Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 1.2 Colombia wanahitaji msaada huku baadhi ya jamii zikiwa bado hazijafikiwa: UN

Watoto watatu wamesimama wakiangalia majengo ya mbao na zege yaliyoharibika katika kitongoji baada ya tetemeko la ardhi.
© UNICEF Hatua za msaada nchini Colombia zinaendelea baada ya tetemeko la ardhi la ukubwa wa vipimo vya Richter 7.4. Huko Barrio Lleras, Buenaventura, zaidi ya nyumba 54 zimeharibiwa au ziko hatarini kuanguka.

Watu milioni 1.2 Colombia wanahitaji msaada huku baadhi ya jamii zikiwa bado hazijafikiwa: UN

Msaada wa Kibinadamu

Siku kumi baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba magharibi mwa Colombia, takribani watu milioni 1.2 wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku baadhi ya jamii zikiwa bado hazijafikiwa au zimepokea msaada mdogo sana, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema leo

Washirika wa misaada ya kibinadamu wanaomba dola milioni 135 ili kukabiliana na mahitaji yaliyosababishwa na tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.4 kwenye kipimo cha Richter, lililotokea tarehe 10 Agosti, kwa mujibu wa taarifa mpya ya  Mpango wa Umoja wa Mataifa wa hatua za Kibinadamu wa Colombia wa mwaka 2026.
Hatua hizo zinalenga kuwafikia watu 671,000, huku hatua za awali zikilenga zaidi maeneo yaliyoathirika vibaya ya Risaralda, Valle del Cauca, Chocó na Caldas.
Akizungumza kutoka Quibdó, mji mkuu wa Chocó na miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi, Jean-Philippe Antolin, mtaalamu wa hatua za kibinadamu na uokoaji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), amesema ukubwa kamili wa maafa hayo bado unaendelea kubainika.
“Kuna jamii ambazo bado hazijafikiwa, au zimefikiwa mara moja tu,” almewaambia waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
“Kwa kiasi kikubwa, kila kitu bado ni cha dharura.”
Jengo lililoporomoka huko Quibdó, Kolombia, lenye vifusi na uchafu barabarani karibu na bango la kivuko cha watembea kwa miguu la manjano.
© UNICEF/Augusto Pinedo Miundombinu huko Quibdó, Chocó, iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi la kipimo cha Rishter 7.4 lililoikumba Colombia.

Hofu ya nyumba kuporomoka

Takwimu za hivi karibuni za serikali zilizonukuliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa zaidi ya watu 300 wameuawa, watu 426 hawajulikani walipo, na zaidi ya 4,500 wamejeruhiwa katika manispaa 472 za idara 15.
Ameongeza kuwa Pia zaidi ya nyumba 163,000 zimeharibiwa na karibu 30,000 zimebomoka, huku angalau barabara 413 zikiathirika, hali inayofanya iwe vigumu kufikia baadhi ya jamii.
Kwa familia nyingi, hata nyumba ambazo bado zimesimama haziwezi kuchukuliwa kuwa salama.
“Ukiangalia kutoka nje, baadhi zinaweza kuonekana hazijaathirika. Lakini ukiingia ndani, utaona nyufa kila mahali,” amesema Antolin.akiongeza kuwa “Watu wanalala nje kwa hofu kwamba paa litawaangukia.”
Amesema tathmini za uimara wa majengo zinahitajika haraka ili familia ziweze kuanza kurejea katika makazi yao kwa usalama.
IOM imebaini angalau maeneo 71 ya makazi ya muda yanayohudumia takribani watu 4,700 katika miji ya Valle del Cauca, Risaralda, Chocó na Caldas. Wengine wanaishi kwa ndugu, wamepanga nyumba au wanaishi katika maeneo ya muda yasiyo rasmi.
Antolin ameonya kwamba makazi rasmi ya muda hayapaswi kuwa “sumaku za misaada, huku familia zinazoishi maeneo mengine zikikosa msaada.”
Mwanamume ameketi katikati ya vifusi vya jengo lililoanguka kufuatia tetemeko la ardhi huko Kolombia.
© UNFPA/Maidinchoco Mwanamume ameketi katikati ya vifusi vya jengo lililoporomoka huko Quibdó, Colombia.

