Kudhibiti Ebola DRC lazima tubadili tahadhari kuwa hatua za haraka: Fletcher
Kudhibiti Ebola DRC lazima tubadili tahadhari kuwa hatua za haraka: Fletcher
Afya
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Tom Fletcher, amesema dunia inapaswa kubadili tahadhari kuhusu mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa hatua za haraka, akionya kuwa virusi hivyo vinaenea kwa kasi kubwa kuliko juhudi za mwitikio.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mtandaoni na nchi wanachama leo tarehe 1 Septemba 2026, Fletcher amesema Ebola imeikumba DRC wakati nchi hiyo tayari inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu, huku karibu watu milioni 11 wakihitaji msaada.
Ebola si dharura ya afya pekee
Fletcher amesema mlipuko huo sasa umeenea katika majimbo sita, yakiwemo maeneo ambako ukosefu wa usalama unazuia wahudumu wa kibinadamu kuwafikia watu walioathirika.
Amesema hali hiyo inafanya iwe vigumu kugundua wagonjwa, kufuatilia waliokutana nao, kutoa matibabu na kujenga imani katika jamii. “Hii si dharura ya afya pekee. Pia ni dharura ya kibinadamu iliyojikita juu ya dharura nyingine nyingi za kibinadamu zilizopo tayari,” amesema.
Wanawake na wasichana, hasa wanawake wajawazito, wameathirika kwa kiwango kikubwa, huku watoto waliopoteza wazazi au walezi wakiwa katika hatari zaidi ya kunyanyaswa, kutumiwa vibaya na kusafirishwa kwa njia haramu.
Hatuwezi kukabili hatua kwa hatua
Akieleza hatua zinazochukuliwa, Fletcher amesema vituo vya operesheni vimeanzishwa Bunia na Beni, huku fedha za kibinadamu zikiendelea kuhamasishwa na uongozi wa mwitikio ukiimarishwa. Hata hivyo, amesema kasi ya kuenea kwa Ebola inahitaji operesheni kubwa na endelevu. “Hatuwezi kujibu kwa hatua ndogo kwa mlipuko ambao sasa unakua kwa kasi kubwa. Tunahitaji operesheni endelevu na ya kiwango kikubwa ambayo itatangulia virusi,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hizo zinahitaji kuongeza uwezo wa matibabu, timu zaidi za mazishi salama na yenye heshima, pamoja na kurahisisha usafirishaji wa wahudumu na vifaa vya misaada.
Wahudumu zaidi ya 40 wamefariki dunia
Fletcher amesema zaidi ya wahudumu 40 wa afya wamefariki dunia kutokana na Ebola wakiwa katika juhudi za kuokoa maisha ya wengine, huku vituo vya matibabu na magari ya wagonjwa pia yakishambuliwa. “Wahudumu hawa walio mstari wa mbele lazima walindwe,” amesisitiza.
Ameonya pia kuwa mapambano dhidi ya Ebola hayawezi kutenganishwa na mahitaji mengine ya kibinadamu, kwani watu wanahitaji huduma za afya zinazofanya kazi, maji safi, usafi wa mazingira, chakula, ulinzi na maisha yao ya kujikimu.
Wakati huo huo, juhudi za kujiandaa zimeimarishwa katika nchi jirani, hususan Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Muda hauko upande wetu
Akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, Fletcher amesema mpango wa mahitaji na hatua za kibinadamu kwa DRC mwaka 2026 unahitaji dola bilioni 2.1, zikiwemo dola milioni 300 kwa shughuli zinazohusiana na Ebola.
Ingawa zaidi ya dola bilioni moja zimepatikana, nusu ya pengo la ufadhili bado halijazibwa.
Kupitia Mfuko Mkuu wa Umoja wa Mataifa waHatua za Dharura (CERF), zaidi ya dola milioni 57 zimetengwa kwa hatua na maandalizi nchini DRC na nchi jirani. “Virusi havitusubiri tupate fedha. Muda hauko upande wetu,” amesema Fletcher, akitaka nchi wanachama kuongeza msaada unaobadilika kulingana na mahitaji, kuruhusu wahudumu na vifaa kufika kwa usalama na kuondoa vikwazo vya kibinadamu. “Tulichawahi kuishinda Ebola. Na tunaweza kuishinda tena.”