Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Barafu inapoyeyuka Himalaya, mafuriko hatari yanaweza kuwa ni hali ya kawaida

Mtu akiwa amesimama juu ya farasi anapita kwenye njia ngumu yenye miamba mbele, huku mlima mkubwa uliofunikwa na theluji ukitawala nyuma chini ya anga safi ya bluu.
© UN Nepal/Ajay Das Safu ya milima ya Himalaya inaenea kote Nepal.

Barafu inapoyeyuka Himalaya, mafuriko hatari yanaweza kuwa ni hali ya kawaida

Na Na Fabrice Robinet
Tabianchi na mazingira

Siku moja kabla ya ukuta wa barafu, miamba na maji yenye matope kuvamia mabonde ya Himalaya kwenye mpaka wa Nepal na China, Dipesh Chapagain alikuwa akizungumza na mwenzake kuhusu jinsi janga kama hilo lingeweza kuwa na madhara makubwa.

Kwa mtafiti huyo wa tabianchi mwenye umri wa miaka 40, aliyekulia katika milima ya mashariki mwa Nepal na ambaye sasa anachunguza majanga ya milimani katika Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa mjini Bonn, Ujerumani, suala hilo lilikuwa la kitaaluma na pia la kibinafsi.
Ameona mabadiliko katika hatari zinazoikabili eneo hilo ndani ya maisha yake mwenyewe.
“Nilipokuwa mtoto, haikuwa hivi,” aliniambia. “Hata wazazi wangu walipokuwa watoto au babu na bibi zangu, hili halikuwa changamoto kubwa waliyokabiliana nayo.”
Dipesh Chapagain amesimama katika jengo la kisasa lenye madirisha ya mbao na mimea ya kijani nyuma yake.
© UNU-EHS/Austin Gonzales Dipesh Chapagain, katika chuo kikuu cha UMOJA WA MATAIFA huko Bonn, Ujerumani.

Barafu inayeyuka, mlima unaanguka

Kisha, Jumatano asubuhi saa 8:37, sehemu ya mlima iliyokuwa juu katika Himalaya iliporomoka.
Mporomoko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba vifaa vya kupima mitetemeko ya ardhi vilirekodi tukio hilo kama tetemeko lenye ukubwa wa vipimo vya Richter 5.2, na mwanzoni kulidhaniwa kuwa ni tetemeko la ardhi. Mwamba uliokuwa chini ya barafu ya mlima uliporomoka, ukisababisha kiasi kikubwa cha barafu na miamba kusafiri takriban mita 1,200 kuelekea chini ya bonde.
Maji, mashapo na mawe makubwa vilisukumwa katika mito iliyokuwa chini, vikivamia miji na vijiji vilivyo kando ya mojawapo ya njia muhimu za biashara za Nepal na China. Katika kituo kimoja cha ufuatiliaji, kiwango cha maji kiliongezeka hadi mita tisa ndani ya nusu saa.
Kufikia Ijumaa, zaidi ya watu 500 walikuwa wameripotiwa kufariki dunia nchini Nepal na Tibet, huku zaidi ya 1,500 wakiwa hawajulikani walipo, wakiwemo mamia ya raia wa kigeni.
Familia ya karibu ya Dkt. Chapagain haikuathirika. Hata hivyo, habari hizo zilimuumiza kihisia.
“Daima ni vigumu kupokea taarifa hizi za majanga makubwa kutoka nyumbani,” amesema. “Yanazidi kutokea mara kwa mara na kuwa makali zaidi.”
Janga hilo ni mfano wa kutisha wa tatizo ambalo wanasayansi wa tabianchi wamekuwa wakionya kuhusu kwa miaka mingi. Mfumo wa barafu wa Himalaya unabadilika, na kuwaweka mamilioni ya watu katika hatari ambazo zinazidi kuwa ngumu kutabirika na, katika baadhi ya matukio, kuwa na madhara makubwa zaidi.
Picha za setilaiti za kando zikionyesha eneo la Timure huko Nepal kabla na baada ya mafuriko makubwa na maporomoko ya matope, huku kijiji kikionekana upande wa kushoto kikiwa kimefunikwa na mashapo upande wa kulia.
PBC ya Maabara ya Sayari Picha za setilaiti zinaonesha Timure, Nepal, kabla na baada ya mafuriko makubwa.

