UDADAVUZI: Virusi vya Bundibugyo ni nini na vina tofauti gani na virusi vingine vinavyosababisha Ebola?
UDADAVUZI: Virusi vya Bundibugyo ni nini na vina tofauti gani na virusi vingine vinavyosababisha Ebola?
Virusi vya Bundibugyo (BDBV), ambavyo mwaka huu wa 2026 vimesababisha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, na kusambaa hadi Uganda, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) ni miongoni mwa virusi vya familia ya Filoviridae vinavyoweza kusababisha ugonjwa mkali na wakati mwingine kifo kwa binadamu.
Virusi vya familia ya Filoviridae ni vimelea vinavyoweza kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Familia hiyo inajumuisha virusi hatari kwa afya ya umma kama vile virusi vya Ebola (EBOV), virusi vya Marburg (MARV), virusi vya Sudan (SUDV) na virusi vya Bundibugyo (BDBV).
Virusi vya Bundibugyo ni nini?
Kwa mujibu wa WHO, virusi vya Bundibugyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007 katika maeneo ya Bundibugyo na Kikyo, wilayani Bundibugyo, magharibi mwa Uganda baada ya kuzuka kwa homa iliyokuwa inasababisha binadamu kuvuja damu.
Jina Bundibugyo linatokana na eneo hilo la Uganda ambako virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza.
Tangu wakati huo, milipuko mitatu inayosababishwa na virusi vya Bundibugyo imeripotiwa. Mlipuko wa kwanza ulitokea mwaka 2007 hadi 2008, wa pili mwaka 2012 na wa tatu ni mlipuko wa mwaka 2026, ulioanzia DRC na kusambaa kuvuka mpaka hadi Uganda.
WHO inasema mlipuko wa mwaka 2026 ndio mkubwa zaidi wa virusi vya Bundibugyo kuwahi kurekodiwa.
Bundibugyo ina tofauti gani na Ebola?
Ingawa virusi vya Bundibugyo vinaweza kusababisha ugonjwa wa Ebola, Bundibugyo si sawa na virusi vya Ebola vinavyojulikana kama EBOV.
Kwa mujibu wa WHO, virusi vya Ebola (EBOV), ambavyo hapo awali vilijulikana kama virusi vya Zaire, vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976 wakati milipuko miwili ilipotokea kwa wakati mmoja. Mmoja ulitokea katika eneo ambalo sasa ni Nzara nchini Sudan Kusini na mwingine katika eneo la Yambuku nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mlipuko wa Yambuku ulitokea katika kijiji kilicho karibu na Mto Ebola, ambao ndio uliotoa jina Ebola.
Virusi vya Sudan (SUDV) pia viliripotiwa kwa mara ya kwanza kusini mwa Sudan mwezi Juni mwaka 1976. Tangu wakati huo, virusi hivyo vimejitokeza mara kwa mara na kusababisha milipuko kadhaa barani Afrika.
Bundibugyo ilitambuliwa miaka 31 baadaye, mwaka 2007 nchini Uganda.
Kwa hiyo, Bundibugyo si jina jingine la virusi vya Ebola aina ya EBOV, bali ni aina tofauti ya virusi vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa Ebola.
Bundibugyo ilianzia wapi?
Historia ya virusi vya Bundibugyo inaanzia magharibi mwa Uganda.
Mwaka 2007, mlipuko wa homa ya kuvuja damu ulianza katika maeneo ya Bundibugyo na Kikyo, wilayani Bundibugyo. Uchunguzi uliofuata ulibaini kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na kirusi ambacho hakikuwa kimetambuliwa hapo awali.
Kirusi hicho hatimaye kikapewa jina Bundibugyo virus (BDBV) kutokana na eneo la Bundibugyo ambako kilitambuliwa kwa mara ya kwanza.
Baada ya mlipuko huo wa kwanza, Bundibugyo ilijitokeza tena mwaka elfu mbili na kumi na mbili.
Mwaka 2026, virusi hivyo vimejitokeza tena nchini DRC na kusambaa kuvuka mpaka hadi Uganda. Kwa mujibu wa WHO, huu ndio mlipuko mkubwa zaidi wa Bundibugyo kuwahi kurekodiwa.
Virusi vya Bundibugyo huambukizwaje?
Virusi vya Bundibugyo vinaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Baada ya kuingia katika jamii, vinaweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia mgusano wa moja kwa moja na damu au majimaji mengine ya mwili ya mtu aliyeambukizwa.
Maambukizi yanaweza pia kutokea kupitia vitu vilivyochafuliwa na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa.
Wahudumu wa afya, wanafamilia na watu wanaowahudumia wagonjwa wanaweza kuwa katika hatari zaidi ikiwa hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi hazitazingatiwa.
Dalili zake ni zipi?
Mtu aliyeambukizwa anaweza kuanza kuonesha dalili ghafla, zikiwemo homa, uchovu mkubwa, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa na koo.
Baadhi ya wagonjwa wanaweza baadaye kutapika, kuharisha, kupata vipele pamoja na matatizo ya figo na ini. Baadhi yao pia wanaweza kutokwa na damu ndani au nje ya mwili.
Kwa kuwa dalili hizo zinaweza kufanana na za magonjwa mengine, vipimo vya maabara ni muhimu katika kuthibitisha maambukizi.
Virusi vingine vya familia ya Filoviridae ni vipi?
Mbali na Bundibugyo, familia ya virusi ya Filoviridae inajumuisha virusi vya Ebola, Marburg na Sudan.
Virusi vya Marburg vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 baada ya wafanyakazi wa maabara katika miji ya Marburg na Frankfurt nchini Ujerumani na Belgrade, katika iliyokuwa Yugoslavia na sasa ni Serbia, kuambukizwa kirusi ambacho wakati huo hakikuwa kimetambuliwa.
Miaka tisa baadaye, mwaka elfu moja mia tisa sabini na sita, virusi vya Ebola vilitambuliwa kufuatia milipuko iliyotokea katika maeneo ambayo sasa ni Sudan Kusini na DRC.
Mwaka huo huo, virusi vya Sudan viliripotiwa kusini mwa Sudan, huku virusi vya Bundibugyo vikija kutambuliwa mwaka elfu mbili na saba nchini Uganda.
Kwa nini Bundibugyo ni tishio kwa afya ya umma?
Tangu virusi vya familia ya Filoviridae vilipotambuliwa, vimekuwa vikisababisha milipuko ya mara kwa mara barani Afrika. Ingawa milipuko mingi iliathiri idadi ndogo ya watu, mlipuko wa Ebola wa mwaka 2014 hadi 2016 katika Afrika Magharibi ulionesha ukubwa wa tishio linaloweza kusababishwa na virusi hivi.
Mlipuko huo ulikuwa mkubwa na tata zaidi wa Ebola kuwahi kurekodiwa na ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 1001 Sasa mlipuko wa Bundibugyo wa mwaka elfu mbili na ishirini na sita unaonesha tena kuwa virusi vya familia hii vinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma.
WHO inasisitiza umuhimu wa kugundua maambukizi mapema, kuwapatia wagonjwa huduma zinazofaa, kufuatilia watu waliokuwa karibu na walioambukizwa na kuimarisha hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Kwa hiyo, ingawa jina Bundibugyo huenda lisifahamike sana kama Ebola, virusi hivyo ni miongoni mwa virusi vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa Ebola na vinaweza kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma iwapo maambukizi hayatagunduliwa na kudhibitiwa mapema.