Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasaidia Colombia baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba taifa hilo

Wahudumu wa dharura na umati wa watu wamekusanyika katika eneo la jengo lililoporomoka huko Cali, Kolombia kufuatia tetemeko la ardhi.
© Valentina Escobar Salazar Waokoaji wakitoa huduma kwenye jengo lililoporomoka huko Cali, nchiin Colombia.

UN yasaidia Colombia baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba taifa hilo

Msaada wa Kibinadamu

Kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililokumba Colombia, taifa lililo Amerika ya Kusini siku ya Jumatatu, Umoja wa Mataifa (UN) umepeleka  msaada wake wakati huu ambapo ripoti zinasema kuwa zaidi ya watu 111 wamekufa na wengine zaidi ya 87 wamejeruhiwa.

Tetemeko hilo la ukumbwa kwa 7.4 katika kipimo cha Richa limekumba eneo la magharibi mwa taifa hilo ambapo miongoni mwa majeruhi ni watoto.

Kwa sasa baadhi ya watu wamenasa kwenye vifusi vya majengo huku tetemeko hilo likisababisha maporomoko ya ardhi na uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu.

Timu za Umoja wa Mataifa  nchini Colombia zinawasiliana na mamlaka za kitaifa pamoja na wakala wa usimamizi wa hatari za majanga nchini humo ili kufuatilia kwa karibu hali hiyo na kusaidia juhudi za mwitikio wa kitaifa.

Akizungumza mjini New York, Marekani na waandishi wa Habari, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema kwa sasa Umoja wa Mataifa unafuatilia maendeleo ya hali hiyo na liko tayari kutoa msaada.

“Tunawapa pole wote walioathirika kutokana na tetemeko hili la ardhi, na tuko tayari kusaidia pale itakapohitajika,” amesema Bwana Haq.

Tetemeko hilo lilitokea majira ya saa 1:34 asubuhi kwa saa za huko Colombia, huku kitovu chake kikiwa karibu na San José del Palmar, katika jimbo la Chocó, karibu na Valle del Cauca.

Kwa mujibu wa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, María José Torres Macho, chombo hicho kina timu zinazotathmini hali katika maeneo yaliyoathirika na inaandaa, kwa kushirikiana na Serikali, kikao cha awali cha mwitikio wa dharura ili kubaini mahitaji na aina ya msaada unaoweza kuhamasishwa.

Watu wanachunguza vifusi vya jengo lililoanguka huko Cali, Kolombia baada ya tetemeko la ardhi.
© Valentina Escobar Salazar Jengo moja huko Cali, Colombia, limebomoka na kusalia vifusi kufuatia tetemeko la ardhi lenye ukumbwa wa 7.4 kwenye kipimo cha Richa.

Kilichojiri wakati wa tetemeko na kiwango cha uharibifu

Mtikisiko huo ulisikika katika maeneo mengi ya Colombia na katika nchi jirani, zikiwemo Panama, Ecuador na Venezuela.

Mamlaka zinaendelea na operesheni za utafutaji na uokoaji huku idadi ya waliofariki ikiendelea kuongezeka. 

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizopatikana saa 8:45 mchana kwa saa za Colombia, nyumba 1,575 zilikuwa zimeharibika na 37 zimebomoka kabisa, huku majengo 61 yakiwa yameporomoka. Uharibifu pia uliripotiwa katika vituo 18 vya afya na taasisi 52 za elimu.

Bwana Haq pia amebainisha kuwa ukosefu wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya vijijini unafanya iwe vigumu kutathmini athari kamili za tetemeko hilo, hivyo ukubwa halisi wa uharibifu bado haujajulikana.

Janga hilo limetokea siku tatu tu baada ya kuapishwa kwa Rais wa Colombia, Abelardo de la Espriella, ambaye leo amesema kipaumbele cha haraka ni kuwaokoa watu ambao bado wamenaswa chini ya vifusi.

Maeneo yaliyoathirika zaidi

Pereira, jiji lenye wakazi takribani 500,000, liko umbali wa takribani maili 35 kutoka kwenye kitovu cha tetemeko hilo. Wakati timu za dharura zikiendelea kuwasaka manusura, meya wa jiji hilo aliripoti kuwa watu 18 wamefariki huko.

Huko Cali, jiji la tatu kwa ukubwa nchini Colombia, mamlaka zimeripoti maporomoko kadhaa ya ardhi yaliyowanasa watu na zimeomba kuongezwa kwa vikosi vya uokoaji.

Tetemeko pia limeharibu miundombinu ya usafirishaji, huku viwanja kadhaa vya ndege magharibi mwa Colombia vikisimamisha shughuli wakati vituo hivyo vikikaguliwa.

Maagizo ya kuwaondoa watu katika maeneo hatarishi yalitolewa hadi katika mji mkuu, Bogotá, ambao uko umbali wa maili 250 mashariki mwa San José del Palmar.

Tayari kwa mwitikio

Mashirika kadhaa ya UN yameonesha mshikamano na jamii zilizoathirika na kusema yako tayari kusaidia, iwapo Serikali itaomba msaada.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema lina uwezo wa kutoa msaada wa kibinadamu kwa kuunga mkono Serikali na mamlaka za kitaifa za dharura.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, kanda ya Amerika, (PAHO) – ambalo ni sehemu ya mfumo mpana wa UN – limesema linaendelea kuwasiliana kwa karibu na mamlaka za kitaifa.

Kwa shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lenyewe linafuatilia hali hiyo na liko tayari kusaidia katika mwitikio, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao.

Mshikamano

Tweet URL

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, ameonesha mshikamano na Colombia na kusema shirika hilo liko tayari kusaidia jamii zilizoathirika.

Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, (UNFPA) limeonya kuwa katika aina hizi za dharura, wasichana, wanawake na vijana balehe wanaweza kukabiliwa na hatari kubwa zaidi ya ukatili wa kijinsia na changamoto za kupata huduma za afya. 

Shirika hilo limeonesha mshikamano na jamii zilizoathirika zaidi na kuhakikishia kuwa linafanya kazi kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kupatikana.

Kwa lile linalohudumia wakimbizi (UNHCR) nalo pia limesema linatathmini athari za tetemeko hilo na liko tayari kusaidia kwa kushirikiana na mamlaka na washirika wengine.