Kina cha Bahari chapanda, hatari zinazoongezeka: Nini maanayake kwa binadamu?
Kina cha Bahari chapanda, hatari zinazoongezeka: Nini maanayake kwa binadamu?
Tabianchi na mazingira
Kina cha bahari kinaongezeka kwa kasi kubwa sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia iliyorekodiwa. Madhara yake tayari yanaonekana, na vitisho vinaendelea kuongezeka.
Ardhi inafunikwa na maji, nyumba zinafurika, na watu wanapoteza vyanzo vyao vya maisha, hali inayosababisha changamoto kubwa kwa watu wanaotafuta mustakabali salama zaidi.
Si mazingira pekee yanayoathirika. Kuongezeka kwa kina cha bahari pia kuna athari kubwa kwa haki za binadamu, maendeleo ya kiuchumi, afya, utamaduni, mustakabali wa nchi nyingi na utu wa msingi wa binadamu.
Kila mtu na karibu kila eneo linaathirika, katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Uwezo wa kuchukua hatua na kukabiliana na hali hii leo ndio utakaokuwa muhimu katika kuamua iwapo kina cha bahari kinachoongezeka kitakuwa changamoto inayoweza kudhibitiwa au janga litakaloathiri vizazi.
Kupanda kwa kina cha bahari ni nini?
Kwa ufupi, kina cha bahari kinaongezeka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binadamu.
Kati ya mwaka 2014 na 2023, kina cha bahari duniani kiliongezeka kwa milimita 4.7 kwa mwaka. Mwaka 2024, ongezeko hilo lilifikia rekodi ya milimita 5.9.
Hata katika hali yenye matumaini zaidi, bahari huenda ikaongezeka kina hadi mita 0.55 ifikapo mwaka 2100, katika hali mbaya zaidi, ongezeko hilo linaweza kuwa zaidi ya mita moja.
Chini ya hali ya uzalishaji mkubwa wa gesi zinazochangia ongezeko la joto, kuna uwezekano mdogo lakini wenye madhara makubwa wa kina cha bahari kuongezeka karibu mita mbili ifikapo mwisho wa karne hii.
Ni nini kinachosababisha ongezeko hilo?
- Kuyeyuka kwa barafu za milimani na tabaka kubwa za barafu.
- Ongezeko la maji kutokana na joto: bahari inapopata joto, maji hupanuka na kuchukua nafasi kubwa zaidi.
- Takriban asilimia 91 ya joto la ziada duniani linafyonzwa na bahari. Hivyo, kadiri tabianchi inavyozidi kupata joto kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi hatari, ongezeko zaidi la kina cha bahari linawekwa katika mfumo wa dunia kwa siku zijazo.
Athari kwa binadamu
Takriban watu milioni 770, sawa na karibu mtu mmoja kati ya 10 duniani, wanaishi chini ya mita tano kutoka kiwango cha juu cha maji wakati wa mafuriko ya bahari.
Huo ni ukaribu wa kutisha, na madhara yake tayari yanaonekana.
- Visima vya maji safi na mashamba vinaanza kuathiriwa na chumvi.
- Mafuriko yanaharibu hospitali, shule na mifumo ya usafi wa mazingira.
- Kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yanayoenezwa kupitia maji kunatishia upatikanaji wa maji ya kunywa na kuchangia kuongezeka kwa msongo wa mawazo.
Uvuvi na utalii, ambao ni nguzo za uchumi wa maeneo mengi ya pwani, vinaathirika.
Nyumba zimepotea baharini kutokana na mmomonyoko wa pwani huko Puerto Rico katika Karibiani.
Baadhi ya makadirio yanaonesha kuwa hadi watu bilioni 1.2 wanaweza kulazimika kuhama makazi duniani ifikapo mwaka 2050, si kwa kutafuta tu maeneo salama, bali pia maeneo ambako wanaweza kujenga upya maisha na vyanzo vyao vya kipato.
Ushahidi mpya unaonesha pia kuwa hatari zinazotokana na kuongezeka kwa kina cha bahari huenda zimepuuzwa kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya maeneo, ikimaanisha kuwa makumi ya mamilioni ya watu zaidi wanaweza kuwa katika hatari kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Zaidi ya athari za kimwili, urithi wa kitamaduni, ardhi za mababu na njia za jadi za maisha vinapotea, hali inayosababisha madhara makubwa ya kisaikolojia.
Gharama ya ongezeko la kina cha bahari
- Uharibifu wa miundombinu ya maeneo ya pwani tayari umezidi dola trilioni 1.8.
