Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL bado ni tishio kubwa barani Afrika laonya Baraza la Usalama la UN

Oguljeren Niyazberdiyeva akizungumza jukwaani wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama UN mjini New York.
Picha ya UN/Eskinder Debebe Oguljeren Niyazberdiyeva, Mkuu wa Ofisi ya Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Ofisi ya UN ya Kupambana na Ugaidi, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa vinavyosababishwa na vitendo vya kigaidi.

ISIL bado ni tishio kubwa barani Afrika laonya Baraza la Usalama la UN

Amani na Usalama
  • Baraza la Usalama la UN laonya kuwa ISIL/Da’esh bado ni tishio kubwa duniani. 
  • Afrika, hususan Sahel na Bonde la Ziwa Chad, imetajwa kuwa eneo lenye hatari kubwa zaidi. 
  • ISWAP ni tawi lenye shughuli nyingi zaidi duniani na linaendelea kutumia teknolojia mpya ikiwemo ndege zisizo na rubani. 
  • UN imeonya kuhusu matumizi ya AI, mawasiliano, majukwaa ya kidijitali na propaganda kama nyenzo za kuimarisha ugaidi. 
  • Wajumbe wa Baraza wametaka ushirikiano wa kimataifa na udhibiti bora wa teknolojia mpya ili kuzuia makundi yenye msimamo mkali.

Kundi la kigaidi la ISIL/Da'esh bado ni tishio kubwa kwa usalama wa kimataifa licha ya operesheni za kupambana na ugaidi zilizodhoofisha uongozi wake wa juu limeonya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Onyo hilo limetolewa Jumatano wajumbe wa Baraza hilo walipokutana jijini New York Marekani kupitia ripoti ya 23 ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kundi hilo, ambapo wameelezwa kuwa ISIL imeendelea kujibadilisha na kuimarisha mitandao yake, huku Afrika, hususan ukanda wa Sahel na Bonde la Ziwa Chad, ikitajwa kuwa eneo linalokabiliwa na hatari kubwa zaidi.

Akizungumza mbele ya Baraza hilo, Mkuu wa Ofisi ya Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi, Oguljeren Niyazberdiyeva, amesema licha ya mafanikio ya operesheni za kijeshi dhidi ya viongozi wa kundi hilo, bado linaendelea kuwa imara.

 "Ingawa operesheni endelevu za kupambana na ugaidi zimevuruga uongozi wa juu wa Da'esh na kupunguza uwezo wake wa kuongoza mashambulizi kutoka katikati, kundi hilo limeendelea kujibadilisha. Muundo wake umeenea zaidi, lakini washirika wake bado wameunganishwa na itikadi moja," amesema.

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama UN mjini New York.
Picha ya UN/Manuel Elías Baraza la Usalama la UN linakutana kujadili vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa vinavyosababishwa na vitendo vya kigaidi.

Afrika yabeba mzigo mkubwa wa tishio

Niyazberdiyeva amesema tishio kubwa zaidi sasa linaonekana barani Afrika ambako matawi ya ISIL yanaendelea kupanua uwezo wake wa kivita na kutumia teknolojia mpya. "Leo hii tishio ni kubwa zaidi liko katika maeneo ya Afrika, hususan Sahel na Bonde la Ziwa Chad, ambako matawi kadhaa yanaendelea kuimarisha uwezo wao, kupanua maeneo ya operesheni na kubadili mbinu zao"

Ameongeza kuwa tawi la ISIL Ukanda wa Afrika Magharibi (ISWAP) ndilo lenye shughuli nyingi zaidi duniani na sasa linaonesha uwezo mkubwa wa kupata na kutumia ndege zisizo na rubani za kibiashara. 

Kuhusu Iraq, alisema mafanikio yaliyopatikana dhidi ya ISIL yanapaswa kulindwa kwa kuimarisha taasisi za serikali, mfumo wa haki, pamoja na mipango ya kuwajumuisha tena waliokuwa wanamgambo katika jamii.

Akili mnemba na dijitali vyabadilisha sura ya ugaidi

Afisa huyo pia ameonya kuhusu matumizi makubwa ya teknolojia mpya na kundi hilo, akisema matumizi ya akili mnemba (AI), mawasiliano yaliyosimbwa, majukwaa ya kidijitali, mali pepe na ndege zisizo na rubani yanahitaji usimamizi madhubuti wa kimataifa. "Hakuna nchi mwanachama inayoweza kukabiliana na tishio hili peke yake," amesema, akisisitiza kuwa "tishio linalotokana na Da'esh litaendelea kubadilika, na hivyo mwitikio wetu wa pamoja lazima ubadilike pia." 

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Carmen G. Cantor wa CTED ahutubia Baraza la Usalama UN kuhusu vitisho vinavyotokana na vitendo vya kigaidi.
Picha ya UN/Manuel Elías Carmen G. Cantor, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kurugenzi ya Utendaji ya Kamati ya Kupambana na Ugaidi (CTED), akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa vinavyosababishwa na vitendo vya kigaidi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kurugenzi ya Kamati ya Kupambana na Ugaidi (CTED), Carmen G. Cantor, amesema propaganda za Da'esh sasa zimegeuka kuwa silaha ya moja kwa moja ya operesheni. 

"Propaganda si tena suala la kuunda simulizi pekee, sasa ni nyenzo inayowezesha makundi ya kigaidi kuajiri wanachama, kukusanya rasilimali na kupanua shughuli zao kuvuka mipaka".

Wajumbe watofautiana kuhusu vitisho vingine 

Katika mjadala huo, baadhi ya wajumbe walielekeza hoja zao kwenye vitisho vingine vinavyoathiri usalama wa kimataifa. 

Naibu Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Tammy Bruce, amesema makundi yanayoungwa mkono na Iran, yakiwemo Houthis, Hezbollah, Hamas na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq, yanaendelea kudhoofisha utulivu wa Mashariki ya Kati na kwamba ushirikiano wa kimataifa katika kubadilishana taarifa ni muhimu ili kuyazuia kupata silaha hatari. 

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi, Vasily Nebenzya, amedai kuwa shughuli za ugaidi zinazohusishwa na utawala wa Kyiv barani Afrika zinahitaji kuchunguzwa tofauti, huku Naibu Mwakilishi wa China, Sun Lei, akitaka kuimarishwa kwa utawala wa kimataifa wa teknolojia mpya ili kuzuia makundi yenye msimamo mkali kutumia maendeleo hayo kueneza ugaidi na misimamo mikali. 

Amesisitiza pia umuhimu wa kusaidia nchi zinazoendelea kupitia uhamishaji wa teknolojia, mafunzo na kubadilishana taarifa ili kuimarisha uwezo wao wa kupambana na ugaidi.