Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Muuguzi wa lishe hupima mzingo wa katikati ya mkono wa juu (MUAC) wa mtoto wa miezi 8 anayeitwa Satayesh katika kliniki ya afya huko Herat, Afghanistan.

Kwa watoto wachanga Afghanistani, mlo kamilifu ni anasa, washindia chai na mkate- WFP

© UNICEF Mtoto mchanga anachunguzwa utapiamlo katika kliniki huko Herat, nchini Afghanistan.

Kwa watoto wachanga Afghanistani, mlo kamilifu ni anasa, washindia chai na mkate- WFP

Msaada wa Kibinadamu
  • Migogoro lukuki yahatarisha uhai wa watoto
  • Mama mmoja asema bila msaada wa WFP watoto wake watakufa
  • Mama na mtoto 1 kati ya 7 ndio wanapatiwa msaada
  • Bila ufadhili hali itazidi kuwa tete
Tweet URL

Hali ya upatikanaji wa chakula nchini Afghanistani ni tete hivi sasa kwani watoto badala ya kunyweshwa maziwa ya mama au badala ya kula vyakula vyenye virutubisho, wanashindia chai hafifu na mkate.

Amesema Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani (WFP) John Aylieff wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kutokea mji mkuu wa taifa hilo la Asia, Kabul.

Bwana Aylieff amezungumzia mama mmoja aitwaye Farida waliyekutana naye walipotembela jimbo la Kandahar, akisema, “tulipozungumza na Farida, mtoto wake alianza kulia kwa sababu ya njaa. Aliingiza mkono kwenye begi lake na kutoa chupa, chupa ya mtoto. Sasa kwa kawaida unatarajia kuona imejaa maziwa. Lakini hii ilikuwa ina chai hafifu. Hakuna fedha kabisa kwa kaya kununua maziwa.”

Masaibu ya Farida

Farida, ni mama wa watoto watatu ambaye maisha yake yanaakisi mateso ya familia nyingi maskini nchini humo.  Mume wake ambaye ana umri mkubwa, ni mchuuzi wa bidhaa mitaani na hupata chini ya dola moja kwa siku, hali inayowafanya washindwe kumudu chakula chenye lishe, huduma za afya na mahitaji mengine muhimu.

Watoto wawili wa Farida wanaugua upungufu wa damu, huku mtoto wake wa miaka sita akiwa dhaifu kiasi kwamba ameshindwa kuhudhuria shule kwa miezi kadhaa kutokana na utapiamlo mkali.

Farida ameieleza WFP kuwa mara kwa mara hulazimika kuwaambia watoto wake kuwa hakuna chakula kingine. Familia hiyo inaendelea kuishi kwa chai na mkate pekee

"Huo ni ujumbe mgumu kuusikia," amesema Bwana. Aylieff. "Lakini ni mgumu zaidi unapogundua kuwa mwaka huu WFP imepata fedha za kuwasaidia mwanamke na mtoto mmoja tu kati ya 7  wenye utapiamlo mkali. Hii ina maana tunawalazimika kuwarudisha sita kati ya saba bila msaada wowote."

Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa Afghanistan

Afisa huyo amesema kwa sasa raia milioni 14 nchini Afghanistan wanakabiliwa na njaa, wakiwemo watoto wachanga ambao wazazi wao maskini na waliokata tamaa kama vile Farida wanawapatia milo hafifu.

Katika tahadhari mpya iliyotolewa Jumanne, WFP inasema kwamba Muafghanistani mmoja kati ya watatu kwa sasa anakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku shirika hilo likikosa rasilimali za kutosha kudhibiti hali hiyo inayozidi kuwa mbaya.

Kwa sasa, majimbo 12 yamefikia viwango vya kutisha vya utapiamlo mkali kwa watoto, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.

Je nini visababishi?

  • Migogoro, mathalani Mashariki ya Kati
  • Ukosefu mkubwa wa ajira, 
  • Ongezeko la bei za vyakula,
  • Kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu 
  • Kuvurugika kwa njia za usambazaji wa bidhaa 
  • Kurejea kwa Waafghanistan milioni sita waliorejeshwa kwa lazima, hasa kutoka Pakistan na Iran tangu Septemba 2023, kumeongeza mzigo kwa uchumi wa nchi ambao tayari ni dhaifu.

Kadiri pengo la ufadhili linavyoendelea kuongezeka, programu za lishe zinazookoa maisha zinaendelea kupunguzwa wakati ambapo mahitaji yanafikia kiwango cha juu zaidi.

Watoto wachanga wako katika hatari zaidi

Udumavu mkali unaotokana na utapiamlo—aina hatari zaidi ya utapiamlo—umefikia viwango vya kutisha katika theluthi moja ya majimbo ya Afghanistan.

"Idadi ya watoto wanaokimbizwa kwenye vituo vya afya inaongezeka kwa kasi na tunaiona wazi. Asilimia 80 ya wagonjwa walio katika hali mbaya zaidi ni watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaripoti kuwa wengi wao wanafikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa mno kuokolewa," ameonya Bw. Aylieff.

Soma taarifa nzima hapa