Mporomoko wa mlima ulivyogeuka kuwa mafuriko 

Wataalamu bado wanachunguza mfululizo wa matukio yaliyosababisha janga la Jumatano iliyopita. Uchambuzi wa picha za satelaiti unaonesha kuwa mwamba uliokuwa chini ya barafu ya mlima uliporomoka, na kusababisha kiasi kikubwa cha barafu na miamba kuingia katika Mto Lhende Khola, ambao ni tawi la Mto Bhotekoshi, na kuchochea mfululizo wa matukio yaliyofuata.
Mfumo huo unatofautiana na mafuriko yanayotokea wakati maziwa ya barafu yanapasuka, ambayo Dkt. Chapagain na wenzake katika mpango wa utafiti wa Global Mountain Safeguard Research, unaojulikana kama GLOMOS, wanayafanyia utafiti katika eneo lote la Hindu Kush Himalaya. GLOMOS ni sehemu ya Taasisi ya Mazingira na Usalama wa Binadamu ya Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa.
Utafiti wao wa hivi karibuni ulichambua mafuriko 493 ya aina hiyo, kuanzia kumbukumbu za awali zilizopatikana hadi mwaka 2024. Uligundua kuwa matukio hayo yameongezeka takriban mara tano tangu mwaka 1950, kutoka wastani wa matukio saba kila muongo hadi 34.
Kwa kawaida, mafuriko hayo hutokea wakati maji yanayotokana na kuyeyuka kwa barafu yanapokusanyika katika maziwa yaliyozungukwa na barafu inayorudi nyuma. Maziwa hayo mara nyingi huzuiwa na barafu isiyo imara au miamba na mashapo yaliyolegea. Mabwawa hayo ya asili yanapopasuka, kiasi kikubwa cha maji kinaweza kuachiliwa kwa ghafla.
Janga la Jumatano linaonekana kufuata mfululizo tofauti wa matukio.
“Safari hii, hatua ya kati ilirukwa,” amesema Dkt. Chapagain.
Badala ya ziwa la barafu kupasuka, miamba na barafu viliporomoka kutoka kando ya mlima na kusababisha mkondo mkubwa wa maji na uchafu chini. Watafiti wanachunguza iwapo mabaki hayo yalizuia mto kwa muda kabla ya kizuizi hicho kusombwa, lakini Dkt. Chapagain amesisitiza kuwa mfululizo huo bado haujathibitishwa.
Kwa wanasayansi, tofauti hiyo ni muhimu. Chini ya bonde, matokeo yanaweza kuonekana kuwa karibu sawa, kiasi kikubwa cha maji, barafu na uchafu huachiliwa bila onyo la kutosha katika mabonde membamba yenye watu.
Haijulikani iwapo mabadiliko ya tabianchi yalisababisha mporomoko wa Jumatano. Hata hivyo, ongezeko la joto duniani linabadilisha kwa kasi mazingira ya maeneo ya mwinuko mkubwa ambako majanga kama haya hutokea. Barafu inapoyeyuka na udongo ulioganda kwa muda mrefu (permafrost) kuyeyuka, miamba ambayo hapo awali ilikuwa imeshikiliwa au kuimarishwa na barafu inaweza kuwa isiyo imara, huku maji mengi zaidi yanayotokana na kuyeyuka kwa barafu yakizidisha kudhoofisha miteremko ya milima.
Madhara yanaenda mbali zaidi ya vijiji vya milimani. Eneo la Hindu Kush Himalaya hulisha mabonde makubwa 10 ya mito, ambayo takriban watu bilioni 2.1 hutegemea kwa ajili ya maji, chakula, nishati na maisha yao.
Mtazamo wa angani wa makazi ya Wanepali katika Wilaya ya Rasuwa umefunikwa na matope mazito ya kijivu baada ya mafuriko ya ghafla mnamo Agosti 26, huku majengo ya ghorofa nyingi na vifusi vikiharibiwa vikiwa vimetawanyika katika mandhari yote.
© UNICEF Matope yamefunika Wilaya ya Rasuwa katikati mwa Nepal kufuatia mafuriko makubwa.

