Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kulinda Ziwa Albert ni jukumu letu sote: Wavuvi Uganda

Nyavu za kuvulia samaki za rangi ya chungwa zenye maboya ya bluu na kijani yaliyotawanywa kwenye ufuo wa ziwa wenye mchanga nchini Uganda karibu na Ziwa Albert, huku wanaume wakitengeneza boti za mbao nyuma.
UN News Nyavu za kuvulia samaki kwenye ufukwe wa Nkondo, Ziwa Albert, wilayani Kikuube, Uganda.

Kulinda Ziwa Albert ni jukumu letu sote: Wavuvi Uganda

Tabianchi na mazingira

Kwenye ufukwe wa Nkondo, wilayani Kikuube nchini Uganda, maisha yanaanza mapema. Wavuvi huingia ziwani kutafuta samaki, huku familia zinazozunguka Ziwa Albert zikitegemea maji yake kwa chakula, kipato na maisha ya kila siku.

Lakini nyuma ya shughuli hizo za kila siku kuna tishio linalozidi kuonekana, taka za plastiki na uchafu mwingine unaoingia Ziwa Albert.
 
Kwa maelfu ya watu wanaoishi kando ya ziwa hilo, Ziwa Albert si tu chanzo cha samaki. Ni sehemu ya maisha yao, historia yao na uchumi wa familia zao. Sasa, viongozi wa jamii ya wavuvi wanaonya kuwa bila hatua za haraka, uchafuzi unaweza kuhatarisha mazalia ya samaki na maisha ya vizazi vijavyo.
 
Mwanamume Mwafrika aliyevaa shati jepesi na miwani ya mviringo anazungumza nje karibu na Ziwa Albert, Uganda, akiwa na ua wa kijani uliopambwa vizuri na jengo nyuma.
UN News Solomon Wamara Mwenyekiti wa Chama Cha Wavuvi kwenye Ziwa Albert nchini Uganda.
Katika maadhimisho ya Siku ya Ziwa Duniani, ambayo kila mwaka huwa 27 Agosti Mwenyekiti wa Wavuvi wa Ziwa Albert nchini Uganda, Solomon Wamara, amesema jamii haiwezi kuendelea kulitazama ziwa kama chanzo cha riziki huku ikiliruhusu kujazwa taka.
 
“Tunafurahia maadhimisho ya Siku ya Ziwa Duniani. Ni wakati mzuri wa kuangazia vitisho vinavyolikabili ziwa hili ambalo ni maisha yetu,” amesema Wamara.

Plastiki zatishia mazalia ya samaki

Kwa Wamara, tatizo la taka za plastiki si suala la usafi pekee. Ni suala linalogusa moja kwa moja mustakabali wa uvuvi na uhakika wa chakula.
 
Amesema mifuko ya plastiki na taka nyingine zinapotupwa ovyo, hatimaye huishia kwenye ziwa ambako zinaweza kuathiri maeneo ambayo samaki huzalia na kukulia.
Tatizo hilo linaongezwa na changamoto nyingine, ikiwemo uvuvi haramu, ambao unaweza kupunguza idadi ya samaki na kuvuruga mzunguko wa kuzaliana kwa viumbe wa majini.

Lakini uchafuzi hauishii kwenye ufukwe wa ziwa.

Wamara ametaja mito ya Wambabya, Waki na Nguse kuwa miongoni mwa njia ambazo uchafu kutoka maeneo ya nchi kavu unaweza kusafirishwa hadi Ziwa Albert.
Shughuli za kilimo, pamoja na utupaji taka ovyo, ni baadhi ya mambo yanayochangia uchafuzi huo.
 
“Uchafuzi wa mito unaathiri mazalia ya samaki na pia uhakika wa chakula. Mito hii ni muhimu kwa maisha ya samaki na jamii zinazotegemea ziwa,” amesema “ziwa ni maisha yetu”

Jamii ina wajibu mkubwa

Wito wa Wamara ni rahisi lakini wenye uzito, jamii ibadilishe namna inavyolitunza ziwa.
 
Anazitaka jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Albert kuacha kutupa taka ovyo, hasa plastiki, na kushiriki zaidi katika shughuli za usafi wa mazingira.
 
Ameunga mkono kampeni za usafi zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, akisema juhudi hizo zinapaswa kupanuliwa na kuhusisha jamii nyingi zaidi.
“Ziwa ni maisha yetu. Tukilinda ziwa, tunalinda maisha yetu na maisha ya vizazi vijavyo,” amesema.
 
Lakini kwa Wamara, uhifadhi wa ziwa haupaswi kutenganishwa na maisha ya watu wanaolitegemea ziwa hilo.
 
Anasema hatua dhidi ya uvuvi haramu ni muhimu, lakini serikali inapaswa pia kuzingatia hali ya wavuvi wa jadi ambao wameishi kwa kutegemea ziwa kwa vizazi.
 
Akizungumzia tozo zinazotozwa kwa wavuvi, Wamara amesema baadhi ya wavuvi 
wa kawaida wanakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi.
 
“Kwa mfanyabiashara inawezekana kulipa kodi. Lakini kumtoza kodi mtu aliyezaliwa kando ya ziwa, akakulia katika uvuvi na anautumia kupata chakula na fedha za mahitaji ya msingi kama sabuni, si jambo rahisi,” amesema.
 
