Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Nepal: Maiti za watu 538 wamepatikana, watu wengine 977 hawajulikani waliko

Makazi yaliyofunikwa na matope katika Wilaya ya Nuwakot, Nepal, huku majengo yaliyoharibika na mashine za uokoaji zikifanya kazi baada ya mafuriko ya ghafla mnamo tarehe 26 Agosti 2026.
© UNICEF/Laxmi-Prasad-Ngakhusi Majengo katika jimbo la Bagmati nchini Nepal, yamefunikwa na matope baada ya mafuriko makubwa.

Mafuriko Nepal: Maiti za watu 538 wamepatikana, watu wengine 977 hawajulikani waliko

Msaada wa Kibinadamu
  • Harakati za uokoaji zinaendelea- Familia nzima yaokolewa
  • Mfumo wa utoaji tahadhari mapema wafanya kazi
  • Milima yahitaji mifumo maalum ya tahadhari
  • WHO yatahadharisha kuhusu magonjwa
Picha ya Habari za UN yenye kichwa cha habari 'MAFUriko ya NEPAL FLASH' inayoonyesha ramani ya Nepal yenye wilaya zilizoathiriwa zaidi za Rasuwa, Nuwakot na Dhading zilizoangaziwa kwa rangi nyekundu kuzunguka katikati mwa Nepal, ikiwa ni pamoja na Gorkha, Sindhupalchok, Dolakha na Chitwan, huku Kathmandu ikiwa na alama.
Habari za UN/Lucica Matei Wilaya za Nepali zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo ni Rasuwa, Nuwakot na Dhading.

Wakati juhudi za utafutaji na uokoaji zikiendelea leo Ijumaa kufuatia mafuriko ya ghafla na maporomoko ya matope kwenye eneo la milimani kaskazini mwa Nepal, huko barani Asia, wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kutathmini ukubwa wa uharibifu, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mafuriko zaidi.

Umoja wa Mataifa ukinukuu takwimu za serikali ya Nepal umesema hadi sasa watu 538 wamekufa, 3,742 wameokolewa kufuatia tukio hilo, huku wengine 977 wakiwa hawajulikani waliko.

Mfanyakazi UNICEF aliyevaa shati la bluu anashirikiana na wanajeshi na wafanyakazi wakipakia mifuko nyeupe ya misaada kwenye lori katika eneo la kusimama uwanja wa ndege.
© UNICEF/Robic Upadhayay Vifaa vya msaada wa dharura vimeandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa jamii zilizoathiriwa na mafuriko nchini Nepal.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kutokea Kathmandu, mji mkuu wa Nepal, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Nepal, Lila Pieters Yahia, amesema kati ya watu ambao hawajulikani walipo, 517 wanaaminika kuwa raia wa kimataifa.

Familia yaokolewa 

Yahia amesema “Utafutaji na uokoaji ukiendelea tulishuhudia watu waliookolewa wakati tukitembelea eneo hilo muda mfupi uliopita tukiwa kwenye mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi. Tuliona lori zima lililojaa watu, familia nzima ambayo ilikuwa imetolewa kwenye eneo la hatari. Na ninaweza kuwaambia kwamba lilikuwa tukio la kugusa hisia sana.”

Amefafanua kuwa “malori yalitumika kuwahamisha watu waliokuwa wakiishi karibu na kingo za mito na kuwapeleka maeneo ya usalama.”

Mfumo wa tahadhari wafanya kazi

Amesema kazi yao ya kutathmini uharibifu ilizuiwa kwa muda baada ya mamlaka kupokea tahadhari ya uwezekano wa mafuriko mengine.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo Mkazi wa UN nchini Nepal, wakazi waliitikia haraka tahadhari hiyo na kutafuta maeneo salama.

Maafisa wa polisi wa Nepal waliovalia fulana za usalama za manjano na helmeti wanashughulikia vifaa vya afya vya dharura vya Shirika la Afya Duniani na masanduku ya vifaa vya kadibodi ndani ya hangari ya mizigo uwanja wa ndege.
© WHO Jamii katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko nchini Nepal sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa huku familia zikikabiliwa na hasara, kuhama makazi na kukatizwa kwa huduma muhimu baada ya mafuriko makubwa.

Uharibifu mkubwa

Kamal Kishore, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kupunguza Hatari za Majanga, akizungumza kwenye mkutano huo Geneva, amesema tukio hilo ni miongoni mwa matukio makubwa ya hatari za milimani kuwahi kushuhudiwa katika kumbukumbu za kizazi cha sasa.

Amesema madhara yameenea katika maisha ya watu, shughuli za kujipatia kipato, majengo, miundombinu, madaraja, miradi ya umeme wa maji na uzalishaji wa nishati.

“Bado kuna umuhimu wa kutathmini kikamilifu ukubwa wa uharibifu,” amesema Kishore.

Takribani watu 93,000 waathirika

David Fisher, Mkuu wa Ujumbe wa Nepal wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), amesema makadirio ya awali yanaonesha takribani watu 93,000 wameathirika na wanahitaji msaada mkubwa na kwamba “mashirika ya misaada yana wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mafuriko ya pili.”

WHO yaonya kuhusu magonjwa

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa majanga makubwa kama haya yanaweza kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.

Msemaji wa WHO, Tarik Jašarević, amesema uhamishaji wa watu, msongamano katika maeneo ya hifadhi ya muda na kukatika kwa huduma za maji, usafi wa mazingira na afya vinaweza kuongeza hatari hiyo.

Milima yahitaji mifumo maalumu ya tahadhari

Akimulika hatari za kuishi milimani, Kishore amesema tukio hilo limeonesha kwa mara nyingine udhaifu wa mifumo ya ikolojia ya milimani na changamoto za kuanzisha mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema.

“Katika maeneo ya milimani si rahisi kutabiri hatari moja pekee, kwa kuwa janga moja linaweza kuchochea mfululizo wa majanga mengine. Jambo muhimu zaidi ni mshikamano na watu wa Nepal wakati shughuli za uokoaji na misaada zikiendelea,” amesema.