Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Nepal: Idadi ya vifo yakaribia 1000 huku kukiwa na hofu kwa wanawake na wasichana

Wafanyakazi waliovalia sare na mavazi ya kiraia wakishughulikia mitungi ya plastiki nyeupe na masanduku ya kadibodi ndani ya ghala kubwa katika Eneo la Kuandaa Maandalizi ya Kibinadamu la Kathmandu wakati wa usafirishaji wa makazi ya dharura unaofadhiliwa na WFP.
© WFP/Sujita Thapa Magar Huko Kathmandu, vifaa muhimu vya dharura vinatayarishwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye vijiji vya milimani vilivyoathiriwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya matope katikati mwa kaskazini mwa Nepal.

Mafuriko Nepal: Idadi ya vifo yakaribia 1000 huku kukiwa na hofu kwa wanawake na wasichana

Tabianchi na mazingira

Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea nchini Nepal, wahudumu wa kibinadamu wanazingatia zaidi namna mafuriko makubwa ya ghafla yaliyosababisha vifo hivi karibuni yalivyoathiri wanawake na wasichana, pamoja na upatikanaji wa huduma za afya.

Idadi ya watu waliofariki dunia sasa imefikia 987, huku watu 4,247 bado hawajulikani walipo, amesema leo mjini Geneva Uswisi Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA).
Mafuriko hayo mabaya zaidi yalisababishwa na kuporomoka kwa barafu kutoka kwenye barafu kubwa ya mlima katika safu ya Himalaya, kwenye mpaka wa Nepal na China. Mamlaka nchini China zimeripoti kuwa watu 16 wamekufa na wengine 546 hawajulikani walipo, amesema Laerke.

Hatari bado zipo

Karibu wiki moja imepita tangu mafuriko hayo yalipoanza, na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) limeweza sasa kufika katika maeneo yaliyoathirika zaidi, likiwemo wilaya ya Rasuwa.
“Utafutaji wa manusura na uokoaji bado unaendelea, na msimu wa mvua za moonson bado haujakoma,” amesema Matt Baden, Meneja wa Operesheni wa IFRC anayesimamia mwitikio wa mgogoro wa Nepal, akizungumza kutoka Kathmandu.
“Njia za maji zilizozibwa bado ziko katika hatari ya kusababisha mafuriko zaidi, na tishio la maporomoko ya ardhi ni halisi na la haraka.”
Wakati huo huo, watu wanarudi katika maeneo yao kutafuta nyumba zao na kile kilichosalia kutokana na maafa hayo.
Watu hujenga jengo la gabion kando ya ukingo wa mto huko Nepal.
UNDP/Azza Aishath Wanawake wakijenga vizuizi nchini Nepal ili kuzuia mto kufurika na kufurika vijiji vilivyo karibu.

Wanawake na wasichana wanahitaji msaada

Kutokana na maafa hayo, takribani wanawake na wasichana 43,000 nchini Nepal sasa wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, kwa mujibu waShirika la Umoja wa Matafa la Masuala ya Wanawake UN Women.
Christine Arab, Mkurugenzi wa Kanda wa shirika hilo kwa Asia na Pasifiki, amesema washirika walioko katika maeneo yaliyoathirika wanasisitiza kuwa wanawake walionusurika wanakabiliwa na upungufu wa chakula, huku upatikanaji wa maji salama ukizidi kuwa mgumu na hatari za kiusalama zikiongezeka.
Amesema kuna hofu kwamba wanawake wanaweza kutengwa katika michakato ya kufanya maamuzi kuhusu mwitikio wa maafa na juhudi za kurejesha hali ya kawaida.

Maafa yanaonesha ukosefu wa usawa

Akizungumza na waandishi wa habari, amesema watu wengi ambao kwa kawaida hupokea msaada wa kibinadamu ikiwemo wanawake wajawazito, kina mama wanaonyonyesha na watu wenye ulemavu “wamesombwa na maji” kwa sababu hawakuweza kufika maeneo ya juu na salama.
“Na hili ndilo hutokea pale maafa yanapokutana na ukosefu wa usawa, watu ambao tayari wameachwa nyuma mara nyingi huwa wa kwanza kusombwa,” amesema akiwa Bangkok.
Kabla ya mafuriko hayo, wanawake na wasichana katika wilaya ya Rasuwa walikuwa tayari wakitumia saa kadhaa kila siku kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.
“Sasa wanawake hawa wanatuambia kwamba upatikanaji wa maji salama umekatika kabisa, kufuatia uharibifu wa mifumo ya maji, barabara na madaraja,” amesema.

Wanawake wana nafasi muhimu katika kujikwamua

Afisa huyo wa ngazi ya juu ameongeza kuwa chakula ndicho kipaumbele cha haraka zaidi kwa wanawake katika maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi.
Aidha, maafa huongeza hatari za ukatili wa kijinsia, unyonyaji na usafirishaji haramu wa binadamu, huku miundombinu na mifumo ya mawasiliano iliyoharibiwa ikifanya iwe vigumu zaidi kwa waathirika kutafuta msaada na kupata huduma za ulinzi.
“Mwitikio wa kibinadamu lazima utambue uzoefu wa wanawake na wasichana,” amesema. “Lazima uwafikie na uwashirikishe kama wadau muhimu katika juhudi za kurejesha hali ya kawaida nchini Nepal.”
Muuguzi katika PPE ya bluu anatembea katika chumba cha hospitali kilicho na vitanda, huko Janakpur, Nepal.
© UNICEF/Rupadhayay Muuguzi anaingia katika chumba cha hospitali huko Janakpur, wilaya ya Dhanusha, kusini mwa Nepal.

Upatikanaji wa huduma za afya ni muhimu

Kudumisha upatikanaji wa huduma za afya bado ni kipaumbele, amesema Christian Lindmeier, msemaji wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO).
Vituo sita vya afya vimeharibika au kusambaratishwa kabisa, huku vituo vingine viwili vikishindwa kufikika. Hii inamaanisha kwamba “watu walioko katika maeneo yaliyoathirika hawana kituo cha afya kinachopatikana wakati wanapohitaji huduma zaidi.”
Alisisitiza kwamba “wakati juhudi za haraka zinaendelea kulenga hatua za kuokoa maisha kuzuia athari za pili kwa afya ya umma ni muhimu vilevile.”
Bwana. Lindmeier ameeleza kuwa mafuriko, kuhama kwa watu, msongamano wa watu na maji yaliyotuama vinaweza kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa.
Kwa kuzingatia hilo, WHO inaunga mkono ufuatiliaji katika maeneo yaliyoathirika na maeneo ya chini ya mto ili kufuatilia uwezekano wa kuongezeka kwa dengue, homa ya scrub typhus na magonjwa mengine ya kuambukiza.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limesaidia kubaini dawa muhimu za kipaumbele, vifaa vya uchunguzi na mahitaji muhimu ya afya, huku likitoa mwongozo wa kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kuhusu kuzuia maambukizi na namna salama na yenye heshima ya kushughulikia miili ya watu waliofariki.