Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: WHO yatoa wito wa kusitishwa mapigano kwa miezi sita ili kukomesha mlipuko wa Ebola

Mfanyakazi wa afya anaandika 'Dk. Moise' mgongoni mwa mtu mwingine aliyevaa PPE nyeupe katika kliniki.
© UNOCHA/Ramatoulaye Moussa Maz Daktari anayewatibu wagonjwa wa Ebola mashariki mwa Congo ameandikwa jina lake mgongoni kwa madhumuni ya utambuzi.

DRC: WHO yatoa wito wa kusitishwa mapigano kwa miezi sita ili kukomesha mlipuko wa Ebola

Afya

Wakati mlipuko wa Ebola ukiendelea kuenea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu kwa angalau miezi sita, ili kuwezesha timu za afya kuwafikia watu walio katika hatari na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya Ebola.

Huko Addis Ababa Ethiopia, kauli ya Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WHO imekuwa wazi: zana za kukabiliana na Ebola zipo, lakini baadhi ya watu walioathirika bado hawafikiwi na timu za afya.
“Changamoto iliyopo leo si ukosefu wa maarifa au zana,” amesema Dkt. Mohamed Yakub Janabi wakati wa ufunguzi wa kikao cha 76 cha WHO Kamati ya Kanda ya Afrika.
Kwa mujibu wa shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa, kuwafikia jamii sasa ndiyo kikwazo kikuu katika kukabiliana na mlipuko huo. Kwa hiyo, WHO imezitaka pande zote kuhakikisha kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu kwa angalau miezi sita, ili timu za afya ziweze kuingilia kati “kwa usalama na bila vikwazo katika jamii zilizoathirika.”
“Tunapoweza kuwafikia watu, tunazuia maambukizi. Tunaposhindwa kuwafikia, virusi vinaendelea kuenea,” amesisitiza Dkt. Janabi.
WHO inahusisha kuongezeka kwa hali hiyo na ukosefu wa usalama unaoendelea, ambao umetokana na miongo kadhaa ya migogoro ya silaha iliyodhoofisha utawala wa sheria na huduma za kijamii na kusababisha zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao.
Wafanyakazi wa afya wakiwa wamevaa mavazi kamili ya kujikinga wakijiandaa kwa kampeni ya chanjo ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
©WHO/Grainne Harrington Wafanyakazi wa afya wakiwa wamevaa mavazi kamili ya kujikinga wakijiandaa kwa kampeni ya chanjo ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kuongeza uwezo wa hatua mara mbili au tatu

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni hadi Agosti 21, 2026, DRC ilikuwa imeripoti wagonjwa 5,514 waliothibitishwa na vifo 2,642 katika maeneo 57 ya afya.
Mlipuko huo sasa unachukuliwa kuwa wa pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa na unaoenea kwa kasi zaidi.
Siku moja kabla, Dkt. Janabi alikuwa ametaja hali hiyo kuwa “mageuzi muhimu”, akisema maambukizi sasa yanaendelea kwa kasi kuliko juhudi za kuyadhibiti.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa mwitikio wanataka hatua zichukuliwe kwa kiwango kikubwa zaidi.
Katika taarifa ya pamoja, Dkt. Janabi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, na Mkurugenzi Mtendaji wa Africa wa kituo cha kudhibito magonjwa CDC Dkt. Jean Kaseya, wametoa wito wa kufikiwa kwa kila eneo lililoathirika, kulindwa kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele na ahadi kutafsiriwa kuwa hatua za vitendo.
“Juhudi hizi bado zinahitaji kuongezwa. Tunahitaji kuongeza mara mbili au tatu uwezo wa sasa wa mwitikio katika maeneo yake yote,” wamesema.
Wapiganaji wa zamani huko Ituri, DR Congo, wakiwa wamevaa fulana nyeupe zenye nembo za Ebola, wanaongoza kampeni ya uhamasishaji umma dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Ebola kwa usaidizi kutoka MONUSCO.
© MONUSCO Waasi wa zamani nchini DR Congo sasa wanaunga mkono uhamasishaji wa kuzuia Ebola katika jamii zao.

