Hali ya kibinadamu Gaza na Ukingo wa Magharibi yazidi kuzorota
Hali ya kibinadamu Gaza na Ukingo wa Magharibi yazidi kuzorota
Amani na Usalama
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la Afya Duniani (WHO) yameonya kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.
Akizungumza na waandishi wa habari, kutokea London Uingereza, Mkurugenzi wa WFP nchini Palestina, Shaun Hughes, amesema shirika hilo litalazimika kupunguza kwa nusu idadi ya watu linaowasaidia katika Ukingo wa Magharibi kuanzia mwezi huu wa Septemba kutokana na upungufu wa fedha, licha ya mahitaji kuwa yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Takribani watu milioni moja, sawa na robo ya wakazi wa Ukingo wa Magharibi, sasa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, ikilinganishwa na asilimia 11 kabla ya kuongezeka kwa mzozo Oktoba 2023.
Hughes amesema kuongezeka kwa ghasia za walowezi, operesheni za kijeshi za Israel, vikwazo vya usafiri, ubomoaji na watu kulazimika kuyahama makazi yao kumeathiri maisha na kipato cha Wapalestina. Ukosefu wa ajira umeongezeka zaidi ya mara mbili hadi asilimia 30 tangu 2023.
WFP inasema inahitaji dola milioni 386 katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuzuia kupungua zaidi kwa msaada wa chakula katika Ukingo wa Magharibi na Gaza.
Gaza inakabiliwa na njaa na magonjwa
Huko Gaza, Hughes amesema mashambulizi ya anga na mabomu yameongezeka katika siku za hivi karibuni, huku baadhi ya maghala ya WFP yakiharibiwa.
Amesema theluthi mbili ya wakazi wa Gaza bado wanakabiliwa na viwango vya dharura vya njaa, na bila kuongezeka kwa msaada wa kibinadamu, hadi asilimia 90 ya wakazi wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkali wa chakula kabla ya mwisho wa mwaka.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa WHO katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel, Dkt. Reinhilde Van De Weerdt, akizungumza kutoka Gaza amesema uchafuzi wa maji unaongezeka Gaza na kuongeza hatari ya magonjwa.
WHO imepima zaidi ya sampuli 6,700 za maji kati ya Januari na Agosti. Uchafuzi wa maji unaotokana na vijidudu umeongezeka kutoka chini ya asilimia sita Januari hadi zaidi ya asilimia 18 mwezi Agosti.
Katika kipindi hicho, wagonjwa wa kuhara wamekaribia kuongezeka mara mbili.
WHO imeonya kuwa mifumo ya majitaka isiyofanya kazi, taka zisizokusanywa na maji machafu vinaongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa, huku maji yaliyotuama na mahema yenye unyevunyevu vikitoa mazingira ya mazalia ya mbu, bakteria na ukungu.
Huduma za afya bado hazitoshelezi
Dkt. Van De Weerdt amesema kumekuwa na ongezeko la huduma za afya, ikiwemo huduma za afya ya msingi na vitanda hospitalini, lakini maendeleo hayo hayajawa ya haraka wala ya kutosha.
WHO inasema takribani watu 6,600 wanahitaji huduma za muda mrefu kutokana na kukatwa viungo. Hata hivyo, viungo bandia havijaruhusiwa kuingia Gaza tangu Mei 2024.
Kufikia Julai 2026, ni asilimia 12 pekee ya takribani watu 4,600 waliopoteza viungo tangu Oktoba 2023 waliokuwa wamepatiwa viungo bandia vilivyoingizwa Gaza na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).
Mashirika hayo mawili yametaka kuongezwa kwa msaada wa kibinadamu, pamoja na kuruhusiwa kwa haraka na bila vikwazo kwa dawa, vifaa vya matibabu, vifaa vya maabara, mafuta na bidhaa nyingine muhimu.
WFP imeonya pia kuhusu hatari ya dunia kuhamisha mwelekeo wake kutoka Palestina wakati mahitaji ya watu yakiendelea kuwa makubwa.
“Huu si wakati wa kugeuka na kutazama upande mwingine,” amesema Hughes.