FAO Tanzania yaimarisha kilimo cha mwani huko Zanzibar
- Mafunzo kwa wanawake na vijana yameongeza uzalishaji na tija
- Vijana wamejengewa uwezo wa usindikaji, ubunifu na uongezaji thamani wa bidhaa za mwani
- Wanawake wanalima mwani huku wakifuga majongoo bahari
- Wakulima wamepatiwa mbinu bora za kuanika na kuhifadhi mwani
Tangu kuanza kwa uzalishaji wa zao la mwani Zanzibar, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO) limekuwa likishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau mbalimbali katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya mwani.
Msaada wa FAO umejikita katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na sera na mipango ya maendeleo ya sekta, utafiti hususan kuhusu changamoto za magonjwa ya mwani, kuimarisha mbinu bora za uzalishaji, uvunaji, uanikaji na uhifadhi, uongezaji wa thamani, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko.
Kuanzia mwaka 2019 hadi sasa, msaada wa FAO Zanzibar umejikita katika maeneo yafuatayo:
1. Kuongeza uzalishaji na tija
FAO imesaidia kuongeza uzalishaji na tija ya mwani kupitia uhamasishaji na matumizi ya mbinu bora za uzalishaji zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi. Msaada huu umejumuisha pia mchango katika uandaaji wa Mwongozo wa Uzalishaji wa Zao la Mwani, unaolenga kuwawezesha wakulima kutumia mbinu bora na endelevu za uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
2. Kuwawezesha vijana katika uongezaji thamani na ujasiriamali
Kupitia Zanzibar Technology and Business Incubator (ZTBI- kituo cha kulelea wajasiriamali), FAO ilijengea uwezo wa vijana katika usindikaji na uongezaji wa thamani wa bidhaa za mwani. Vikundi viwili vya vijana vilipatiwa mafunzo kuhusu ubunifu na uundaji wa bidhaa za mwani, uboreshaji wa ubora, uongezaji wa thamani, taratibu za kupata ithibati (certification) kutoka mamlaka husika, pamoja na mikakati ya kufikia masoko.
Aidha, vikundi hivyo vilipatiwa mashine na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya uzalishaji na usindikaji wa bidhaa za mwani. Vifaa hivyo bado vinapatikana katika kituo kwa ajili ya matumizi ya vijana na kuendeleza shughuli za ujasiriamali na ubunifu.
3. Kuimarisha uzalishaji kupitia kilimo mchanganyiko cha mwani na viumbe wa baharini
FAO ilisaidia uanzishwaji wa Mariculture Hatchery kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga vya viumbe wa baharini, ikiwemo majongoo bahari.
Kupitia mpango huu, wanawake wamejengewa uwezo kuhusu teknolojia ya Integrated Multi-Trophic Aquaculture (IMTA), inayowawezesha kuchanganya ufugaji wa majongoo bahari na kilimo cha mwani.
Teknolojia hii inalenga kuongeza tija na kipato cha wakulima, kutumia rasilimali za bahari kwa ufanisi zaidi, pamoja na kuimarisha uwezo wa jamii za pwani kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pia inatoa fursa ya wanawake kutengeneza vyanzo mbalimbali vya kipato ndani ya shughuli zao za uzalishaji wa baharini.
4. Kuongeza ubora wa mwani baada ya kuvuna
FAO imeendelea kuwajengea uwezo wakulima, hususan wanawake, kuhusu mbinu bora za uanikaji na uhifadhi wa mwani kwa lengo la kuboresha ubora wa zao na kupunguza upotevu baada ya mavuno.
Katika kuunga mkono juhudi hizi, vikundi 33 vya wanawake vimewezeshwa kwa kujengewa chanja bora za kuanikia mwani pamoja na kupatiwa maturubai maalum ya kufunikia mwani, hususan wakati wa mvua. Hatua hii imechangia kuwezesha wakulima kuboresha mazingira ya uanikaji na uhifadhi na hivyo kuongeza uwezekano wa kupata mwani wenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Kwa ujumla, uwekezaji wa FAO katika sekta ya mwani Zanzibar umejikita katika kujenga mfumo jumuishi unaounganisha uzalishaji bora, utafiti na ubunifu, uhimilivu wa tabianchi, uongezaji wa thamani, uwezeshaji wa wanawake na vijana, ubora wa bidhaa na upatikanaji wa masoko. Juhudi hizi zinaendelea kuchangia katika kuimarisha ushindani wa sekta ya mwani na kuongeza fursa za kipato na ajira kwa jamii zinazotegemea shughuli za mwani Zanzibar.