WFP yaongeza operesheni za msaada kwa manusura wa teteko la ardhi Colombia
WFP yaongeza operesheni za msaada kwa manusura wa teteko la ardhi Colombia
Msaada wa Kibinadamu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa, WFP, limeongeza operesheni za dharura nchini Colombia baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa vipimo vya Richter 7.4 kupiga maeneo kadhaa ya nchi hiyo tarehe 10 Agosti.
Maelfu ya familia zimeathirika, huku baadhi zikilazimika kuishi katika makaazi ya muda baada ya nyumba zao kuharibika. WFP inalenga kuwafikia watu 100,000 kwa msaada wa chakula katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Vumbi linaanza kutulia nchini Colombia, lakini kwa maelfu ya familia zilizoathiriwa na tetemeko kubwa la 10 Agosti, hali ya dharura bado haijaisha.
Huko Quibdó, katika jimbo la Chocó, magharibi mwa nchi, majengo yaliyoharibiwa ni ushahidi wa wazi wa tetemeko hilo. Timu za WFP, ziko katika eneo hilo kutathmini mahitaji na kuandaa msaada wa chakula kwa baadhi ya jamii zilizo katika mazingira magumu zaidi nchini Colombia.
Huko Pereira, katika jimbo la Risaralda, msaada tayari umeanza kutolewa.
Makaazi ya muda yamejengwa kwa haraka katika maeneo ya wazi huku familia zikikabiliana na nyumba zilizoharibiwa na huduma kuvurugika.
Lengo ni kkuwafikia manusura wengi na msaada
Jumapili mwishoni mwa wiki pekee, zaidi ya watu 2,000 huko Pereira na Quibdó walipokea msaada wa chakula kutoka WFP. Nils Grede Mkurugenzi wa WFP nchini Colombia anasema “Kama Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, tunaona tunahitaji kuwasaidia watu 100,000, ambapo 40,000 kati yao wako Chocó. Watu wawili kati ya watatu huko Chocó wanaishi katika umaskini, hivyo wanahitaji msaada wa kila mtu.”
Tani 25 za chakula zikiwemo mchele, unga, maharagwe na dengu zinashushwa na kufungwa katika vifurushi vya dharura.
Wahudmu wa kujitolea pamoja na wafanyakazi wa WFP na timu za serikali za kukabiliana na dharura, sasa wanashusha bidhaa za msaada kutoka kwenye malori na kuzifunga katika vifurushi maalum kwa ajili ya familia zinazohitaji msaada zaidi.
WFP inasema inalenga kuwafikia watu 100,000 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, na inaomba dola milioni 23 za Marekani kufanikisha operesheni hiyo.
Katika maeneo ya mbali ambako masoko yamevurugika na barabara ni ngumu kufikika, familia zitapatiwa chakula moja kwa moja.
Msaada wa fedha pia kutolewa kwa jamii
Katika miji ambako masoko yanaanza kurejea katika hali ya kawaida, WFP inapanga kutoa msaada wa fedha, ili familia ziweze kununua chakula wanachohitaji huku zikiendelea kusaidia wafanyabiashara wa eneo hilo.
Kwa jamii za Chocó na Valle del Cauca, tetemeko hili limeongeza changamoto zilizokuwepo tayari. Karibu mtu mmoja kati ya watatu katika maeneo haya alikuwa tayari anakabiliwa na ukosefu wa chakula kabla ya tetemeko.
Sasa familia zinakabiliwa na kupoteza nyumba, kipato na huduma muhimu.
Grede anasema “Mshikamano uliooneshwa mara tu baada ya tetemeko umekuwa wa kipekee. Lakini tunajua kutokana na uzoefu kwamba kupona hakumaliziki baada ya wimbi la kwanza la msaada kupita.”
Wakati Colombia ikianza safari ndefu ya kujiimarisha, mashirika ya kibinadamu yanaonya kwamba mahitaji ya chakula na msaada yataendelea kuwepo kwa muda.