Mkutano wa SCO: Guterres ataka mfumo wa dunia uendane na enzi ya leo
Mkutano wa SCO: Guterres ataka mfumo wa dunia uendane na enzi ya leo
Masuala ya UM
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kuimarishwa kwa mfumo wa dunia uwe wenye mamlaka ya kimataifa, akisisitiza kuwa taasisi za kimataifa lazima zifanyiwe mageuzi ili ziakisi hali halisi ya dunia ya leo.
Akizungumza leo Jumanne katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) mjini Bishkek Kyrgyzstan, Guterres amesema usawa wa mamlaka duniani umebadilika, lakini taasisi za kimataifa bado kwa kiasi kikubwa zinaakisi mazingira ya mwaka 1945.
‘Dunia yenye Malaka ya kimataifa ni jambo zuri’
Guterres amesema kuongezeka kwa wigo wa mamlaka duniani ni jambo chanya ambalo linapaswa kuimarishwa, lakini akasisitiza kuwa mabadiliko hayo lazima yaambatane na mageuzi ya taasisi zinazoratibu mahusiano ya kimataifa.
“Hili ni jambo zuri na linahitaji kuimarishwa,” amesema Guterres. Ameutaka Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi za Bretton Woods, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), zifanyiwe mageuzi ili ziendane na “uhalisia wa leo na kuzipa nchi zinazoendelea uwakilishi na ushawishi mkubwa zaidi.”
SCO yaongeza nafasi katika ushirikiano wa kimataifa
Guterres ameielezea SCO kama “nguzo muhimu ya mfumo wa kimataifa wa ushirikiano” na kutaja maeneo manne ambayo yanaweza kuimarishwa kupitia ushirikiano zaidi, usalama wa kimataifa, ufadhili wa maendeleo, mabadiliko ya tabianchi na akili mnemba.
Amesema mfumo wenye mamlaka ya kimataifa unaweza kuwa msingi wa haki katika utawala wa kimataifa na pia kusaidia kujenga ushirikiano madhubuti wa kimataifa unaozingatia sheria na kanuni za pamoja.
Guterres atoa wito wa kusitisha vita Ukraine
Akiwa mbele ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, Guterres amesema baada ya zaidi ya miaka minne ya vita nchini Ukraine, “ni wakati muafaka wa kuanzisha usitishaji kamili na wa mara moja wa mapigano.”
Amesema hatua hiyo inapaswa kufungua njia ya mazungumzo ya amani “ya haki, endelevu na ya kina,” kwa kuzingatia sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.
Kuhusu Mashariki ya Kati, ametoa wito wa kuheshimiwa kwa usitishaji mapigano na makubaliano yaliyopo, huku akitaka uhuru wa usafiri wa meli katika maeneo ya Mlango Bahari wa Hormuz na Bab al-Mandab ulindwe.
Gaza na Ukingo wa Magharibi
Kuhusu Gaza, Guterres amesisitiza kuwa usitishaji mapigano lazima uheshimiwe na vikwazo vinavyozuia misaada ya kibinadamu kuingia viondolewe mara moja. Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi ya walowezi na upanuzi wa makazi ya walowezi, akisisitiza kuwa amani ya kudumu inahitaji kuwepo kwa mataifa mawili, Israel na Palestina, yanayoishi pamoja kwa amani na usalama.
Mfumo wa fedha wa dunia ubadilike
Guterres amesema mageuzi hayo hayapaswi kuishia katika muundo wa kisiasa pekee, bali yanapaswa pia kufanyika katika mfumo wa fedha wa kimataifa. Ameonya kuwa nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni na kuzitaka benki za maendeleo za kimataifa kuwa “kubwa zaidi, bora zaidi na zenye ujasiri zaidi” katika kusaidia maendeleo.
Amesema mfumo wa sasa unahitaji kuhakikisha kuwa nchi zinazoendelea zinapata nafasi ya kutosha ya kufadhili vipaumbele vyao vya maendeleo.
Mabadiliko ya tabianchi yahitaji hatua za haraka
Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Guterres amesema dunia iko katika njia ya kuvuka kiwango cha ongezeko la joto cha nyuzi joto 1.5 Celsiasi, hivyo kuna haja ya kupunguza kwa kasi uzalishaji wa hewa chafu na kuharakisha mpito kuelekea nishati jadidifu.
Pia ametaka kuongezwa kwa kiasi kikubwa kwa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea, ambazo mara nyingi ndizo zinazoathirika zaidi licha ya kuchangia kwa kiwango kidogo katika uzalishaji wa hewa chafu.
Hakuna tena uporaji
Guterres amesisitiza pia umuhimu wa kusimamia kwa uwajibikaji madini muhimu yanayotumika katika teknolojia za mpito wa nishati.
Amesema uchimbaji wake lazima uwe “wa kuwajibika na endelevu” na uzisaidie nchi zinazozalisha madini hayo kupata sehemu kubwa zaidi ya thamani inayotokana nayo.
“Hakuna tena uporaji,” ametangaza, akitaka mfumo wa kimataifa unaohakikisha rasilimali za nchi zinazozalisha madini zinawanufaisha watu wake.
AI isiwe chini ya mamlaka ya mataifa machache
Kuhusu akili mnemba, Guterres ametaka kuwepo kwa mfumo wa utawala wa teknolojia hiyo ambao hauko chini ya udhibiti wa mataifa machache yenye nguvu kiteknolojia.
Ameunga mkono kuundwa, chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kwa kundi huru la kimataifa la wanasayansi pamoja na mazungumzo ya kimataifa kuhusu namna bora ya kusimamia utawala wa akili mnemba.
‘Tusibadilishe tu aina moja ya utawala na nyingine’
Akihitimisha ujumbe wake mjini Bishkek, Guterres amesema mfumo wa dunia unapaswa kubadilika ili kuakisi mgawanyo mpya wa mamlaka, lakini mabadiliko hayo hayapaswi kusababisha aina moja ya utawala kubadilishwa na aina nyingine. Badala yake, amesema, dunia inahitaji taasisi imara zinazoweza kuhakikisha kuwa sheria na kanuni zilezile zinawahusu wote, bila kujali ukubwa au nguvu ya nchi.