Mashambulizi mapya ya Urusi Ukraine yaua raia 17, UN yataka ulinzi wa haraka kwa kuwanusuru
Wimbi jipya la mashambulizi makubwa ya Urusi dhidi ya Ukraine yaliyosababisha vifo vya raia na majeruhi wengi, limelaaniwa vikali na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matthias Schmale, akisisitiza kuwa raia lazima walindwe kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Mashambulizi hayo ya usiku yaliyoanza mwezi huu wa Agosti yamekuja baada ya mwezi Julai kuwa mwezi ulioshuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia nchini Ukraine tangu Aprili mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 12 wameuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyolenga Mkoa wa Kyiv na Jiji la Kyiv, huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kutafuta manusura chini ya vifusi na wahudumu wa kibinadamu wakitoa msaada kwa waathirika.
"Baada ya mwezi uliokuwa mbaya zaidi kwa raia tangu Aprili 2022, mwezi Agosti umeanza kwa mashambulizi makubwa yaliyokatiza maisha ya watu wasio na hatia. Raia kote Ukraine wanapaswa kuishi, kufanya kazi na kulea watoto wao bila hofu ya mashambulizi mapya," amesema Matthias Schmale.
Watoto ni miongoni mwa waathirika wakubwa
Mbali na Kyiv, mashambulizi ya anga na ndege zisizo na rubani yameripotiwa katika miji ya Kramatorsk, Kherson na Zaporizhzhia, yakisababisha vifo na majeruhi kwa makumi ya watu, wakiwemo watoto.
Mashambulizi hayo pia yameharibu nyumba, shule, magari ya usafiri wa umma, mifumo ya maji pamoja na maghala ya misaada ya kibinadamu, hali inayozidisha mateso kwa familia ambazo tayari zimepoteza makazi au zinalazimika kuhama mara kwa mara.
Schmale amesema kuendelea kwa mashambulizi hayo kunawaacha maelfu ya wananchi wakiwa wamevunjika moyo, wamefurushwa makwao au wakihangaika kujenga upya maisha yao.
HRMMU: Vifo vya raia yaongezeka
Wakati huo huo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Binadamu nchini Ukraine (HRMMU) umeeleza kuwa mashambulizi makubwa ya usiku wa kuamkia leo tarehe 5 Agosti yanathibitisha mwenendo unaoongeza idadi ya vifo vya raia nchini humo.
Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, watu wasiopungua 17 wameuawa na wengine 44 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani yaliyolenga hasa Kyiv na maeneo yanayozunguka mji huo. Miongoni mwa waliouawa ni watu waliokuwa kwenye jukwaa la kituo cha reli katika wilaya ya Brovarskyi, mkoani Kyiv.
Mkuu wa HRMMU, Danielle Bell, amesema mashambulizi hayo ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi makubwa yaliyoikumba Kyiv katika kipindi chote cha majira ya joto.
"Shambulio hili la karibuni ni sehemu ya msimu wa kiangazi uliogubikwa na mashambulizi makubwa ya mara kwa mara dhidi ya Kyiv yenye madhara makubwa kwa raia. Kuongezeka kwa matumizi ya makombora ya balistiki na silaha nyingine za masafa marefu katika maeneo yenye watu wengi kunachangia kuongezeka kwa vifo vya raia na uharibifu mkubwa wa nyumba, biashara na miundombinu mingine ya kiraia," amesema Bell.
Sheria za kimataifa ziheshimiwe
Umoja wa Mataifa umekumbusha kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu zinazitaka pande zote zinazohusika katika mapigano kuchukua tahadhari zote zinazowezekana kulinda raia na miundombinu ya kiraia.
Shirika hilo limetoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi yanayowaweka wananchi hatarini, likisisitiza kuwa raia wa Ukraine wana haki ya kuishi kwa usalama bila hofu ya mashambulizi ya kila siku.