Wahudumu wa kibinadamu wanaohatarisha maisha kuwaokoa wengine lazima walindwe: UN
Wahudumu wa kibinadamu wanaohatarisha maisha kuwaokoa wengine lazima walindwe: UN
Msaada wa Kibinadamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kuwalinda wahudumu wa kibinadamu wanaotoa msaada wa kuokoa maisha katika maeneo yenye migogoro, akisema kuwahudumia wengine sasa kumekuwa hatari zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Katika ujumbe wake wa Siku ya Wahudumu wa Kibinadamu Duniani, Guterres amewasifu mamilioni ya wahudumu wanaowafikia watu walio katika uhitaji, huku akionya kuhusu ongezeko la mashambulizi dhidi yao.
“Kuwahudumia wengine sasa kumekuwa hatari zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” amesema Guterres.
Zaidi ya wahudumu 1,000 wameuawa
Guterres amesema zaidi ya wahudumu 1,000 wa kibinadamu wameuawa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, wengi wao wakiwa wahudumu wa ndani waliokuwa wakisaidia jamii zao wenyewe.
Amesema wengine wengi wamenusurika kwa shida baada ya kushambuliwa kwa risasi, makombora na mabomu, pamoja na kutekwa nyara au kubakwa.
Wakati huohuo, shule na hospitali zinazidi kushambuliwa, huku matumizi ya zana mpya za vita, ikiwemo ndege zisizo na rubani droni zenye silaha, yakileta hatari zaidi kwa wahudumu na raia.
Ufadhili na upatikanaji wa misaada unapungua
Katibu Mkuu amesema changamoto hizo zinaongezwa na taarifa potofu, kupunguzwa kwa ufadhili wa kibinadamu na vikwazo vya kufikisha misaada kwa watu wanaohitaji.
“Tunaona misafara ya misaada ikizuiwa. Wahudumu wa misaada wakitishiwa, kukamatwa na kuwekwa kizuizini. Na watu wenye mahitaji makubwa wakiachwa bila msaada,” amesema.
Amesema mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu ni kinyume cha sheria na yana madhara makubwa kwa familia zinazopambana kuishi, watoto wanaosubiri chakula na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.
“Ni lazima tusimame kwa ajili yao”
Guterres amesema jumuiya ya kimataifa imeweka ahadi za kuwalinda wahudumu wa kibinadamu na kuhakikisha misaada inawafikia wanaohitaji, lakini sasa ahadi hizo lazima zigeuzwe kuwa hatua.
Ametaka mataifa yaheshimu sheria za vita, yahakikishe upatikanaji salama wa misaada, yawawajibishe wanaohusika na mashambulizi na yatoe rasilimali za kutosha kwa operesheni za kibinadamu.
Ameongeza kuwa “Wahudumu wa kibinadamu hujitokeza kuwatetea na kuwasaidia watu wenye mahitaji. Ni lazima tusimame kwa ajili yao.”
Akihitimisha ujumbe wake, Katibu Mkuu ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa, akisema: “Ni lazima tuchukue hatua kwa ajili ya ubinadamu sasa.”