- Bila hatua za kukabiliana na hali hiyo, hasara za kila mwaka duniani zinaweza kufikia dola trilioni 1.4.
- Nchi zinazoendelea za visiwa vidogo zilipoteza dola bilioni 153 kutokana na majanga ya tabianchi kati ya mwaka 1970 na 2020.
- Malipo ya bima ya nyumba nchini Marekani yaliongezeka kwa asilimia 33 kati ya 2020 na 2023 katika maeneo yenye hatari ya majanga.
Bandari zinazohudumia zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya dunia zinazidi kuwa katika hatari ya mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari, jambo linalotishia minyororo ya usambazaji duniani.
Miji ya kisasa kama Guangzhou nchini China inakabiliwa na mafuriko huku kina cha bahari kikiongezeka.
Ni maeneo gani yaliyo katika hatari zaidi?
Nchi nyingi zinazokabiliwa na hatari kubwa zaidi kwa sasa ndizo zinazochangia kwa kiwango kidogo zaidi uzalishaji wa gesi zinazosababisha ongezeko la kina cha bahari, na mara nyingi zina rasilimali chache za kukabiliana na hali hiyo.
- Visiwa vidogo: Baadhi ya nchi za Pasifiki zinakabiliwa na ongezeko la kina cha bahari linalozidi mara mbili ya wastani wa dunia na ziko katika hatari kubwa kutokana na mafuriko yanayotokea mara kwa mara.
- Miji ya delta iliyo kwenye maeneo ya chini: Dhaka, Mumbai na Kolkata, ambako zaidi ya watu milioni 14 wako katika hatari ya kupoteza nyumba, maisha na vyanzo vyao vya kipato.
- Miji mikubwa ya pwani: Miami, New York na Guangzhou inakabiliwa na uwezekano wa hasara za matrilioni ya dola iwapo miundombinu yake itaathiriwa.
Je, ongezeko hilo linaweza kuzuiwa?
Si kikamilifu, kwa sababu ongezeko fulani tayari limejikita katika mfumo wa tabianchi.
Hata hivyo, kiasi gani cha ongezeko zaidi kitatokea kinategemea kiwango ambacho uzalishaji wa gesi hatari unaweza kupunguzwa sasa.
Jambo moja linalotia wasiwasi ni barafu ya Thwaites nchini Antarctica, yenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 190,000.
Kuporomoka kwake pekee kunaweza kusababisha ongezeko la ghafla na lisiloweza kurekebishwa la kina cha bahari la zaidi ya nusu mita hatua hatari ambayo inaweza kuwa vigumu sana kurejea nyuma.
Kukabiliana na hali ambayo haiwezi kuepukika
Kuondoka katika matumizi ya nishati ya kisukuku inayobadilisha tabianchi ni kipaumbele muhimu zaidi duniani katika kupunguza ongezeko la joto na hivyo kupunguza kasi ya kuongezeka kwa kina cha bahari. Lakini hatua za kukabiliana na athari hizo zinahitajika sasa.
Hatua hizo ni pamoja na:
- Mifumo ya tahadhari ya mapema ili kuwalinda watu kabla ya majanga kutokea.
- Kujenga kuta za bahari, kuhifadhi mikoko, kurejesha matuta ya mchanga na kuwahamisha kwa mpango watu kutoka maeneo yaliyo hatarini.
- Kuboresha data, kwa kuwa maeneo mengi bado hayana mifumo ya msingi ya kufuatilia hali ya bahari.
- Kuweka uwazi kuhusu masuala ya kisheria, yakiwemo hadhi ya nchi na mipaka ya baharini, iwapo ardhi itafunikwa na maji.
Nchi zinazoendelea zinahitaji wastani wa dola bilioni 310 hadi 365 kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini fedha za kukabiliana na hali hiyo duniani zilikuwa takriban dola bilioni 26 mwaka 2023.
Jambo la msingi
Vina vya bahari vinazoongezeka vinaweza kuonekana kama nguvu isiyoweza kuzuilika, lakini kiasi cha uharibifu kitakachotokea, na nani atakayeathirika zaidi, bado kinategemea maamuzi ambayo watu, jamii na Serikali zitafanya leo.
Hatimaye, kuongeza fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha kuwa ongezeko la kina cha bahari haliathiri hadhi ya nchi, na kulifanya suala hili kuwa kipaumbele cha kudumu na cha haraka duniani ndilo litakalohitajika ili kulinda nyumba, historia, maisha na utambulisho wa watu.