Baraza la Usalama: Mvutano waongezeka Gaza na Ukingo wa Magharibi hatua zahitajika
Huku kukiwa na ongezeko la makazi haramu ya walowezi wa Israel, mashambulizi yakiendelea Gaza na Ukingo wa Magharibi pamoja na mvutano katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kusikiliza taarifa kuhusu maendeleo ya hivi karibuni.
Mambo muhimu ya kufahamu
- Gaza, watu wengi bado wamekimbia makazi yao ndani ya eneo hilo, wakiishi katika mazingira magumu na kukabiliwa na mashambulizi ya kijeshi ya Israel yanayoendelea kusababisha vifo. Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, asilimia 90 ya wakazi walikabiliwa na ukosefu wa usalama wa maji wa kiwango cha kati hadi cha juu mwezi Julai.
- Katika Ukingo wa Magharibi, operesheni za Israel ziliwaumiza zaidi ya Wapalestina 50 na kubomoa miundo 25 inayomilikiwa na Wapalestina, huku mashambulizi 38 ya walowezi wa Israel yakiripotiwa ndani ya wiki moja pekee, yakisababisha vifo na majeraha, uharibifu wa mali au yote mawili.
- Mamlaka za Israel zimechukua mali ya shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, katika Ukingo wa Magharibi.
Miongoni mwa watoa taarifa katika kikao hicho cha leo ni pamoja na Bwana. Ramiz Alakbarov, Naibu Mratibu Maalum na Mratibu Mkazi katika Ofisi ya Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, Bwana Nickolay Mladenov, Mwakilishi Mkuu wa Baraza la Amani la Gaza, pamoja na mwakilishi wa mashirika ya kiraia.
Alakbarov : Ongezeko la hali ya sintofahamu
Mjumbe Maalum afafanua kuongezeka kwa sintofahamu, kuzidi kwa mvutano katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu. Ameliambia Baraza la Usalama kwamba “Wakati mazungumzo yakiendelea kuhusu utekelezaji wa azimio nambari 2803 (2025) na Mpango Kamili wa Kukomesha Mzozo wa Gaza, usitishaji wa mapigano bado ni dhaifu,” amesema Kaimu Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, Ramiz Alakbarov.
Amesema mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanaendelea na kwamba hali katika Ukingo wa Magharibi “inaendelea kuzorota kwa kasi.”
Utekelezaji kamili wa Ramani ya mwelekeo yenye vipengele 15 ungeendeleza mipango ya mpito iliyoainishwa katika Mpango huo. Mipango hiyo inajumuisha kuwapokonya silaha Hamas na makundi mengine yote yenye silaha, kuondolewa kwa Jeshi la Ulinzi la Israel kutoka Gaza, kupelekwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kuweka Utulivu, pamoja na kukabidhi majukumu ya utawala wa mpito kwa Kamati ya Kitaifa ya Utawala wa Gaza.
“Natoa wito kwa pande zote kujenga juu ya kasi hii, kutimiza ahadi zao na kuendeleza Ramani ya Barabara kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema.
Jambo lingine la msingi ni kushughulikia hali mbaya inayowakabili wananchi wa Gaza. “Wanapoteza matumaini,” amesema.
Mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yalianza tena tarehe 12 Agosti baada ya utulivu wa wiki moja, huku shughuli za kijeshi, zikiwemo mashambulizi ya mabomu, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na operesheni za ardhini, zikiendelea bila kusimama. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, katika kipindi cha taarifa zaidi ya Wapalestina 100 waliuawa na zaidi ya 400 walijeruhiwa.
Takribani theluthi mbili ya Gaza bado hazifikiki au zinakabiliwa na vikwazo vikali vya upatikanaji, huku Rufaa ya Dharura ya 2026 ya misaada ya kibinadamu ikiwa imepata ufadhili wa asilimia 40 pekee.
“Zaidi ya miezi 10 tangu kuanza kwa usitishaji wa mapigano, hali hii haikubaliki,” amesema. Vikwazo muhimu vya kiutendaji vinapaswa kushughulikiwa na “heshima ya utu wa binadamu lazima iwe kiini cha juhudi zote.”
Mashambulizi makubwa ya Walowezi
Katika Ukingo wa Magharibi, amesema mashambulizi makubwa ya walowezi yanaendelea “bila kuwapo kwa uwajibikaji wa maana kwa uhalifu huu.”
Tarehe 18 Agosti, mamlaka za Israel zilifungua zabuni kwa ajili ya ujenzi wa zaidi ya nyumba 1,200 zinazochukuliwa kuwa haramu katika eneo la E1, mashariki mwa Jerusalem.
“Iwapo mpango wa E1 utatekelezwa, kwa ufanisi utatenganisha maeneo ya kaskazini na kusini ya Ukingo wa Magharibi pamoja na uhusiano wake na Jerusalem Mashariki, na kudhoofisha matarajio ya kuanzishwa kwa Dola ya Palestina inayoweza kufanya kazi,” amesema.
Jana Jumanne, mamlaka za Israel ziliingia kwa nguvu na kuchukua kinyume cha sheria Kituo cha Mafunzo cha Kalandia cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) huko Jerusalem Mashariki.
“Ninarudia wito wangu kwa Israel kutenda kwa mujibu wa wajibu wake chini ya sheria za kimataifa. Juhudi zote za kutwaa, kudhibiti au kunyang’anya mali za vituo vya UNRWA lazima zikomeshwe,” amesema.
Utekelezaji wa Ramani ya vipengele 15