Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya ebola DRC kufunguliwa wiki hii jimboni Ituri

Wafanyakazi wa matibabu wa WHO wakiwa wamevaa vifaa kamili vya kujikinga wakisafirisha machela karibu na ambulensi katika eneo la ujenzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO/Josua Mulala Raymond Mhudumu wa afya akiwa amebeba machela kuelekea kituo kipya cha matibabu ya Ebola jimboni Ituri, nchini DR Congo.

Kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya ebola DRC kufunguliwa wiki hii jimboni Ituri

Afya
  • Kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 
  • Kinalenga kuimarisha mapambano dhidi ya mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC
  • Wahudumu wa afya watakuwa zaidi ya 300

Kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),  kinafunguliwa wiki hii na wadau wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha mwitikio dhidi ya mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo unaoendelea katika jimbo la Ituri, mashariki mwa  taifa hilo.

Kituo hicho kipya kilichojengwa eneo la Rwankole, takribani kilomita tano kutoka makazi ya wakimbizi ya Kigonze, jimboni Ituri, kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 na kinatarajiwa kuongeza uwezo wa mfumo wa afya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa.

Picha ya WHO inayoonyesha takwimu za mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufikia Julai 30, 2026, ikijumuisha idadi ya visa, vifo, maeneo yaliyoathiriwa, na viwango vya chanjo.
WHO Taarifa za WHO kuhusu Mlipuko wa Ebola nchini DRC kufikia Julai 2026

Kituo cha mpito cha Ebola kinaendelea kupokea washukiwa

Wakati maandalizi ya ufunguzi wa kituo kipya kinachojengwa na Shirika la International Medical Corps (IMC),kituo cha Mpito cha Ebola cha Kigonze kinaendelea kuwa sehemu ya kwanza ya uchunguzi na uangalizi wa wagonjwa wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola.

Daktari Francis Bigirimwami Chibanvunya amesema wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola hutengwa mara moja na kufanyiwa vipimo kabla ya kuhamishiwa kwenye kituo cha matibabu endapo maambukizi yatathibitishwa.

Kwa mujibu wa daktari huyo:
  • Kituo kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 8 kwa wakati mmoja.
  • Sampuli za wagonjwa huchukuliwa mara moja kwa ajili ya vipimo.
  • Wagonjwa hupimwa mara mbili ndani ya kipindi cha saa 48 kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani ikiwa hawana Ebola.
  • Kwa sasa wagonjwa wanne wamewekwa kwenye eneo la kutengwa.

Miongoni mwa wagonjwa hao ni mtoto mwenye umri wa miaka miwili ambaye baba yake alifariki kutokana na Ebola. Mtoto huyo ameonesha dalili za homa, kuharisha na kutapika na kwa sasa anasubiri majibu ya vipimo ili kubaini kama ameambukizwa virusi hivyo.

Hatua kali za kudhibiti maambukizi

Katika Kituo cha Mpito cha Kigonze, hatua za kuzuia maambukizi zinaendelea kutekelezwa kwa umakini. Wahudumu husafisha na kufua mavazi ya kitabibu kwa kufuata taratibu maalumu, huku kunawa mikono na matumizi ya vifaa vya kujikinga vikiendelea kuwa sehemu muhimu ya huduma zinazotolewa.

Afisa wa Mawasiliano wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), Ramatoulaye Moussa Mazou, amesema  OCHA inaendelea kuratibu mashirika ya kibinadamu na kuhakikisha fedha za dharura zinapatikana kwa haraka ili kuimarisha mwitikio wa Ebola.

Kituo kipya kuongeza uwezo wa matibabu

Katika eneo la Rwankole, mafundi wanafanya kazi za mwisho za kukamilisha kituo kipya cha matibabu kabla ya kufunguliwa rasmi wiki hii.

Kwa mujibu wa IMC, kituo hicho kitakuwa na:
  • Uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100.
  • Vitanda 60 kwa wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.
  • Vitanda 40 kwa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi.
  • Mabanda manne ya wagonjwa, mawili kwa wanaume na mawili kwa wanawake.
  • Vyumba vya mtu mmoja mmoja vyenye bafu na choo binafsi.
  • Zaidi ya wahudumu 300 wa afya na huduma za usaidizi.

Daktari Sambo Sidikou wa IMC amesema ushirikiano wa jamii katika kutambua wagonjwa mapema utakuwa muhimu ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Huduma maalumu kwa wajawazito

Kutokana na uzoefu wa mlipuko wa sasa, wataalamu wa afya wamebaini kuwa virusi vya Ebola vinaweza kuongeza hatari ya kutoka kwa mimba, mimba kuharibika na kujifungua kabla ya wakati.

Kutokana na hali hiyo, kituo kipya kimeanzisha:
  • Wodi maalumu kwa wajawazito wanaoshukiwa kuwa na Ebola.
  • Wodi tofauti kwa wajawazito waliothibitishwa kuwa na maambukizi.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanawake wajawazito wanapata huduma salama na maalumu huku ikipunguza hatari ya maambukizi ndani ya vituo vya afya.

Maafisa wa afya wanaamini kuwa kufunguliwa kwa kituo hiki kutaimarisha uwezo wa DRC kukabiliana na mlipuko wa sasa wa Ebola na kuongeza nafasi ya wagonjwa kupata huduma kwa wakati, huku Kituo cha Mpito cha Kigonze kikiendelea kuwa lango muhimu la uchunguzi, utambuzi wa mapema na rufaa za wagonjwa.