Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwitikio dhidi ya Ebola katika DRC lazima pia ukidhi mahitaji ya msingi ya watu – WHO

Wajitolea wa Msalaba Mwekundu huko Bunia, DRC, waendesha kikao cha uhamasishaji wa kuzuia Ebola na wanajamii huko Ujio wa Heri.
© UNOCHA/Priscilla Lecomte Wahudumu wa kujitolea kutoka shirika la Msalaba Mwekundu wakitoa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu Ebola huko Bunia jimboni Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC)

Mwitikio dhidi ya Ebola katika DRC lazima pia ukidhi mahitaji ya msingi ya watu – WHO

Afya
  • Kasi ya hatua dhidi ya Ebola iongezwe na ifikie kila jamii iliyoathirika
  • Jamii zinaomba kushirikishwa zaidi katika mwitikio na zinasema Ebola si changamoto pekee inayowatia wasiwasi
  • Bila kuongeza kwa kiasi kikubwa juhudi za mwitikio, mlipuko unaweza kuendelea kwa miezi au hata miaka.

Akizungumza kutoka Bunia, Ituri, huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako in kitovu cha mlipuko wa sasa wa Ebola, Dkt. Anne Ancia, ambaye ni Mwakilishi wa WHO nchini humo amesema jamii zilizoathiriwa na mlipuko wa sasa wa Ebola zinahitaji si tu matibabu dhidi ya ugonjwa huo, bali pia maji, chakula, matibabu ya malaria, chanjo na huduma za afya ya uzazi na mama.

Dkt. Ancia amemweleza EleuterIo Guevane wa UN News kwamba watu wana wasiwasi mkubwa kuhusu Ebola, lakini pia wanakabiliwa na changamoto pana za kibinadamu na kiafya.

“Watu katika vijiji vilivyoathiriwa hivi karibuni wameweka wazi kwamba wanataka kushirikishwa kwa karibu zaidi katika mwitikio. Pia wanataka msaada kwa mahitaji mengine ya dharura, yakiwemo maji, chakula, matibabu ya malaria, huduma za VVU na chanjo za kawaida kwa watoto,” amesema, akiongeza kwamba*,* “walisema si Ebola pekee. Ni kila kitu kingine. Ni suala la kuendelea kuishi siku hadi siku.”

‘Msije na Ebola pekee’

Dkt. Ancia amesema hivi karibuni alizungumza na mamlaka za mitaa, madereva wa teksi, vikundi vya jamii na wakazi katika vijiji vilivyoathirika. amesema madereva wa teksi wameathiriwa sana, huku vifo vikiripotiwa miongoni mwa wenzao.

Katika kijiji kimoja, amesema wakazi waliwaeleza wahudumu wa afya kwamba kituo chao cha afya kilikuwa kimegeuzwa kuwa kituo cha matibabu ya Ebola, huku mahitaji mengine ya matibabu yakiendelea kutotimizwa.

Walitueleza: mmechukua kituo chetu cha afya na kukigeuza kuwa kituo cha matibabu ya Ebola, lakini tuna mateso mengine hapa,” alisema.

Anakumbuka kushuhudia kifo cha mwanamke aliyekuwa akijifungua mapacha. Mwanamke huyo, ambaye alikuwa na upungufu wa damu wa muda mrefu, alihitaji kuhamishiwa katika huduma ya dharura baada ya kupata matatizo wakati wa kujifungua. Alifariki wakati akihamishiwa katika kituo kingine.

“Hakufariki kutokana na Ebola,” amesema Dkt. Ancia, akisisitiza kwamba tukio hilo lilionyesha kwa nini mwitikio lazima upanuke zaidi ya ugonjwa mmoja.

Dkt. Ancia amesema sehemu ya mashariki ya DRC inakabiliwa na hali tete sana ya uhakika wa kupata chakula, huku familia nyingi zikihangaika kukidhi mahitaji ya msingi.

Afisa huyo wa WHO amesema washirika wa kibinadamu wanafanya kazi kuongeza msaada, lakini ameonya kwamba mwitikio lazima uende kwa kasi zaidi.

“Tunahitaji kuleta kwa haraka zaidi huduma zote muhimu za afya na huduma za matibabu,” amesema. “Si kuongeza tu juhudi dhidi ya Ebola, bali kuongeza mwitikio mpana zaidi unaoshughulikia mahitaji yote.”

Tuongeze kasi ya ufuatiliaji

Dkt. Ancia amesema mwitikio dhidi ya Ebola lazima upanuliwe katika maeneo yote yaliyoathirika, yakiwemo vijiji na jamii za mbali. “Tunahitaji kuongeza uwezo wa ufuatiliaji; idadi ya vitanda vinavyopatikana kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji tiba ya Ebola; mifumo ya kutoa tahadhari katika jamii; usafiri wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola; uwezo wa uchunguzi wa maabara; ushirikishwaji wa jamii; na uwepo wa shughuli za mwitikio nje ya vituo vikuu.”

Hatari ya Ebola kudumu kwa muda mrefu

Alipoulizwa nini kinaweza kutokea ikiwa mwitikio wa kimataifa hautaongezwa kwa kiasi kikubwa, Dkt. Ancia ameonya kwamba mlipuko huo unaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi na kuwa vigumu zaidi kudhibiti.

Ametamatisha akisema kuwa kipaumbele kwa sasa ni kuunganisha udhibiti wa Ebola na hatua pana za kibinadamu zinazoakisi mahitaji ambayo jamii zinaomba yatimizwe.