Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola DRC: Mtu mmoja anafariki kila baada ya dakika 30

Wajumbe wa timu ya Mazishi Salama na Yenye Heshima katika jamii wakiwa wamevaa vifaa vya kujikinga wakijiandaa kubeba jeneza katika Kituo cha Matibabu cha Ebola cha Rwampara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNOCHA/Ramatoulaye Moussa Maz Ebola imesababisha vifo vya watu wapatao 2,000 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC.

Ebola DRC: Mtu mmoja anafariki kila baada ya dakika 30

Taarifa mahususi
Msaada wa Kibinadamu

Kila baada ya dakika 30, familia moja nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, inapoteza mpendwa wake kutokana na ugonjwa wa Ebola. Zaidi ya watu 2,000 tayari wamefariki dunia huku mlipuko huo ukitajwa kuwa unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kurekodiwa.

“Ebola inashinda nchini DRC. Hatuwezi kuruhusu virusi hivi (aina ya Bundibugyo) viendelee kukimbia kwa kasi kuliko mwitikio wetu,” ameonya Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Misaada ya Dharura, OCHA, Tom Fletcher, katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake mjini Geneva, Uswisi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya kuongoza mkutano wa dharura wa viongozi wa mashirika makubwa ya kibinadamu duniani, Fletcher ametangaza nyongeza ya dola milioni 30.5 kutoka Mfuko Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Dharura, CERF.

Fedha hizo zinaongezea dola milioni 24 zilizotolewa awali kwa DRC na nchi nne jirani.

Watumishi wengine 20 pia wametumwa katika maeneo yaliyoathirika. 

Hata hivyo, juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza vituo vya matibabu, kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa, kuhakikisha mazishi salama na kutoa maji safi, huduma za afya na usafi.

Wapiganaji wa zamani huko Ituri, DR Congo, wakiwa wamevaa fulana nyeupe zenye nembo za Ebola, wanaongoza kampeni ya uhamasishaji umma dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Ebola kwa usaidizi kutoka MONUSCO.
© MONUSCO Waasi wa zamani nchini DR Congo sasa wanaunga mkono uhamasishaji wa kuzuia Ebola katika jamii zao.

Kunahitajika kuongeza nguvu

“Huu ni wito wa kuamka. Tunahitaji kasi, mwitikio mkubwa na mshikamano kabla virusi hivi havijatutangulia mbali zaidi,” amesema Fletcher. “Zaidi ya watu 2,000 tayari wamefariki. Wengine wengi wako hatarini. Dunia inapaswa kuamka na kujitokeza.”

Katika taarifa yake ameeeleza kuwa mpango wa kuongeza mwitikio unalenga kuongeza mara mbili idadi ya timu zinazohakikisha mazishi salama na yenye kuheshimu utu wa waliofariki, kuongeza mara tatu uwezo wa vituo vya matibabu, kuboresha ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa pamoja na kupeleka mameneja zaidi wenye uzoefu.

Mashirika ya kibinadamu pia yanahitaji kukidhi mahitaji makubwa ya maji safi, huduma za usafi, matibabu na huduma nyingine za msingi katika maeneo yaliyoathirika.