UN yatenga dola milioni 5 kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Colombia
Kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi ya Colombia, mahitaji ya kibinadamu yameongezeka na kuzidi uwezo wa mamlaka za maeneo yaliyoathirika kukabiliana na dharura hiyo, hali iliyoufanya Umoja wa Mataifa na wadau wake kuingilia kati ili kusaidia jamii zilizoathirika.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imetangaza kuwa dola milioni tano zimetengwa kupitia Mfuko Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Dharura, CERF, ili kupanua operesheni za kuokoa maisha na kufikisha msaada kwa watu walioathirika zaidi.
Takwimu za hali ilivyo mpaka sasa
Kwa mujibu wa taarifa ya OCHA iliyotolewa Agosti 12, tetemeko hilo limeathiri watu wasiopungua 49,214 kutoka familia 30,324 katika majimbo 13 ya Colombia.
Watu 241 wamefariki dunia na wengine 3,771 wamejeruhiwa.
Zaidi ya nyumba 54,900 zimeharibiwa kabisa au kupata uharibifu wa viwango tofauti. Shule, vituo vya afya, mifumo ya usambazaji wa maji na barabara pia zimeathirika, na hivyo kuwaacha maelfu ya watu bila huduma muhimu, ikiwemo matibabu, maji salama, ulinzi na njia za kujipatia kipato.
OCHA imesema mahitaji ni makubwa katika sekta mbalimbali, huku mapengo makubwa ya misaada yakiripotiwa katika maeneo ya Risaralda, Valle del Cauca, Chocó na Caldas.
Uharibifu wa barabara na miundombinu mingine unaendelea kuzuia baadhi ya jamii kufikiwa kwa urahisi.
Wadau waunganisha nguvu
Serikali ya Colombia, Umoja wa Mataifa na wadau wa masuala ya kibinadamu wanaendelea na operesheni za utafutaji na uokoaji, tathmini za haraka za mahitaji na usambazaji wa misaada.
Fedha hizo za CERF zinatarajiwa kuimarisha juhudi hizo na kusaidia mamlaka za nchi hiyo kukidhi mahitaji ya haraka ya waathirika.
OCHA imeonya kuwa dharura hiyo bado inaendelea kupanuka na inahitaji mwitikio endelevu na ulioratibiwa ili kuokoa maisha na kuhakikisha walioathirika wanapata makazi, huduma za afya, maji salama, ulinzi na mahitaji mengine ya msingi.