Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabaki ya nywele yageuzwa mbolea, yawaletea wakulima Tanzania suluhisho la gharama nafuu

Mwonekano wa juu wa ndoo ya plastiki ya kijani iliyojaa samadi nyeusi na yenye mabunda ya kikaboni iliyochanganywa na vipande vya nywele za binadamu na vifaa vingine vya kikaboni vya kahawia.
UN News Mabaki ya nywele za binadamu yanayotumika kutengeneza mbolea asilia nchini Tanzania

Mabaki ya nywele yageuzwa mbolea, yawaletea wakulima Tanzania suluhisho la gharama nafuu

Malengo ya Maendeleo Endelevu
  • Taka za nywele zageuka lulu
  • Nywele za binadamu zina kiwango kikubwa cha Keratin
  • Mbolea inayopatikana yaonesha mafanikio makubwa shambani
  • Ni utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa
Tweet URL
Methali ya “ganda la mua la jana chungu kaona kivuno,” imekuwa dhahiri  huko mkoani Kigoma, mkoa ulioko Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania ambako mtafiti Ibrahim Isaack Mnigambogi anaokota mabaki ya  nywele na kugeuza kuwa mbolea asilia, au kwa lugha ya kiingereza, “organic manure.”
 
Bwana Mnigambogi ambaye ni Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani humo, na pia hutumiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO) nchini Tanzania kutoa mafunzo kwa maafisa ugani anasema ubunifu huo unalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira huku ikiwasaidia wakulima kupata mbolea ya gharama nafuu.
 
Ubunifu huo, unaojulikana kwa jina la "Keratic Cycle", unatokana na juhudi za kutafuta matumizi bora ya taka za nywele ambazo mara nyingi hutupwa ovyo kwenye mitaro, madampo na njia za maji.
 
"Nilitaka kusaidia kutatua changamoto ya uchafuzi wa mazingira na kusaidia wakulima kupata mbolea kwa gharama nafuu na yenye tija ambayo inaweza kurutubisha udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao," amesema Mnigambogi.

Jinsi wazo lilivyozaliwa

Kwa mujibu wa Mnigambogi, aliona kuwa nywele zinazotupwa ovyo zina virutubisho muhimu ambavyo vinaweza kutumika katika kilimo.
Amesema nywele zina kiwango kikubwa cha keratin na naitrojeni, virutubisho ambavyo vina mchango mkubwa katika ukuaji wa mimea. Wakati huo huo, wakulima wengi wa Kasulu wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa rutuba ya udongo na gharama kubwa za mbolea za kawaida.
 
"Nywele haziozi kwa haraka kutokana na uwepo wa keratin, lakini zina virutubisho vingi vinavyoweza kusaidia mimea baada ya kuchakatwa," amesema.

Hatua 5 za kutengeneza mbolea ya nywele

1. Ukusanyaji wa nywele
  • Kukusanya mabaki ya nywele kutoka saluni, kwa vinyozi na kwenye madampo ya taka.
2. Usafishaji na usalama
  • Nywele husafishwa na kisha huchakatwa ili kuhakikisha ni salama kwa matumizi ya kilimo. Taka kama karatasi au udongo huondolewa.
Wanaume wawili nchini Tanzania wakichakata marundo ya biochar shambani ambayo ni mavumbi yanayopatikana baada ya kuchoma moto magunzi ya mahindi na pumba za mpunga.
UN News Wanaume wawili nchini Tanzania wakichakata marundo ya biochar shambani ambayo ni mavumbi yanayopatikana baada ya kuchoma moto magunzi ya mahindi na pumba za mpunga.
3. Uvunjaji wa Keratin
  • Nywele huyeyushwa kwa kutumia kemikali maalumu. Hapa Keratin huvunjwa na kubadilishwa kuwa virutubisho vinavyoweza kufyonzwa na mimea.
    • Virutubisho vinavyopatikana ni pamoja na: Naitrojeni; tindikali ya amino; Peptidi; Fosforasi na Potasiamu
4. Uandaaji wa mbolea
  • Kimiminika kinachotokana na nywele huchanganywa na biochar. Biochar ni vumbi linalopatikana baada ya kuchomwa kwa magunzi ya mahindi au pumba za mpunga Hii huhifadhi virutubisho, huongeza uwezo wa udongo kushikilia maji na pia huhifadhi hewa ya ukaa kwenye udongo.
5. Ufungaji na usambazaji
  • Mbolea huandaliwa kwa matumizi ya wakulima na huitumia kwenye Mbogamboga, mahindi, maharage na miti ya matunda
Wakati wa maonesho ya hivi karibuni ya sikukuu ya wakulima, Nane Nane nchini Tanzania, mtafiti Ibrahim alipata fursa ya kuonesha ubunifu wake wa kugeuza mabaki ya nywele za binadamu kuwa mbolea asilia.
UN News Wakati wa maonesho ya hivi karibuni ya siku ya wakulima, Nane Nane nchini Tanzania,baadhi ya wananchi walifika kwenye banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma kushuhudia mbolea itokanayo na mabaki ya nywele za binadamu.

Mradi unavyochangia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Bwana Mnigambogi amesema mradi huo unagusa malengo kadhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu.
SDG 6: Maji safi na usafi wa mazingira
  • Kuzuia nywele kuingia kwenye mitaro na njia za maji.
  • Kupunguza uchafuzi wa mazingira.
SDG 8: Ajira zenye staha na ukuaji wa uchumi
  • Kutoa ajira za kijani kwa vijana na wanawake.
  • Kukuza shughuli za ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa mbolea.
SDG 13: Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
  • Kupunguza kiasi cha taka kinachoishia kwenye madampo.
  • Kuimarisha matumizi ya rasilimali zinazoweza kurejelewa.
"Mradi huu unaweza kutoa ajira za kijani kwa vijana na wanawake katika ukusanyaji, uchakataji, ufungaji na ushauri wa kilimo," amesema.
Mfuko wa plastiki ulio wazi uliojaa mbolea ya kikaboni nyeusi iliyotengenezwa kwa kinyesi cha nywele za binadamu.
UN News Mbolea asilia iliyopatikana baada ya kugeuza mabaki ya nywele ya za binadamu kuwa mbolea.

Changamoto zinazoikabili teknolojia hiyo

Licha ya mafanikio yaliyoanza kuonekana, Bwana Mnigambogi amesema bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa malighafi kwa wingi  unaohitajika, kuelimisha wananchi kuhusu thamani ya nywele kama rasilimali na kuweka mfumo endelevu wa ukusanyaji kutoka saluni na vinyozi.

Je inatumika?

Afisa huyo amesema mbolea hiyo tayari imeanza kutumika na imeonesha matokeo mazuri katika mashamba ya wakulima. “Wakulima waliotumia mbolea hiyo wameanza kuona ongezeko la uzalishaji na kuboresha rutuba ya ardhi.”