Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko kubwa la ardhi Colombia: UN yasema hakuna ombi rasmi la msaada, lakini iko tayari kusaidia

Watu wamesimama kati ya vifusi na jengo lililoanguka huku waokoaji wakipekua eneo hilo, huku kuta za matofali zilizoharibika na mihimili iliyoanguka ikiwa nyuma.
© Valentina Escobar Salazar Juhudi za uokoaji zinaendelea kusini mwa Cali, nchini Colombia, kufuatia tetemeko la ardhi la Agosti 10.

Tetemeko kubwa la ardhi Colombia: UN yasema hakuna ombi rasmi la msaada, lakini iko tayari kusaidia

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya saa 24 baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuikumba Colombia, Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Dharura (OCHA) umesema bado haujapokea ombi rasmi la msaada wa kimataifa kutoka kwa mamlaka za nchi hiyo, lakini umejipanga kutoa msaada wowote utakaohitajika.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Colombia, watu 126 wamefariki dunia huku zaidi ya 1,490 wamijeruhiwa kufuatia tetemeko hilo la ukubwa wa kiwango cha 7.4 katika kipimo cha Richta

Picha ya infographic inayoelezea athari za tetemeko la ardhi huko Kolombia mnamo Agosti 10, 2026, ikionyesha data kuhusu vifo, majeruhi, nyumba zilizoharibiwa, na vifaa vya umma vilivyoharibika.
UN News Athari mbaya ya tetemeko la ardhi Colombia

OCHA: Tuko tayari kusaidia

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OCHA, Jens Laerke, amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali kwa karibu huku ukisubiri maamuzi ya serikali ya Colombia.

"Kwa sasa hakujakuwa na ombi rasmi la usaidizi wa kimataifa; hivi ni kwa wakati huu ninapozungumza, na inawezekana msimamo huo ukabadilika. Iwapo itakuwa hivyo, mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, bila shaka, hususan wahudumu wa kibinadamu tuko tayari kusaidia kwa chochote kile tulichonacho," amesema Laerke.

Uharibifu mkubwa waripotiwa

Tetemeko hilo lilitokea saa 1:34 asubuhi kwa saa za Colombia, likiwa na kitovu karibu na mji wa San José del Palmar katika jimbo la Chocó, magharibi mwa nchi karibu na Valle del Cauca.

Mitetemo yaendelea kurekodiwa

Mamlaka zimeendelea kufuatilia hali baada ya tetemeko kuu, huku takribani mitetemo 12 ya baadaye yenye ukubwa wa zaidi ya 2.0 katika kipimo cha Richta ikirekodiwa tangu tukio lilipotokea.

Wataalamu wanaonya kuwa mitetemo ya baadae inaweza kuongeza hatari kwa majengo yaliyodhoofishwa na shughuli za uokoaji zinazoendelea.

Umoja wa Mataifa wafuatilia kwa karibu

Ingawa serikali mpya ya Colombia, iliyoingia madarakani tarehe 7 Agosti 2026, bado haijaomba msaada rasmi wa kimataifa, Umoja wa Mataifa unasema unaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa.

"Timu ya Umoja wa Mataifa, bila shaka, inafuatilia kwa karibu sana, sana. Timu ya OCHA inafuatilia kwa karibu sana, sana. Na timu nzima ya Umoja wa Mataifa nchini Colombia inakutana leo ili kuona jinsi inavyoweza kuendelea kusaidia mwitikio wa kitaifa wa mamlaka za Colombia kwa namna yoyote ile ambayo inaweza kuombwa, kuhitajika au kuwa muhimu," amesema Laerke.

Marundo makubwa ya maji ya chupa na vifaa vya msaada yanakusanywa nje ya jengo huko Cali, Kolombia, kufuatia tetemeko la ardhi.
© Helena Gutiérrez Maji yakiwa tayari yamekusanywa kwa ajili ya kupatia manusura wa tetemeko la ardhi lililoikumba Colombia.

WHO yatuma timu za dharura

Kwa upande wake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema tayari limeanza mwitikio wa dharura katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi. Msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic, amesema timu za kitaalamu zimepelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Cali na Chocó kusaidia tathmini ya mahitaji na uratibu wa huduma za afya.

"Ofisi yetu nchini Colombia ilianzisha mwitikio wake wa dharura, na timu zake za mashinani pamoja na timu nyingine zimetumwa katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko, yakiwemo Cali na Chocó, ili kusaidia katika tathmini na uratibu wa sekta ya afya."

Tetemeko lasikika nchi jirani

Mbali na Colombia, tetemeko hilo liliripotiwa kusikika pia katika nchi jirani za Panama, Ecuador na Venezuela ambayo yenyewe ilikumbwa na tetemeko la ardhi mwezi Juni mwaka huu, jambo linalozidisha wasiwasi kuhusu shughuli za kijiolojia katika ukanda huo wa Amerika Kusini.