Mvua zinaongeza hatari ya magonjwa

Mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko hilo, yakiwemo Pereira, Buenaventura na Quibdó, zinazidisha hali ngumu kwa familia zinazoishi katika makazi ya muda au maeneo yasiyo rasmi.
,” Antolin ameonya kuwa “Mvua pia inarahisisha kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na wadudu, kama vile homa ya kidingapopo.
Huko Chocó, mafuriko ya vyanzo vya maji na watu kukabiliwa na maji machafu pia vinaongeza hatari ya magonjwa ya kuhara na njia ya hewa.
Katika maeneo yaliyoathirika, takriban hospitali 50 zimepata uharibifu mkubwa, huku kukatika kwa umeme, maji, upatikanaji wa oksijeni, vifaa tiba na usafiri kukiongeza zaidi shinikizo kwenye huduma za afya.

Athari kwa maisha ya vijijini bado hazijajulikana

Mbali na dharura ya sasa, athari za tetemeko hilo kwa maisha na shughuli za kiuchumi za jamii za vijijini bado hazijafahamika kikamilifu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limesema kuna “pengo kubwa la taarifa kuhusu uharibifu wa mazao, mifugo, uvuvi wa jadi, mifumo ya umwagiliaji na mavuno”.
Jamii nyingi za vijijini, kandokando ya mito na maeneo ya pwani zilizoathirika hutegemea zaidi kilimo cha familia na uvuvi wa jadi, lakini ukubwa kamili wa uharibifu bado haujaainishwa.
FAO pia imeonya kuwa tetemeko hilo limetokea wakati wa msimu wa kupanda na kuvuna katika baadhi ya maeneo, hivyo kupotea kwa msimu mmoja wa uzalishaji kunaweza kuziacha familia zikiwa na rasilimali chache kwa msimu unaofuata.
Watu wamesimama kati ya vifusi na jengo lililoanguka huku waokoaji wakipekua eneo hilo, huku kuta za matofali zilizoharibika na mihimili iliyoanguka ikiwa nyuma.
© Valentina Escobar Salazar Juhudi za uokoaji zinaendelea kusini mwa Cali, nchini Colombia, kufuatia tetemeko la ardhi la Agosti 10.

Mashirika ya UN yaongeza msaada

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaongeza msaada kadiri mahitaji yanavyoendelea kubainika.
  • IOM imezindua ombi la dola milioni 30 kwa ajili ya makazi, maeneo ya malazi ya muda, maji na usafi wa mazingira, afya, ulinzi na uokoaji katika kipindi cha miezi sita ijayo.
  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeanza kutoa msaada wa chakula cha dharura huko Pereira na Quibdó na linajiandaa kuupanua katika maeneo mengine yaliyoathirika, huku likiomba dola milioni 23 kuwasaidia takribani watu 100,000.
  • UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika Idadi ya Watu na afya ya uzazi, linapeleka timu zinazohama huko Chocó kusaidia manusura wa ukatili wa kijinsia na wanawake wajawazito, huku likitoa vifaa vya usafi na mahitaji ya afya ya mama.
  • UNICEF inatoa msaada wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa familia zilizoathirika na kushirikiana na mamlaka za kitaifa katika ulinzi wa watoto.
  • Mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ametoa dola milioni 5 kutoka Mfuko wa Dharura waUmoja wa Mataifa (CERF) kusaidia hatua zinazoongozwa na serikali.
Ingawa juhudi za uokoaji na urejeshaji zimeanza, Antolin amesisitiza kuwa mahitaji ya haraka ya kibinadamu bado ni makubwa.
“Urejeshaji maisha huanza siku ya kwanza,” amesema. “Lakini huchukua muda. Zimepita siku kumi tu.”