Guterres aomba dola bilioni 1.1 kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini DRC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa dharura kwa jumuiya ya kimataifa kuchangia dola bilioni 1.1 zinazohitajika kukamilisha ufadhili wa mpango wa kukabiliana na Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani, amesema fedha hizo zitawezesha kupanua huduma za afya, ufuatiliaji wa ugonjwa, usafirishaji wa vifaa, ushirikishwaji wa jamii, kuajiri wafanyakazi wa dharura na kutoa misaada ya kibinadamu.
Guterres amesema “Jamii zilizoathirika zinastahili msaada mkubwa zaidi. Na hatua za kukabiliana na mlipuko huu zinastahili kuungwa mkono zaidi.”
Mlipuko unaongezeka kwa kasi
Katibu Mkuu ameonya kuwa huu ndio mlipuko wa Ebola unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kurekodiwa duniani na mkubwa zaidi katika historia ya DRC.
Hadi kufikia tarehe 24 Agosti, watu 5,656 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa na wengine 2,715 wamefariki dunia. Takribani wagonjwa wapya 500 wanaripotiwa kila wiki, huku wanawake na watoto wakiathirika zaidi.
“Tunajua jinsi ya kudhibiti Ebola, kukatiza maambukizi na kuokoa maisha. Lakini lazima pia tushinde virusi vingine, virusi vya kutojali,” amesema.
Hali ni ngumu zaidi kutokana na migogoro, mifumo dhaifu ya afya na ugumu wa kufikia baadhi ya jamii. Zaidi ya watu milioni 12 katika eneo hilo wanahitaji msaada na ulinzi wa kibinadamu.
Zaidi ya wahudumu 40 wa afya wamefariki wakijaribu kuokoa wengine, huku vituo vya matibabu na magari ya wagonjwa yakishambuliwa.
Umoja wa Mataifa umefanya nini?
Serikali ya DRC inaongoza juhudi za kudhibiti mlipuko huo, ikisaidiwa na Umoja wa Mataifa chini ya uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, pamoja na wadau wengine.
Umoja wa Mataifa umeteua Mratibu Mwandamizi wa Ebola na kuelekeza juhudi katika vipaumbele vitano: kuimarisha ushirikishwaji wa jamii, ufuatiliaji wa maambukizi, matibabu, maziko salama, na kuzuia ugonjwa kusambaa zaidi.
Maandalizi pia yanaimarishwa nchini Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC, kikihamasisha wataalamu na ushirikiano wa kikanda.
Fedha zilizopo zitaisha baada ya wiki chache
Hadi sasa, zaidi ya dola milioni 80 zimetolewa kupitia mifuko ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na msaada wa wadau. Hata hivyo, mpango wa mahitaji na mwitikio wa kibinadamu wa dola bilioni 2.13 umefadhiliwa kwa asilimia 48 pekee.
Guterres ameonya kuwa fedha zilizopo zitatosha kwa wiki chache, si miezi, na shughuli muhimu zinaweza kusimama wakati zinapohitajika kupanuliwa.
“Dunia ina maarifa, uwezo na rasilimali za kuzuia mlipuko huu. Ni wakati wa kuonesha dhamira ya pamoja na kuchukua hatua kabla gharama haijawa kubwa zaidi, utekelezaji kuwa mgumu zaidi na watu wengi zaidi kupoteza maisha,” amehitimisha.