Kwa maoni yake, suluhisho si kuwaondoa wavuvi kwenye ziwa, bali kuwawezesha kuendelea kuvua kwa njia endelevu, kufuata sheria na kulinda rasilimali zinazowategemeza.

Serikali: Ziwa Albert ni rasilimali ya wote

Serikali ya Uganda inasema inatambua umuhimu wa Ziwa Albert na maziwa mengine kwa maisha ya wananchi.
 
Godwin Angalia, Kamishna wa Wilaya ya Kikuube, ambaye pia anatoka katika jamii ya wavuvi na aliwahi kuwa mvuvi, amesema serikali inayaona maziwa kama nguzo muhimu ya maisha na uchumi wa wananchi.
Mwanamume aliyevaa suti ya kijivu na shati la bluu ameketi kwenye sofa ya ngozi ya kahawia, akiashiria kwa mikono yake huku akiwa amevaa kipaza sauti cha begi.
UN News Godwin Angalia, Kamishna wa Wilaya ya Kikuube nchini Uganda
“Kama serikali, tunathamini maziwa kwa sababu yanawezesha maisha ya mamilioni ya wananchi. Pia yanatoa rasilimali mbalimbali zinazosaidia jamii,” amesema Angalia.
 
Hata hivyo, amesema Ziwa Albert linakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo uchafuzi wa mazingira na uvuvi haramu.
 
Kwa mujibu wa Angalia, serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na uchafuzi unaotokana na shughuli za binadamu, huku ikilenga pia kulinda vyanzo vya maji vinavyolisha ziwa.
 
“Bila shaka mito kama Nguse na Wambabya imechafuliwa. Pia msitu wa Bugoma ni muhimu sana kwa uhai wa Ziwa Albert na viumbe vilivyomo,” amesema.
 
Angalia amesema juhudi zinaendelea kulinda Msitu wa Bugoma na mito inayomwaga maji yake katika Ziwa Albert dhidi ya uharibifu na uchafuzi.
 
Pia amewataka viongozi wa vijiji kuwa macho na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu watu wanaochafua mazingira au kuharibu rasilimali za ziwa.
Kundi la watu waliovaa fulana za kuokoa maisha za rangi ya chungwa wakifanya kazi kwenye mashua ya mbao kwenye ufuo wa mchanga nchini Uganda. Mwanamke aliyevaa gauni jekundu amesimama karibu huku wanaume wakishughulikia mbao na vifaa karibu na Ziwa Albert.
UN News Wavuvi kwenye ufukwe wa Nkondo, Ziwa Albert, wilayani Kikuube nchini Uganda.

Wavuvi washirikishwe katika ulinzi wa ziwa

Mbali na hatua za serikali, Angalia amesema jamii yenyewe inapaswa kuwa sehemu ya suluhisho.
 
Serikali imeanza kuunda kamati za jamii za asili zitakazosaidia katika usimamizi wa uvuvi katika maeneo yao.
 
Kwa Angalia, ushiriki wa wavuvi ni muhimu kwa sababu wao wanafahamu zaidi mazingira ya ziwa na wanaelewa namna ambavyo rasilimali zake zinaweza kutumiwa bila kuzimaliza.
 
“Wavuvi wenyewe tunajua kuwa hatupaswi kuvua samaki wachanga. Hatuli samaki wachanga, na tunajua hilo. Tunatumia mbinu za asili na rafiki kwa mazingira katika uvuvi,” amesema.
 
Kauli hiyo inaweka wavuvi katikati ya mjadala wa uhifadhi, si kama sehemu ya tatizo pekee, bali pia kama walinzi muhimu wa rasilimali wanayoitegemea.

Mustakabali wa ziwa uko mikononi mwa wote

Kwa muda mrefu, Ziwa Albert limekuwa tegemeo la jamii zinazolizunguka, likitoa samaki, maji, ajira na kipato.
 
Lakini kadiri shughuli za binadamu zinavyoongezeka, shinikizo kwa mfumo wa ikolojia wa ziwa linaongezeka pia. Uchafuzi wa mito, taka za plastiki na uvuvi usio endelevu vinaweza kuhatarisha sio tu samaki, bali pia maisha ya watu wanaotegemea ziwa.
 
Siku ya Ziwa Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Agosti, inalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa maziwa na kuhamasisha hatua za kuyahifadhi dhidi ya uchafuzi na vitisho vingine.
 
Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa kuna zaidi ya maziwa milioni 117 duniani, yakichukua takribani asilimia nne ya eneo la ardhi ya dunia. Umoja wa Mataifa pia umeonya kuhusu kupungua kwa viumbe wa maji baridi kutokana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika miongo ya hivi karibuni.
 
Kwa wakazi wanaozunguka Ziwa Albert, ujumbe kutoka kwa wavuvi na viongozi wao ni wazi, ziwa haliwezi kulindwa na serikali pekee.
 
Kila mfuko wa plastiki unaotupwa hovyo, kila taka inayosafirishwa na mto, na kila samaki anayevuliwa kabla hajakomaa ni sehemu ya changamoto kubwa zaidi.
 
Na kama anavyosema Wamara “Ziwa ni maisha yetu.”
Kulilinda, basi, ni kulinda chakula, kipato na maisha ya jamii inayolizunguka leo na kwa vizazi vijavyo.