Wahudumu wa kibinadamu washambuliwa huku droni huku zikibadili sura ya vita: OCHA/WHO
Msaada wa Kibinadamu
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba wahudumu wa kibinadamu wanakabiliwa na tishio linalozidi kuwa la hatari na kubadilika kwa kasi, huku ndege zisizo na rubani zenye silaha zikibadilisha medani za vita duniani na kuyaweka zaidi makundi ya kibinadamu katika mstari wa mashambulizi.
Katika tathmini mpya, ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura (OCHA) iliyotolewa leo katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahudumu wa Kibinadamu imeonya kwamba wahudumu 907 wa kibinadamu walikumbwa na vitendo vya ukatili mwaka jana, wakati wakitekeleza kazi zao za kuokoa maisha katika maeneo ya migogoro yanayozidi kuwa ya hatari.
Kwa mujibu wa tathimini hiyo Vifo vilipungua mwaka 2025 lakini bado vilibaki katika kiwango cha juu kihistoria, huku wahudumu 350 wa kibinadamu wakiuawa idadi ya pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa.
Mwelekeo mkubwa wa ukatili haujaonesha dalili za kupungua mwaka huu. Kwa mujibu wa kitengo cha takwimu za usalama wa wahuddumu wa kibinadamu kinachofadhiliwa na serikali za Australia na Canada, hadi sasa wahudumu wengine 322 wamejeruhiwa na 235 wametekwa nyara.
Gaza bado ni eneo hatari zaidi
Licha ya kutangazwa kwa kusitishwa kwa mapigano Oktoba mwaka jana, Gaza tathimini inasema imeendelea kuwa eneo hatari zaidi kwa wahudumu wa kibinadamu mwaka 2025, ikiwa ni kwa mwaka wa tatu mfululizo, huku wahudumu 186 wakiuawa. Asilimia 68 ya vifo hivyo vilisababishwa na mashambulizi ya angani.
Nchini Sudan, mapigano makali yameendelea kuongeza idadi ya vifo kwa mwaka wa tano mfululizo, huku wahudumu 71 wakiuawa idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa, wengi wao wakipigwa risasi kwa kutumia silaha ndogo.
Maeneo mengine yaliyokuwa na ukosefu mkubwa wa usalama mwaka 2025 ni pamoja na Ukraine, Ethiopia, Syria, Haiti, Chad na Cameroon, ambako utekaji nyara na mashambulizi ya angani yalikuwa miongoni mwa aina kuu za ukatili.
Hadi sasa mwaka 2026, wahudumu 82 wa kibinadamu wameuawa, 97 wamejeruhiwa na 39 wametekwa nyara duniani kote.
“Zaidi ya wahudumu 1,000 wa kibinadamu wameuawa katika kipindi cha miaka mitatu pekee, na hilo halikubaliki kabisa,” amesema Tom Fletcher, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa.
“Lakini kulaani hali hii pekee hakutamlinda mhudumu anayefuata. Mataifa lazima yaheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kutumia kila njia kulinda raia na wafanyakazi wenzetu. Na kwa wale wanaokiuka sheria, lazima kuwe na adhabu za kweli,” ameongeza.
Kifo kutoka angani
Mashirika ya kibinadamu pia yanakabiliwa na mabadiliko ya haraka katika medani za vita, ambako ndege zisizo na rubani zenye silaha au droni, ambazo ni nafuu na rahisi kubadilishwa kwa matumizi mbalimbali, zinawezesha watu wengi zaidi kupata uwezo wa kufanya mashambulizi ya kuua na kurusha vilipuzi hadi ndani zaidi ya miji na maeneo ya makazi.
Nchini Sudan, ndege zisizo na rubani zenye silaha zilisababisha asilimia 80 ya vifo vya raia katika miezi minne ya kwanza ya 2026, zikilenga maeneo kama masoko na vituo vya afya, kwa mujibu wa OCHA.
Nchini Ukraine, ndege zisizo na rubani ziliwaua raia 80 mwezi Aprili pekee mwaka huu. Nchini Urusi, mashambulizi ya ndege hizo pia yamesababisha vifo vya raia na kuharibu miundombinu ya kiraia.
Nchini Colombia, mashambulizi yaliyohusisha ndege zisizo na rubani zilizobeba silaha yaliongezeka mara nne kati ya 2024 na 2025.
Wahudumu wa kibinadamu wanazidi kukumbwa na tishio hilo. Wahudumu wa afya na misaada ya kibinadamu wanazidi kulengwa. Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) limerekodi mashambulizi 639 dhidi ya huduma za afya tayari mwaka huu.
Mwezi Machi, mhudumu wa kibinadamu aliuawa baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia jengo la makazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Nchini Ukraine, misafara minne ya misaada ya kibinadamu ilishambuliwa ndani ya wiki moja mwezi Mei.
“Ndege zisizo na rubani zenye silaha zimekuwa sura mpya ya hatari ya zamani: uharibifu wa makusudi au wa uzembe wa maisha ya raia,” alisema Fletcher.
“Teknolojia inaweza kubadilika, lakini sheria za vita hazibadiliki.”
Wito wa ulinzi
Sheria za kimataifa za kibinadamu zinazitaka pande zinazohusika katika migogoro ya silaha kuwalinda raia na kuheshimu wahudumu wa kibinadamu wanaofanya kazi ya kuwasaidia.
Mashirika ya kibinadamu yanafanya kazi kufikia watu milioni 87 wanaokabiliwa na mahitaji makubwa zaidi duniani mwaka huu.
Kukumbuka shambulizi katika hotel ya Canal
Siku ya Kimataifa ya Kibinadamu huadhimishwa kila mwaka tarehe 19 Agosti, ikiwa ni kumbukumbu ya shambulio la bomu dhidi ya hoteli ya Canal mjini Baghdad, Iraq, mwaka 2003.
Wafanyakazi 22 wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika shambulio hilo, akiwemo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Sergio Vieira de Mello.
Miaka mitano baadaye, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliteua tarehe 19 Agosti kuwa Siku ya Kimataifa ya Kibinadamu.
Mwaka huu, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa wale wenye mamlaka Chukua hatua kwa ajili ya ubinadamu, #ActForHumanity