Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yaeleza mikakati ya kukabili ukame na uharibifu wa ardhi

Mbeba mizigo akiwa amebeba mzigo mkubwa wa kijani kibichi na kontena akitembea kwenye njia nyuma ya kundi la wapanda milima wanaopanda Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania.
© Unsplash/Tom Cleary Zaidi ya 50% ya eneo lote la Tanzania linapitia uharibifu wa ardhi kwa kasi.

Tanzania yaeleza mikakati ya kukabili ukame na uharibifu wa ardhi

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 17 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, UNCCD COP17, ukiendelea Ulaanbaatar, Mongolia, Tanzania imeeleza mikakati yake ya kukabiliana na ukame, mmomonyoko wa udongo na kupungua kwa rutuba ya ardhi.

Mkutano huo, unaofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 28 Agosti, umewakutanisha wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia na wadau wengine kujadili hatua za kulinda ardhi na kuimarisha maisha ya jamii zinazoathiriwa na ukame.

Akizungumza na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Timotheo Mande, ambaye ni Afisa kiungo cha Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa UNCCD, amesema maeneo kadhaa nchini yameathiriwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

Ametaja mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Simiyu na Geita, pamoja na baadhi ya maeneo ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Tanzania imejipanga vipi?

Kwa mujibu wa Mande, Tanzania imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ukame utakaotekelezwa hadi mwaka 2032, pamoja na kufanya mapitio ya programu yake ya kupambana na kuenea kwa jangwa na ukame.

Amesema Mpango wa Mageuzi ya Kijani pia unalenga kuongeza juhudi za kurejesha mazingira, ikiwemo kupanda miti bilioni mbili kila mwaka.

“Tuna utashi wa kisiasa. Serikali inakubali kwamba tuna tatizo na inajitoa mstari wa mbele kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi,” amesema.

Mande ameongeza kuwa Tanzania inatarajia maamuzi ya COP17 yatasaidia kukabili changamoto za nyanda za malisho. Uhaba wa malisho, amesema, huacha ardhi wazi na kuongeza mmomonyoko unaoondoa tabaka la juu la udongo, hivyo kupunguza rutuba na mazao ya wakulima.

Wafanyakazi wa FAO nchini Tanzania wakionyesha matibabu ya maji ya moto kwa mimea ya ndizi kwa kikundi cha wakulima wa eneo hilo huko Pemba.
FAO Tanzania Ili kuepuka kusambaza magonjwa, baadhi ya mizizi ya migomba huondolewa, kisha mgomba hutumbukizwa kwenye maji ya moto na ndipo unapandwa kwenye shimo lengo likiwa ni kuua wadudu waharibifu wa mimea. ( Maktaba)

Usawa kijinsia uzingatiwe katika kila hatua

Sara Samwel Pima, mwakilishi wa asasi za kiraia anayeshughulikia masuala ya jinsia barani Afrika, amesema juhudi za kulinda ardhi haziwezi kutenganishwa na ushiriki wa wanawake, vijana na makundi maalumu.

Amesisitiza kuwa makundi hayo lazima yafikiwe na fedha zinazotolewa kwa ajili ya ardhi, maji na uhifadhi wa bayoanuai.

Pima amesema ukame na ukosefu wa maji vinaongeza njaa na umaskini, hivyo fedha na suluhisho zinazokubaliwa katika mikutano ya kimataifa zinapaswa kuzifikia kwa wakati jamii zilizoathiriwa zaidi.