Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 100 tangu Ebola kutangazwa nchini DRC hali inazidi kuwa mbaya

Mfanyakazi UNICEF anaonyesha bango la elimu la 'STOP EBOLA' kwa mwanamke aliyemshikilia mtoto wakati wa tukio la uhamasishaji wa jamii nchini DR Congo.
© UNICEF/Christian Kalengera Mfanyakazi wa jamii huko Bukavu, mashariki mwa DR Congo, anatoa elimu kuhusu jinsi ya kuzuia Ebola.

Siku 100 tangu Ebola kutangazwa nchini DRC hali inazidi kuwa mbaya

Afya

Zikiwa zimepita siku 100 tangu kutangazwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, maambukizi yanaendelea kuongezeka kwa kasi huku shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO likisema takribani wagonjwa 90 walithibitishwa kila siku katika miezi mitatu ya kwanza hiki kikiwa ni kiwango cha juu cha milipuko ikilinganishwa milipuko ya awali ya Ebola nchini DRC.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO kutoka Kinshasha nchini DRC, idadi ya wagonjwa wa Ebola nchini humo imefikia zaidi ya 5,200, huku mlipuko huu ukiwa ndio unaokua kwa kasi zaidi katika historia ya nchi hiyo. 

Mlipuko huo sasa umeenea katika majimbo sita, huku jimbo la Ituri likiendelea kuwa kitovu, llikibeba asilimia 85 ya wagonjwa wote na asilimia 79 ya vifo.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema, namnukuu “Tunaweza kudhibiti mlipuko huu wa Ebola, lakini kwa kuongeza nguvu za utekelezaji katika jamii zilizoathirika, ikiongozwa na viongozi wa kitaifa, wa majimbo na wa ngazi za chini pamoja na jamii husika, ikiungwa mkono na rasilimali zinazohitajika na ushirikiano thabiti wa wadau wote ndani na nje ya DRC. WHO na wadau wataendelea kuunga mkono serikali ya DRC, jamii na nchi jirani katika kutoa mwitikio unaohitajika kumaliza mlipuko huu.”

Vifo vinaendelea kuwa vingi, hasa vinavyotokea nje ya vituo vya matibabu ya Ebola, ambavyo vimechangia asilimia 60 ya vifo 260 vilivyoripotiwa kila wiki katika wiki sita zilizopita. Hali hii inaonesha changamoto kubwa katika ugunduzi wa mapema, urejeshaji wa wagonjwa na upatikanaji wa matibabu.

Wafanyakazi wa afya wakiwa wamevaa mavazi kamili ya kujikinga wakijiandaa kwa kampeni ya chanjo ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
©WHO/Grainne Harrington Wafanyakazi wa afya wakiwa wamevaa mavazi kamili ya kujikinga wakijiandaa kwa kampeni ya chanjo ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumza kuhusu hatua zinazohitajika, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Mohamed Janabi, anasema, namnukuu “Mlipuko huu umefikia hatua ya maamuzi muhimu. Maendeleo yaliyopatikana katika miezi mitatu iliyopita yanaonesha kuwa hatua imara huleta matokeo, lakini pia yanatukumbusha kuwa mafanikio madogo madogo hayatatosha. Sasa tunahitaji kuongeza kasi ya mwitikio: kuharakisha ugunduzi wa wagonjwa, kufikia jamii mapema zaidi na kuimarisha shughuli pale zinapohitajika zaidi. Maamuzi tunayofanya sasa ndiyo yataamua jinsi tutakavyoweza kudhibiti mlipuko huu haraka, kulinda na kuokoa maisha.”

Licha ya changamoto hizo ikiwemo ukosefu wa usalama, mizozo, wakimbizi wa ndani na mashambulizi kwenye vituo vya afya jitihada kubwa zimefanyika ikiwemo maabara zimeongezeka kutoka moja hadi 19, vitanda vya matibabu vimeongezeka kutoka chini ya kumi hadi zaidi ya 1,300, na kampeni za uhamasishaji jamii zimefikia zaidi ya watu milioni 2.5. 

WHO imepeleka wataalamu zaidi ya 260 na tani zaidi ya 330 za vifaa vya matibabu.

Wataalamu wanasema hatua za pamoja, usalama na uwekezaji endelevu ndizo zitakazoamua kama DRC itaweza kuzima mlipuko huu katika miezi ijayo.