Lenacapavir: Dawa mpya ya kujikinga na VVU yawapa matumaini vijana Afrika Kusini
Lenacapavir: Dawa mpya ya kujikinga na VVU yawapa matumaini vijana Afrika Kusini
Kwa mara ya kwanza, mtu anaweza kujikinga na Virusi Vya Ukimwi, VVU, kwa sindano moja tu kila baada ya miezi sita bila kumeza kidonge kila siku. Dawa hiyo iitwayo Lenacapavir.
Katika kijiji cha Philippi, viungani mwa jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini. Picha zilizopigwa kutoka juu zinaonesha chini nyumba za mabati zikiwa zimesongamana, na katikati ya eneo la maegesho ya magari, kliniki tembezi zimepangwa. Nje ya mlango kuna bango lililoandikwa, "FAST PrEP – usichelewe, jikinge leo."
Ndani ya kliniki hiyo, muuguzi amevaa glavu, akiandaa sindano. Kwenye meza kando yake kuna kijitabu cha kinga, vipeperushi na kisanduku cha dawa.
Muuguzi Zimasa Zwide, anayefanya kazi katika kliniki hiyo tembezi ya Philippi, anaeleza kwa nini kinga hii ya VVU ni muhimu hasa kwa wasichana na wanawake vijana.
"Kuna wimbi kubwa la ukatili wa kijinsia, ambapo wanawake vijana wanashambuliwa, na wengi wao wanajikuta katika hatari ya maambukizi kupitia ubakaji. Kwa hiyo tunawahimiza wajikinge muda wote, ili hata kama mtu akibakwa, angalau kwa upande wa VVU awe salama zaidi."
Mratibu wa Mawasiliano wa Taasisi ya Afya ya Desmond Tutu, Mbali Jonas, anasema jamii imepokea habari hii kwa shauku kubwa kwani, "Kuna furaha kubwa sana ndani ya jamii. Sindano hii ya LEN imetambulika kama mabadiliko makubwa katika kukabiliana na janga la VVU, hasa kwa vijana, kwa sababu inakupa usiri.Unapata sindano mbili kwa mwaka, na umemaliza."
Nje ya kliniki, kundi la vijana limekaa kwenye mkutano wa elimu ya afya na kinga dhidi ya VVU, mkutano ukiongozwa na Sive Mphambaniso.
Wanawake wanne wananyoosha mikono, wawili kati yao ni miongoni mwa waliokwisha kupata Lenacapavir (dawa ya muda mrefu ya kuzuia na kutibu maambukizi ya VVU).
Wanajadiliana kwa sauti, wakiulizana maswali. Lakini Mphambaniso anasema bado kuna pengo kubwa la uelewa."Ninapokwenda kwenye jamii, nikiwaeleza watu mambo haya, wengine wanashangaa sana. Naamini hawana taarifa za kutosha kama inavyopaswa. Kwa sababu baadhi ya watu wanajihusisha na ngono bila kujua kinachoweza kutokea, wala madhara ya ngono zisizo salama. Na njia zote hizi tulizo nazo, wengi wao hawazijui."
Hapa ndipo penye changamoto. Afrika Kusini ina watu milioni nane wanaoishi na VVU, na kila mwaka bado kunakuwa na maambukizi mapya yanayofikia takriban laki moja na sabini elfu. Lakini dozi zilizopo kwa sasa ni laki nne na hamsini elfu tu.
Mkurugenzi wa Kituo cha VVU cha Desmond Tutu, Profesa Linda-Gail Bekker, anasema hilo linaibua swali zito kwani "Hili linaibua swali kubwa. Hii ni nchi ambayo watu milioni nane wanaishi na VVU. Bado tunaona maambukizi mapya yapatayo laki moja na themanini elfu kila mwaka. Tunahitaji kuifikisha kinga hii kwa watu wengi zaidi ya laki nne na hamsini elfu. Kwa hiyo, itabidi tuwe wachaguzi kuhusu nani apate Lenacapavir."
Tunahamia mji wa Secunda, jimbo la Mpumalanga. Umati umejaa nje ya kliniki, ukisubiri kuwasili kwa Rais wa Afrika Kusini na Waziri wa Afya, kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Lenacapavir. Rais Cyril Ramaphosa anapanda jukwaani na kusema, "Usalama wa afya hauwezi tena kutenganishwa na maendeleo ya kiuchumi. Uwezo wa kubuni, kutengeneza na kusambaza dawa ni jambo la msingi kwa mamlaka yetu, ustahimilivu wetu na ustawi wetu. Kwa hiyo tuwe wazi Lenacapavir si suluhisho la kila kitu. Ni silaha moja zaidi yenye nguvu katika ghala letu."
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Gilead Sciences inayotengeneza dawa hiyo, Daniel O'Day, anasema kasi ya kuifikisha dawa hii barani Afrika haijawahi kushuhudiwa.
"Lenacapavir ni dawa mpya ya kwanza ya aina yake ya VVU kufika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara katika mwaka ule ule ilipoidhinishwa Marekani. Hili halijawahi kufanyika. Na hili ni jambo ambalo sisi Gilead tulidhamiria kulifikia mara tu tulipojua ufanisi wa Lenacapavir katika kutokomeza VVU."
Mwakilishi wa UNAIDS nchini Afrika Kusini, Alankar Malviya, anasisitiza kuwa dawa hii ni sehemu tu ya mkakati mpana kwa kuwa "Inatupatia mojawapo ya njia bora zaidi za kuwalinda vijana dhidi ya maambukizi mapya. Lakini kwa kuwa itatolewa kwa awamu, ni muhimu kutambua kuwa hii ni sehemu ya zana nyingi tulizo nazo za kuzuia maambukizi mapya, sambamba na kondomu, vidonge vya kujikinga na njia nyingine, ili kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030."
Video inahitimisha kwa picha ya Rais akiwa na Waziri wa Afya wakiinua masanduku ya dawa ya Lenacapavir juu, huku umati ukishangilia. Matumaini ni makubwa lakini swali la bei, uzalishaji na usambazaji bado liko wazi.