Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshtuko na uharibifu mkubwa waendelea, siku moja baada ya mafuriko Himalaya

Mwonekano wa angani wa makazi yaliyofunikwa na matope katika Wilaya ya Rasuwa, katikati mwa kaskazini mwa Nepal, yenye majengo yaliyoharibika kando ya mto uliojaa matope baada ya mafuriko ya ghafla.
© UNICEF Makazi katika wilaya ya Rasuwa katikati ya kaskazini mwa Nepal yangali yamezama kwenye matope kufuatia mafuriko makubwa ya ghafla.

Mshtuko na uharibifu mkubwa waendelea, siku moja baada ya mafuriko Himalaya

Tabianchi na mazingira
  • Mamia ya watu bado hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa nchini Nepal na China
  • Dola milioni 2 zimetolewa kutoka Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa
  • Shirika la Afya Duniani (WHO) latuma dawa, vifaa na mahema
Wakati taarifa zikieleza kuwa mamia ya watu bado hawajulikani walipo nchini Nepal na China baada ya mafuriko makubwa ya ghafla kuvamia miji na vijiji siku ya Jumatano, timu za misaada zimekuwa zikifanya juhudi kuwafikia wananchi waliotengwa na maafa hayo.
Dola milioni 2 za Marekani za awali zimetolewa kutoka Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa wa CERF kwa ajili ya “kuokoa maisha kupitia huduma za dharura za afya, makazi na maji”, Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesema kwenye mtandao wa X.
Nchini Nepal, mahitaji ya haraka ya kibinadamu ni makubwa katika wilaya za Rasuwa, Nuwakot na Dhading, huku jamii zikikabiliwa na changamoto kubwa wakati familia zikikabiliana na vifo, kuhama makazi na kuvurugika kwa huduma muhimu.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameahidi msaada wa haraka.
“Umoja wa Mataifa unahamasisha vifaa na timu za huduma za kibinadamu, na tunaahidi kuunga mkono juhudi za kitaifa katika kutoa msaada wa dharura na usaidizi,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.

Watoto 17,000 wameathirika

Mafuriko ya ghafla yamechukua au kutenga jamii nzima, huku barabara, madaraja, miundombinu ya kuzalisha umeme wa maji, mifumo ya maji na mitandao ya mawasiliano ikiwa imeharibiwa vibaya. Hali hiyo imeacha maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa bila kufikika na imekwamisha utoaji wa misaada ya kuokoa maisha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilisema leo Alhamisi.
Takribani watoto 17,000 wameathiriwa na mafuriko hayo makubwa ya ghafla yaliyokumba wilaya za Rasuwa, Nuwakot na Dhading nchini Nepal.
“Watoto kote Rasuwa na Dhading waliona maisha yao yakisombwa na maji mbele ya macho yao ndani ya muda mfupi sana, huku nyumba, madarasa na vituo vya afya vikiharibiwa,” amesema Alice Akunga, Mwakilishi wa UNICEF nchini Nepal.
“Wengi sana wamepoteza maisha na wapendwa wao. Huku idadi ya waliofariki dunia ikiendelea kuongezeka, tunajua kwamba janga hili bado halijaisha. Watoto walionusurika mafuriko sasa wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya magonjwa, utapiamlo, ukatili na unyonyaji.”
Kwa upande wake, UNICEF iko katika maeneo yaliyoathirika na inaongeza msaada wake, “lakini tunahitaji haraka rasilimali zaidi ili kumfikia kila mtoto anayehitaji msaada,” Bi. Akunga alisema.

