Angola yaimarisha mkakati wake wa kutokomeza ugonjwa hatari wa Polio
Angola yaimarisha mkakati wake wa kutokomeza ugonjwa hatari wa Polio
Baada ya kufanikisha kampeni mbili za kitaifa za chanjo dhidi ya polio na kampeni mbili za pamoja kwa kushirikiana na Namibia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC zilizowafikia zaidi ya watoto milioni tisa wenye umri chini ya miaka mitano, Angola sasa inaimarisha mkakati wake wa kutokomeza ugonjwa huo kwa kutumia mafunzo kuboresha kampeni zijazo na huduma za kawaida za chanjo.
Warsha ya Kitaifa ya Tathmini ya Kampeni za Chanjo, iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa Afya Duniani (WHO) na wadau wengine, ilichambua matokeo ya kampeni zilizofanyika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026 ili kubaini mafanikio, changamoto na hatua za kuimarisha utoaji wa chanjo.
Kwa muda wa siku tatu, washiriki walitathmini takwimu za chanjo, ubora wa kampeni, ufuatiliaji wa magonjwa, usimamizi wa vifaa, pamoja na shughuli za uhamasishaji wa jamii. Tathmini hiyo ilibaini umuhimu wa kuimarisha matumizi ya takwimu katika maamuzi, kuwafikia watoto ambao hawajapata chanjo na kuboresha huduma katika maeneo ya mbali.
Warsha hiyo pia ilisisitiza kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa wagonjwa wenye kupooza ghafla kwa misuli bila kukakamaa kwa lugha ya kitabibu Acute Flaccid Paralysis (AFP) na ufuatiliaji wa mazingira ili kubaini mapema uwepo wa virusi vya polio na kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa.
Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Chanjo, Dkt. Alda de Morais, anasema, "tumejizatiti kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki bila chanjo na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika kutokomeza polio."
Naye Mratibu wa Mpango wa Kimataifa wa Kutokomeza Polio nchini Angola, Dkt. Nirakar Panda, anasisitiza akisema, "kutokomeza polio kunahitaji kutumia ushahidi na takwimu kugeuza maarifa kuwa hatua halisi za kulinda watoto wote."
Warsha hiyo ilikubaliana kuandaa mpango wa kitaifa wa utekelezaji wenye mapendekezo ya kipaumbele, majukumu na muda wa utekelezaji ili kuboresha kampeni za chanjo, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuharakisha safari ya Angola kuelekea kutokomeza kabisa ugonjwa wa polio.