Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda yaimarisha ubora wa kofia ngumu ili kuokoa maisha ya watumiaji wa pikipiki

Gari la UNICEF likiingia kwenye lango la Hospitali ya Muhima mjini Kigali, Rwanda.
Picha: Screenshot_UNICEF video Kituo cha afya cha Muhima kilichoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Rwanda yaimarisha ubora wa kofia ngumu ili kuokoa maisha ya watumiaji wa pikipiki

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Zaidi ya safari milioni moja za pikipiki hufanyika katika barabara za Rwanda kila siku, huku usafiri huo ukiwa chanzo muhimu cha ajira na njia ya kila siku ya usafiri kwa wananchi wengi.

Hata hivyo, ajali inapotokea, ubora wa kofia anayovaa mwendesha pikipiki au abiria unaweza kutenganisha uhai na janga.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, takribani watu milioni 1.16 hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani kila mwaka. Zaidi ya nusu ni watumiaji wa barabara walio katika hatari zaidi, wakiwemo watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na waendesha pikipiki.

Utafiti wabaini changamoto

Robert Lisinge, Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia, Ubunifu, Muunganisho na Maendeleo ya Miundombinu katika Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika, ECA, anasema Rwanda inafanya vizuri katika usalama barabarani ikilinganishwa na nchi nyingi barani Afrika.

“Nchini Rwanda, idadi ya watu wanaopoteza maisha katika ajali za barabarani ni takribani 11.6 kwa kila watu 100,000, ikilinganishwa na zaidi ya watu 19 katika maeneo mengine ya bara la Afrika,” amesema.

Licha ya hatua hiyo, uchunguzi uliofanywa na shirika la Healthy People Rwanda, HPR, umebaini kuwa kuvaa kofia pekee hakutoshi ikiwa kofia hiyo imeharibika, haina ubora unaotakiwa au haijavaliwa kwa usahihi.

Mratibu wa mradi huo, Nadine Nivemfura, amesema asilimia 98.7 ya waendesha pikipiki na abiria waliochunguzwa walikuwa wamevaa kofia. Hata hivyo, ni asilimia 71 pekee waliokuwa wamezivaa kwa usahihi.

Aidha, asilimia 35.3 ya kofia zilizokuwa zikitumika zilionekana kuwa zimeharibika, huku asilimia 11 zikiwa zimeharibika vibaya sana.

Kanuni za Umoja wa Mataifa

Kufuatia changamoto hizo, Serikali ya Rwanda, ECA na Wakfu wa FIA wameunganisha nguvu kutekeleza mradi unaohakikisha kofia zinazotumika nchini humo zinakidhi viwango vya usalama.

Kwa mujibu wa Lisinge, hatua ya kwanza ilikuwa Rwanda kupitisha Kanuni Na. 22.06 ya Umoja wa Mataifa kuhusu kofia ngumu.

Kanuni hiyo ni miongoni mwa kanuni za usafiri zinazosimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Ulaya. Hatua nyingine ilikuwa kupata vifaa vya kupima kofia ili kuhakikisha zinazotumika Rwanda zinakidhi viwango vya Umoja wa Mataifa.

Samuel Mporanzi, Meneja wa Kitengo cha Kitaifa cha Uthibitishaji katika Bodi ya Viwango ya Rwanda, RSB, amesema bodi hiyo inaandaa viwango, kupima ubora na usalama wa kofia na kutoa uthibitisho.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa kofia zote zinazoingia nchini kupitia mipakani, pamoja na zile zinazouzwa sokoni, zinakidhi matakwa ya viwango vilivyowekwa,” amesema.

Mabadiliko yaonekana

Nivemfura amesema mradi huo umeanza kubadilisha tabia za watumiaji, huku watu wengi zaidi wakivaa kofia kwa usahihi na mahitaji ya kofia zilizothibitishwa yakiongezeka.

Mradi pia unaweza kufungua fursa za uwekezaji katika utengenezaji wa kofia. Lisinge anasema uzalishaji wa kofia una faida mbili: kuokoa maisha na kuibua biashara yenye manufaa kwa jamii.

Kwa waendesha boda boda, mabadiliko hayo yanagusa maisha yao moja kwa moja.

Nkurikiyehe Jean, ambaye alianza kuendesha boda boda mwaka 2018, amesema kofia walizotumia zamani zilikuwa laini na dhaifu na zingeweza kuvunjika wakati wa ajali.

“Kofia hizi mpya zilizo salama ni tofauti. Zina uwezo wa kupunguza nguvu ya mgongano na kumlinda mtu anapotokea ajali,” amesema.

Mutabazi Alex, mwendesha boda boda na meneja katika eneo la Gasabo, amesema kofia bora zimewafanya wajisikie salama zaidi.

“Ujumbe wangu kwa waendesha pikipiki wenzangu ni huu: huwezi kununua uhai. Usalama na maisha yako vina thamani kubwa zaidi kuliko fedha unazopata.”