Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR: Ukingo wa Magharibi Walowezi kuzingira Wapalestina si haki

Familia na watoto wa Kipalestina wakipita majengo yaliyoharibiwa na magari ya kijeshi yaliyoegeshwa katika kambi ya wakimbizi ya Jenin.
© UNICEF/Alaa Badarneh Wanawake na watoto wakitembe Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Isarel

OHCHR: Ukingo wa Magharibi Walowezi kuzingira Wapalestina si haki

Haki za binadamu

Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, OHCHR, leo imezitaka mamlaka za Israel kuzisaidia familia za Wapalestina zilizonaswa majumbani mwao kwa siku kadhaa kutokana na kuzingirwa na walowezi, huku kampeni ya kunyakua ardhi yao ikiendelea kushika kasi.

Mambo muhimu

  • Ukingo wa Magharibi umekuwa chini ya uvamizi wa Israel tangu vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1967.
  • Makazi ya walowezi wa Israel yalianza kupanuka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa muda mfupi baada ya mwaka 1967.
  • Mwaka 2005, Israel iliondoa makazi manne ya walowezi kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
  • Eneo hilo linalokaliwa ni sehemu muhimu ya mipango ya kuanzishwa kwa taifa la baadaye la Palestina, lakini upanuzi wa makazi ya walowezi unaoambatana na ghasia unazidi kuwa kikwazo kwa suluhu aa mataifa mawili.
Kwa mujibu wa taarifa, Marekani imehusika katika juhudi za kukomesha mzingiro huo ulioanza Jumapili, huku Balozi wa Marekani nchini Israel akitaka kuondolewa kwa watu aliowaita “magaidi wa Israel”.
Familia tatu za Wapalestina takriban watu 15 kwa jumla, wakiwemo angalau watoto wawili zimeendelea kufungiwa ndani ya nyumba zao “katika hali ya hofu kubwa” katika eneo la Ras al Ein, kijiji cha Qusra, kusini mwa Nablus, imesema ofisi ya OHCHR, ikidai kuwa walowezi wamekata umeme na maji.
“Vitendo hivi vya uhalifu vinavyofanywa na walowezi, vinavyoungwa mkono au kuvumiliwa na Israel, ambayo ni mamlaka inayokalia eneo hilo, vinafanya maisha kuwa magumu kuvumilika kwa familia hizi za Wapalestina na vinalenga waziwazi kuwalazimisha kuondoka katika nyumba na ardhi yao,” imesema ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa. “Muda unazidi kuyoyoma kwa familia hizi tatu kabla hazijalazimishwa kuhama.”
Uzio wa usalama wa Israeli unapita kando ya kilima, ukitenganisha eneo la ujenzi mbele na eneo la makazi lenye majengo meupe kwenye kilima nyuma chini ya anga safi la bluu.
© Adobe Stock/Voddol Kizuizi cha usalama kinaonesha eneo la makazi katika Ukingo wa Magharibi.

Hakuna mahali pa kwenda

Baada ya taarifa ya awali ya OHCHR, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Eneo la Palestina linalokaliwa na Israel , Ajith Sunghay, ameiambia UN News kwamba familia hizo baadaye zilihamishwa na kuwekwa katika nyumba moja tu, ambayo bado imezungukwa na walowezi wa Israel.
“Kwa mara nyingine, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) ama haliwezi au halitaki kuzilinda jamii za Wapalestina, jambo ambalo linatarajiwa kulifanya chini ya Mkataba wa Geneva, au, jambo baya zaidi, IDF iko katika ushirikiano na walowezi wa Israel, yote hayo yakilenga kuwahamisha Wapalestina na kutwaa ardhi zao,” amesema Bwana. Sunghay.
Amebainisha pia kuwa takriban familia 20 za Wapalestina kutoka Qusra ziliondolewa na wanajeshi wa IDF “kwa madhumuni ya usalama”, kabla ya kusisitiza umuhimu wa haraka wa msaada wa kimataifa ili kukomesha hali inayozidi kuwa hatari katika eneo linalokaliwa.
Ameongeza kuwa “Tunakaribisha sana taarifa za kulaani, tunakaribisha sana mazungumzo. Hata hivyo, hii haitoshi kabisa. Nadhani tumepita hatua ya kufikia kiwango cha kuchemka. Tunaona kiwango cha ghasia za walowezi ambacho hakijawahi kushuhudiwa, na tunaziomba nchi Wanachama zichukue hatua na zitumie ushawishi wao kwa kila njia inayowezekana.”
OHCHR imebainisha kuwa Wapalestina wanaoishi Qusra wamekuwa wakilengwa na “mashambulizi yanayoongezeka mara kwa mara” tangu Novemba 2025, wakati walowezi wa Israel walipoanzisha kituo cha walowezi katika eneo lililo karibu.
Maombi ya awali kutoka kwa familia hizo za Wapalestina kwa wanajeshi wa Israel waliokuwa katika eneo hilo kuingilia kati hayakusaidia.
“Badala yake, vikosi vya usalama vya Israel vinaonekana kuwazuia wahudumu wa afya, wanaharakati wa mshikamano na waandishi wa habari kuwafikia familia hizo,” imesema OHCHR, ikiongeza kuwa ingawa wanajeshi walivunja mahema ya walowezi siku ya Jumatano, waliendelea kuzunguka nyumba za Wapalestina.
Mwanamume Mpalestina amesimama katikati ya magofu kufuatia uharibifu wa nyumba yake huko Al Jiftlik-Abu al 'Ajaj, jimbo la Jericho, kutokana na ukosefu wa vibali vya ujenzi.
© UNOCHA Wapalestina wengi katika jumuiya tisa katika Ukingo wa Magharibi wamehamishwa kutokana na mashambulizi sasa mnamo 2026.

