Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Sudan tishio kubwa kwa wakulima

Kundi la wanawake, wakiwemo wakimbizi wa ndani na wakimbizi wa Eritrea, wakitembea katika mashamba ya bamia katika kijiji cha Um Al-Khair, Sudan.
© UNOCHA/Giles Clarke Wakulima wanawake katika eneo la kati-mashariki mwa Sudan (Picha ya mataba)

Vita Sudan tishio kubwa kwa wakulima

Amani na Usalama

· Asilimia 90 ya wakulima wamepata upungufu wa mazao

· Uzalishaji umeshuka kati ya asilimia 22 hadi 71 

· Zaidi ya asilimia 70 ya wakulima hawapati mikopo

Ripoti mpya ya Uchambuzi wa Mnepo wa Kilimo na Masoko wa Sudan, iliyotolewa Agosti 4 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na Kituo cha Kimataifa cha Biashara (ITC), inaonesha kuwa sekta ya kilimo bado ina uwezo mkubwa wa kuimarisha uhakika wa chakula na uchumi wa Sudan, endapo itapata uwekezaji wa haraka.

Mavuno yaporomoka, biashara yadorora

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, iliyotokana na takwimu za majimbo mbalimbali na mashauriano zaidi ya 80 na wadau tofauti, uzalishaji umepungua kati ya asilimia 22 na 71 kutegemea ukubwa wa mapigano eneo husika, huku zaidi ya nusu ya wakulima wakishindwa kuvuna kwa usalama. Gharama za biashara zimepanda kwa asilimia 40, na biashara ya mipakani imeshuka kwa asilimia 45, huku minyororo ya usambazaji ikivunjika na bei za chakula kupaa maradufu katika baadhi ya maeneo.

Upatikanaji wa mikopo na taarifa waendelea kuwa changamoto

Ripoti inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wakulima na wafanyabiashara wadogo hawana uwezo wa kupata mikopo, huku asilimia 80 wakikosa taarifa muhimu za masoko.

Fursa bado ipo

Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Sudan, Luca Renda, amesema licha ya uharibifu mkubwa, sekta ya kilimo inaweza kurejeshwa iwapo wakulima na masoko watapewa uwekezaji wa dharura utakaowezesha upatikanaji wa chakula kwa bei nafuu.

Ripoti inapendekeza kuimarisha minyororo saba ya thamani, ufuta, mtama, soya, karanga, mchaichai, utomvu wa mpingo na mifugo  pamoja na kuboresha miundombinu ya masoko, kupunguza vikwazo vya biashara, na kuwawezesha wanawake, vijana na watu waliohama makazi wanaotawala masoko yasiyo rasmi.

UNDP na programu ya mafunzo ya Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) zinasisitiza kuwa uwekezaji katika kilimo na biashara ni msingi muhimu wa kufufua uchumi wa Sudan na kuimarisha usalama wa chakula kwa mamilioni ya wananchi.