Bado hawajulikani walipo

“Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametumwa katika maeneo yaliyoathirika yakiwa na chakula, vifaa vya matibabu na vifaa vya misaada ili kuunga mkono mwitikio unaoongozwa na serikali, na yako tayari kufanya zaidi,” Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Nepal imeandika kwenye mtandao wake wa Facebook.
Nchini China, takribani watu 560 bado hawajulikani walipo, kwa mujibu wa mamlaka. Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo iliripoti jana Jumatano kuhusu uharibifu na idadi kubwa ya watu waliofariki dunia pamoja na uharibifu katika eneo linalojiendesha la Tibet nchini China.
Wakati huo huo, katika kuunga mkono mamlaka na juhudi kubwa za kukabiliana na janga hilo, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) limetuma kifurushi cha dharura cha afya cha mashirika mbalimbali, chenye dawa na vifaa vinavyotosheleza kutoa huduma za msingi za afya kwa hadi watu 10,000.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limetoa mahema sita yenye matumizi mbalimbali ili kusaidia kuendeleza utoaji wa huduma za afya katika jamii zilizoathirika.
“Vifaa hivi vinalenga kuwaunga mkono wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wanapoendelea kutoa huduma muhimu na kukabiliana na mahitaji ya haraka ya kiafya ya watu walioathirika,” WHO ilieleza kwenye mtandao wa Facebook.
Mwonekano wa angani wa majengo na vifusi vilivyofunikwa na matope katika makazi katika Wilaya ya Rasuwa, katikati mwa kaskazini mwa Nepal, kufuatia mafuriko ya ghafla yaliyoharibu nyumba na miundombinu.
© UNICEF Majengo yamezama kwenye matope kufuatia mafuriko ya ghafla katika wilaya ya Rasuwa katikati mwa kaskazini mwa Nepal.

Timu mpya za msaada zatumwa

“WHO itaendelea kujitolea kufanya kazi kwa karibu na mamlaka za afya na washirika ili kutathmini hali inavyoendelea, kuunga mkono huduma za afya za dharura na kusaidia kuhakikisha kwamba watu wanaendelea kupata huduma wanazohitaji katika kipindi hiki kigumu.”
Aidha, Alhamisi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na UNICEF zimepanga kuanza kutuma wafanyakazi pamoja na malori yaliyobeba vifaa vya misaada.
Juhudi pia ziliendelea kwa ajili ya kutathmini kwa haraka ukubwa wa maafa hayo, hasa kupitia picha za satelaiti salama na uchambuzi wa maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko. Taarifa hizo zilitolewa kupitia jukwaa la Umoja wa Mataifa la UN-SPIDER, linalohusika na matumizi ya taarifa za anga katika usimamizi wa maafa na mwitikio wa dharura.
Mpango huo, unaosimamiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga za Juu (UNOOSA), unaunganisha wataalamu wa usimamizi wa maafa na mashirika ya anga ili kusaidia shughuli za kupunguza hatari za maafa, kutoa tahadhari za mapema na kukabiliana na dharura.

Barafu toka mlimani yawajibika

Kuanguka kwa barafu kubwa ya mlimani katika maeneo ya juu yenye mabonde yenye miteremko mikali ya Himalaya kumetajwa kuwa huenda ndiyo chanzo cha mafuriko hayo ya ghafla na maporomoko ya matope yaliyoharibu jamii nzima na kusomba madaraja na barabara.
Wilaya ya Rasuwa, iliyoko takribani kilomita 80 kaskazini mwa Kathmandu, kaskazini mwa Nepal, imeathirika pakubwa, ikiwemo miji ya Timure, Rasuwagadhi na Syabrubesi. Syabrubesi ni eneo maarufu la utalii kwa watalii, wapanda milima na mahujaji wanaotaka kufikia bonde la Langtang.
Eneo hilo pia lilikumbwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa vipimo vya Richter 7.8 mwezi Aprili 2015, ambalo liliua zaidi ya watu 8,800. Oktoba mwaka jana, mvua kubwa zilisababisha mafuriko ya kasi na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya mashariki na katikati mwa Nepal, na kuathiri zaidi ya watu 30,000.

Hatari ya maafa yazidi kuongezeka

UNDRR, shirika kuu la Umoja wa Mataifa linaloratibu juhudi za kupunguza hatari za maafa, linakadiria kuwa dunia itakumbwa na wastani wa maafa 560 ya ukubwa wa kati hadi mkubwa kila mwaka ifikapo 2030.
“Maafa duniani yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 40 kati ya mwaka 2015 na 2030, yakichochewa na mabadiliko ya tabianchi na makadirio duni ya hatari za kimfumo,” shirika hilo limesema.
Mbali na gharama kwa maisha ya binadamu, gharama ya kila mwaka ya maafa hayo ni dola trilioni 2.29 za Marekani na inaendelea kuongezeka, wakati athari zisizo za moja kwa moja pamoja na zile kwa mifumo ya ikolojia zinapozingatiwa, UNDRR ilisema.
Kiasi hicho ni karibu mara 10 ya hasara za moja kwa moja za kila mwaka zinazoripotiwa katika takwimu rasmi.