Hali yazidi kuwa mbaya

Bwana. Sunghay amebainisha kuwa matukio makubwa ya Qusra yalikuwa yakitokea sambamba na matukio mengine yanayotia wasiwasi mkubwa yanayoongozwa na walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Hii ni pamoja na hatua ya IDF siku ya Jumanne ya kuweka vizuizi katika mji wa Taybeh kwa watu wasioishi huko, ikidaiwa kuwa ni hatua ya kuwalinda dhidi ya mashambulizi ya walowezi wa Israel.
“Katika hali kama hi ni Wapalestina wanaolipa gharama na kubeba mzigo mkubwa wa matatizo, ingawa ni Waisraeli ambao ni walowezi wanaosababisha ghasia, mashambulizi na matatizo kwa Wapalestina,” amesisitiza afisa huyo mwandamizi wa OHCHR.
Katika pigo jingine kwa juhudi za amani katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, Bwana. Sunghay amebainisha kuwa walowezi wa Israel wamerudi Ganim, moja ya makazi manne ya Israel kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi ambayo yaliondolewa mwaka 2005 (mengine yakiwa Kadim, Sa-Nur na Homesh). “Huu ni mwelekeo ambao tumeuona mara kwa mara ukitokea katika Ukingo wa Magharibi,” amesema.
Takwimu za hivi karibuni kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, leo zimeonesha jinsi “ghasia na unyanyasaji” wa walowezi wa Israel ulivyoendelea kulenga jamii za Wapalestina kote katika Ukingo wa Magharibi. Hii inajumuisha wale wanaoishi katika Milima ya Hebron Kusini na Bonde la Jordan.
“Wakati huohuo, upanuzi wa makazi ya walowezi umeendelea, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo kadhaa vipya vya walowezi,” imesema UNRWA.
Mkulima katika Ukingo wa Magharibi, akiwa na kondoo mchanga, akionesha mazoea ya kilimo yanayoungwa mkono na FAO.
© FAO Mkulima katika Ukingo wa Magharibi, akiwa na kondoo mchanga, akionesha mazoea ya kilimo yanayoungwa mkono na FAO.

Uhalisia wa Operesheni ‘Iron Wall’

Shirika hilo limebainisha kuwa vikosi vya Israel vimeongeza muda wa amri ya kufungwa kijeshi inayoathiri kambi za Tulkarm na Nur Shams kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi hadi tarehe 30 Septemba 2026, na kambi ya Jenin hadi tarehe 20 Agosti 2026.
UNRWA imesisitiza kuwa hatua hiyo ni kuendeleza amri za awali za kufungwa ambazo zimezuia kwa kiasi kikubwa watu kufikia kambi hizo, ambazo kwa sehemu kubwa zimekuwa tupu.
Kwa sasa, zaidi ya wakimbizi 34,000 wa Kipalestina bado wamelazimika kuhama kutoka katika kambi za Tulkarm, Nur Shams na Jenin kutokana na operesheni ya kijeshi ya Israel ya “Iron Wall”, iliyoanza Januari 2025.