Wahudumu wa afya nao wako hatarini

Kulinda wahudumu wa afya pia kumekuwa kipaumbele cha dharura. Hadi Agosti 20, wahudumu wa afya 158 walikuwa wameambukizwa na 45 wamefariki dunia.
Katika maeneo yaliyoathirika au yaliyo katika hatari kubwa, vituo vya afya vinahitaji kuwa na wafanyakazi waliofunzwa, vifaa vya kujikinga, maji safi na mifumo madhubuti ya kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Kwa WHO na Afrika CDC, kipaumbele kinaendelea kuwa kutambua kila mgonjwa, kuwafuatilia watu wote waliokutana naye na kuvunja kila mlolongo wa maambukizi, huku ikiimarisha uratibu wa kuvuka mipaka na msaada wa kimataifa ili “hakuna jamii itakayoachwa nyuma.”

WHO yataka DRC kuimarisha hatua

Malengo hayo sasa yamegeuzwa kuwa mapendekezo kadhaa yenye lengo la kuimarisha mwitikio na kupunguza hatari ya mlipuko huo kuenea nje ya maeneo yaliyoathirika.
Baada ya kikao cha kamati yake ya dharura wiki iliyopita, WHO ilichapisha Jana Jumatatu mapendekezo ya Mkurugenzi Mkuu.
Shirika hilo limeitaka serikali ya DRC kuimarisha mfumo mzima wa mwitikio, kuanzia ufuatiliaji, usimamizi wa wagonjwa na uhamasishaji wa jamii hadi ufuatiliaji wa mienendo na mikusanyiko ya watu pamoja na ulinzi wa wahudumu wa afya.
Bango la kuzuia Ebola limesimama kando ya barabara ya vumbi katika Mkoa wa Ituri, DRC, huku watu wakitembea kando ya njia.
© UNOCHA Bango la uhamasishaji kuhusu Ebola limewekwa kwenye barabara ya vijijini katika Jimbo la Ituri mashariki mwa Congo DRC.

Harakati na mikusanyiko ya watu vifuatiliwe

Kwa mara ya kwanza, WHO pia imeitaka DRC kuwezesha kutumwa kwa timu za kimataifa za afya na vifaa vinavyohitajika, hususan kwa kuharakisha taratibu za uhamiaji na forodha.
WHO pia inapendekeza kuchunguza vifo vyovyote vinavyotokea nje ya vituo vya matibabu ili kubaini uwezekano wa uhusiano na maambukizi na kuelewa vizuri zaidi sababu za baadhi ya jamii kusita kuhusu mazishi salama na yenye heshima.
WHO imeendelea kuainisha mlipuko huo kama dharura ya afya ya umma yenye umuhimu wa kimataifa. Inasema hatari kwa nchi jirani bado ni “kubwa”, wakati kwa nchi nyingine inabaki kuwa “ndogo.”
Ili kupunguza hatari ya maambukizi, WHO imeitaka DRC kuimarisha ufuatiliaji wa watu wanaosafiri na kuahirisha mikusanyiko mikubwa katika maeneo yenye maambukizi. Pia inapendekeza kupunguza msongamano katika maeneo ya burudani, kuimarisha ukaguzi wa afya barabarani, kuhamasisha ufunguzi salama wa shule na kuzuia usafiri wa pikipiki kwa zaidi ya abiria mmoja.
WHO pia inapendekeza kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa boti zinazounganisha maeneo yaliyoathirika na miji mikubwa, hususan Kinshasa.
Kwa WHO, changamoto sasa ni kushinda mbio dhidi ya virusi, kufikia jamii, kuwalinda wanaowahudumia na kuvunja minyororo ya maambukizi kabla Ebola haijaendelea kusambaa zaidi.