Watu wanapohamia maeneo hatarishi

Lakini milima si kitu pekee kinachobadilika. Hali ya maisha ya watu wanaoishi chini ya milima hiyo pia inabadilika.
Dkt. Chapagain amesema alipokuwa mtoto, familia katika maeneo mengi ya milima ya Nepal zilikuwa zikijenga nyumba zao sehemu za juu za miteremko, huku zikilima mpunga na mazao mengine katika maeneo tambarare yaliyo karibu na mito. Nyumba ya familia yake ilikuwa juu ya mlima, huku mashamba yao ya mpunga yakiwa chini karibu na mto.
Kadiri muda ulivyopita, barabara, biashara, hoteli na miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu za maji imezidi kujikita katika mabonde ya mito, ambako ujenzi ni rahisi na fursa za kiuchumi ni nyingi. Dkt. Chapagain alisema vyanzo vya maji katika baadhi ya makazi ya maeneo ya juu pia vimeanza kukauka, jambo linalowasukuma watu kuhamia maeneo ya chini.
Hali hiyo imeleta muunganiko hatari, wakati ongezeko la joto linabadilisha milima iliyo juu, watu na miundombinu zaidi wanajikusanya katika njia ambazo maji na uchafu hushuka.
Bonde lililoathiriwa vibaya na mafuriko ya Jumatano ni mfano wa mgongano huo. Ukanda wa Bhote Koshi-Trishuli una njia kuu ya biashara kuelekea Kathmandu na umezungukwa na mitambo ya kuzalisha umeme kwa maji, madaraja, barabara, hoteli na makazi. Mafuriko hayo yaliharibu miundombinu ya nishati na kukata mawasiliano ya usafiri na mawasiliano katika eneo hilo.
Hatari hiyo ilikuwa tayari imeonekana. Mwaka jana, mafuriko yaliyosababishwa na kupasuka kwa ziwa la barafu yaliikumba mifumo hiyo hiyo ya mito, na kusababisha vifo vya watu tisa huku wengine 24 wakiripotiwa kutoweka.
Makazi yaliyofunikwa na matope katika Wilaya ya Nuwakot, Nepal, huku majengo yaliyoharibika na mashine za uokoaji zikifanya kazi baada ya mafuriko ya ghafla mnamo tarehe 26 Agosti 2026.
© UNICEF/Laxmi-Prasad-Ngakhusi Majengo katika jimbo la Bagmati nchini Nepal, yamefunikwa na matope baada ya mafuriko makubwa.

Dakika zinapokuwa muhimu

Kwa Dkt. Chapagain, janga la Jumatano pia limefichua udhaifu muhimu, muda mfupi sana wa onyo ambao jamii zinaweza kupata kabla janga linalotokea juu milimani kuwafikia.
Amesema mamlaka za Nepal ziligundua mafuriko hayo wakati tayari yalikuwa yakikaribia mpaka. Tahadhari zilisambazwa baadaye kuelekea maeneo ya chini kupitia ujumbe mfupi wa simu, mitandao ya kijamii, simu za kawaida na ving’ora.
Kwa maoni yake, kupunguza hatari kunapaswa kuanzia maeneo ya juu milimani: ufuatiliaji wa barafu na miteremko isiyo imara wakati wote, uchunguzi wa satelaiti, vipimo vya hali ya hewa na mito, pamoja na mifumo ya tahadhari ya mapema inayoweza kuyapa jamii muda wa kutosha wa kuondoka katika maeneo hatarishi. Kwa kuwa mito na barafu haviheshimu mipaka ya nchi, China, Nepal na nchi nyingine zilizo chini ya mkondo zinapaswa pia kubadilishana taarifa kwa haraka.
Kuna tatizo kubwa zaidi. Hata kama uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani ungepunguzwa kwa kiwango kikubwa, Dkt. Chapagain amesema, barafu ingeendelea kupoteza ujazo kwa miongo kadhaa kutokana na ongezeko la joto ambalo tayari limejikita katika mfumo wa tabianchi. Kiasi gani cha barafu kitakachopotea hatimaye bado kiko mikononi mwa binadamu. Hata hivyo, kile kitakachotokea katika kipindi cha karibu hakiwezi kudhibitiwa kwa kiwango sawa.
Hilo linaifanya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa, kwa mtazamo wake, si maandalizi ya siku zijazo za mbali tena.
Kwa jamii zinazoishi chini ya Himalaya, siku hiyo ya baadaye ilifika Jumatano iliyopita.