Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za Rwanda kujikinga na Ebola zaungwa mkono na Umoja wa Mataifa

Mfanyakazi wa afya wa jamii wa kiume aliyevaa sare ya bluu akimpa mtoto mdogo aliyeshikiliwa na mama kwenye benchi nje ya kituo cha afya nchini Rwanda. Mfanyakazi mwingine wa afya aliyevaa scrub ya bluu anaandika maelezo karibu.
© WHO/Isaac Rudakubana WHO imekuwa ikiunga mkono Mpango wa Afya kwa Wote nchini Rwanda, kwa kusaidia familia kutokomeza magonjwa ya kitropiki na malaria kwa watoto na kinamama. (PICHA YA MAKTABA)

Juhudi za Rwanda kujikinga na Ebola zaungwa mkono na Umoja wa Mataifa

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) limesema Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaendelea kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Serikali ya Rwanda za kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na Ebola.

Juhudi hizo zinajumuisha ufuatiliaji katika vituo vya afya, kwenye jamii na mipakani. Zaidi ya wahudumu 100 wametumwa katika maeneo muhimu ya kuvuka mipaka kwa njia ya nchi kavu na kwenye viwanja vya ndege.
Juhudi za kuimarisha mifumo ya maji na usafi wa mazingira zinaendelea katika vituo vya afya na shule katika wilaya zilizo hatarini zaidi, zikilenga kuboresha upatikanaji wa maji, huduma za usafi wa mazingira na usimamizi wa taka.

Sio nchi kavu na anga pekee

Katika maeneo muhimu ya kuingilia nchini, yakiwemo vivuko vya Rubavu na Kagitumba, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanasaidia kuboresha huduma za kunawa mikono, upatikanaji wa maji salama, mifumo ya usafi wa mazingira na usimamizi wa maji taka.

Mafunzo

Pia, Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaunga mkono mafunzo katika vituo 11 vya afya katika eneo la Mibilizi, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Takribani wahudumu 400 walio mstari wa mbele wanapatiwa mafunzo kuhusu utambuzi wa mapema wa ugonjwa, uchunguzi na upangaji wa wagonjwa kulingana na hali zao, kinga na udhibiti wa maambukizi, usimamizi wa taka, mazishi salama na yenye heshima, pamoja na utoaji wa ujumbe wa afya ya umma.