wa teknolojia, uwekezaji, utaalamu wa uzalishaji na ubunifu ili kuimarisha uzalishaji wa dawa barani Afrika.
Ratiba ya majadiliano hayo inajumuisha mikutano ya ngazi ya juu ya kisera kati ya serikali na taasisi za udhibiti, mazungumzo na washirika wa maendeleo na kifedha, pamoja na ziara katika viwanda vya dawa na vituo vya utafiti katika miji ya Johannesburg, Durban na Cape Town.
Majadiliano hayo pia yanaangazia namna ya kuongeza uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia, kuboresha taarifa kuhusu masoko na mahitaji ya bidhaa, kuimarisha utayari wa mifumo ya udhibiti, ununuzi wa pamoja wa dawa na usalama wa upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya.
Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Ubunifu katika GHII, Gary Yang, amesema sekta ya afya nchini China imekua na kuimarika kwa kiwango kikubwa katika miongo kadhaa iliyopita na kampuni zake sasa zinatafuta fursa katika masoko ya kimataifa, huku Afrika ikitajwa kuwa soko la siku zijazo. Kwa mujibu wa Yang, utayari uliooneshwa na kampuni pamoja na watunga sera nchini Afrika Kusini unatoa fursa nzuri ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kupitia ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.
Majadiliano hayo yatakapohitimishwa tarehe 4 Septemba, washirika wanatarajiwa kubainisha maeneo ya kipaumbele na hatua mahsusi za kuimarisha uzalishaji wa dawa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na kuhakikisha usalama na upatikanaji endelevu wa dawa na bidhaa nyingine muhimu za afya.