Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 81 baada ya shambulio Hiroshima, UN yaonya kuhusu hatari ya silaha za nyuklia

Mtazamo wa usiku wa Kuba la Genbaku (Kuba la bomu) huko Hiroshima, Japani, likiwa na mwangaza wake majini.
© Unsplash/Alessandro Stech Taswira ya usiku ya Bustani ya Amani huko Hiroshima nchini Japani. Jengo hili liliharibiwa kwa kiasi kikubwa na bomu B-52 lililoangushwa na Marekani Agosti 6, 1945.

Miaka 81 baada ya shambulio Hiroshima, UN yaonya kuhusu hatari ya silaha za nyuklia

Amani na Usalama
  • Siku ya leo miaka 81 iliyopita Marekani iliangusha bomu la atomiki Hiroshima
  • Maelfu walikufa, madhara yake yaishi hadi leo
  • Guterres asihi dunia ichague amani badala ya hofu na mgawanyiko
Tweet URL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kuwa dunia inakabiliwa na ongezeko la hatari ya matumizi ya silaha za nyuklia kutokana na kuongezeka kwa migawanyiko ya kisiasa, kutokuaminiana na mashindano ya kijeshi. 

Ametoa ujumbe huo leo katika kumbukumbu ya miaka 81 tangu bomu la atomiki lilipoangushwa katika mji wa Hiroshima nchini Japan, ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Izumi Nakamitsu ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja ya Mataifa inayohusika na kuzuia kuenea kwa silaha.

“Wakati umefika kwa mataifa kuchagua njia ya mazungumzo, ushirikiano na upokonyaji wa silaha badala ya kutegemea nguvu za kijeshi ili kutatua mizozo,” amesema Katibu Mkuu.

Hiroshima bado ni somo kwa dunia

Guterres amesema miaka 81 iliyopita, Hiroshima iligeuzwa kuwa kifusi, maelfu ya watu wakapoteza maisha na dunia ikashuhudia kwa mara ya kwanza madhara mabaya ya vita vya nyuklia.

Amesema leo ni kuwakumbuka waliopoteza maisha na kuwaheshimu manusura wa shambulizi hilo, wanaojulikana kama hibakusha, ambao idadi yao inaendelea kupungua, lakini ujumbe wao wa amani unaendelea kuwa muhimu kwa dunia.

"Kumbukizi hii si siku ya kumbukumbu pekee, bali pia ni wakati wa kujiuliza kama tumejifunza kwa dhati kilichotokana na maafa ya Hiroshima, na kama ubinadamu utachagua mustakabali wa amani au utaendelea kuishi chini ya kivuli cha maangamizi ya nyuklia," amesema.

Mwanamume mzee aliyevaa koti la kahawia akizungumza na hadhira iliyoketi katika chumba cha mikutano.
UN/Jihye Shin Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani ya UN, jijini New York, Marekani

Onyo kuhusu kuongezeka kwa hatari ya nyuklia

Katibu Mkuu amesema mazingira ya sasa duniani yanazidi kuwa hatarishi kutokana na migogoro ya kisiasa na kuongezeka kwa mashindano ya kijeshi.

Mambo muhimu aliyoyaangazia

  • Migawanyiko ya kisiasa na kutokuaminiana kati ya mataifa inaongezeka.
  • Hatua zilizokuwa zikisaidia kuzuia maafa ya nyuklia zinaendelea kudhoofika.
  • Mwelekeo wa kupunguza idadi ya silaha za nyuklia uliodumu kwa miongo kadhaa umeanza kubadilika.
  • Kanuni za kimataifa zinazopinga majaribio ya silaha za nyuklia zinakabiliwa na changamoto.
  • Matumizi ya kijeshi duniani yalifikia dola trilioni 2.9 mwaka 2025.
  • Mataifa yanaendelea kutumia vitisho vya nyuklia kama njia ya kuonyesha nguvu na kushinikiza wengine.

Amani haiwezi kujengwa kwa vitisho

Kwa mujibu wa Guterres, somo la Hiroshima halihusu tu madhara ya silaha za nyuklia, bali pia umuhimu wa kujenga dunia ambayo matumizi au hata tishio la kutumia silaha hizo litakuwa jambo lisilokubalika.

"Amani hujengwa kwa kuaminiana, mazungumzo ya kudumu, diplomasia, ushirikiano wa kimataifa na kuheshimu sheria za kimataifa."

Aidha, amezitaka nchi zote, hususan zile zenye silaha za nyuklia, kuchukua hatua za kupunguza hatari, kurejesha imani na kuharakisha juhudi za kuondoa kabisa silaha hizo.

Picha nyeusi na nyeupe ya kihistoria ya raia watatu wa Japani, ambao huenda wamenusurika bomu la atomiki la Hiroshima, ambao wamepokea huduma ya matibabu.
UN Photo/Hajime Miyatake Manusura wa bomu la Hiroshima ambao walikuwa wamepatiwa matibabu

Wito wa kuimarisha upokonyaji wa silaha

Katibu Mkuu amesema mfumo wa kimataifa wa upokonyaji silaha unahitaji kuimarishwa zaidi, huku akipinga dhana kwamba silaha za nyuklia ndizo dhamana kuu ya usalama wa taifa.

Amesema badala yake, silaha hizo ndizo zinazoendelea kuhatarisha usalama wa dunia.

Hatua zinazohitajika

  • Kuimarisha mazungumzo ya kimataifa.
  • Kupanua ushirikiano wa kidiplomasia.
  • Kuheshimu sheria za kimataifa.
  • Kupunguza hatari zinazohusiana na silaha za nyuklia.
  • Kuendeleza upokonyaji kamili wa silaha za nyuklia.

Ahadi ya Umoja wa Mataifa bado haijatimia

Guterres amekumbusha kuwa Umoja wa Mataifa ulianzishwa kwa lengo la kuiondoa dunia katika janga la vita, na kwamba azimio la kwanza kabisa la Baraza Kuu mwaka 1946 lilitaka kuondolewa kwa silaha za nyuklia.

Amesema ingawa ahadi hiyo bado haijatekelezwa kikamilifu, bado inawezekana kufikiwa ikiwa kutakuwepo dhamira ya kisiasa na ushirikiano wa kimataifa.

Mtazamo wa angani wa Kuba la Bomu la Atomiki na Mto Naka huko Hiroshima, Japani, ukiwa na mashua ya watalii juu ya maji na anga ya jiji la kisasa nyuma.
© Unsplash/Desmond Tawiah Bustani ya kumbukumbu ya amani ya Hiroshima ambako bomu la atomiki lilianguka kusini mwa Japan

Hiroshima ni alama ya matumaini

Katibu Mkuu amesema pamoja na historia yake ya maafa, Hiroshima leo ni mfano wa ustahimilivu, kujijenga upya na matumaini.

Kwa mujibu wake, wakazi wa mji huo wameendelea kuikumbusha dunia kwamba hata baada ya kipindi kigumu zaidi, bado ubinadamu unaweza kuchagua na kujenga mustakabali tofauti.