Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajawazito Sudan wasema wakunga wanaotoa huduma za kiutu Sudan wamewaokoa

Mwanamke wa Sudan anayetabasamu akiwa amembeba mtoto mchanga kwenye kibanda rahisi katika kambi ya wakimbizi katika Jimbo la Blue Nile, Sudan.
© UNFPA Sudan Mama akiwa amembeba mtoto mchanga katika kambi ya wakimbizi wa ndani jimboni Blue Nile nchini Sudan.

Wajawazito Sudan wasema wakunga wanaotoa huduma za kiutu Sudan wamewaokoa

Afya
  • Wakunga wamenusuru maisha ya wajawazito 
  • Hutoa huduma za dharura na wanufaika watoa mifano
  • Uwekezaji kwa wakunga ni uwekezaji wenye matokeo chanya

“Baadhi ya wanawake walijifungua njiani,” amesema Sa’aida, mkunga kutoka Bot, eneo lililoko jimboni la Blue Nile nchini Sudan. “Tulitoa huduma za dharura na msaada wowote uliokuwa unahitajika. Kama kusingekuwa na wakunga waliopata mafunzo, hali ingekuwa ngumu sana.”

Sa’aida ni mkunga ambaye anatoa simulizi yake kupitia chapisho la shirika la Umoja wa Maifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya watu, UNFPA.

Kuanzia Januari hadi Mei 2026, mapigano makali yalisababisha makumi ya maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao katika Jimbo la Blue Nile, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. 

Wakati wengi wao wakisaka hifadhi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani zenye msongamano , ghasia zinazoendelea, uharibifu wa miundombinu na mafuriko ya mara kwa mara vinafanya upatikanaji wa huduma muhimu za afya kuwa mgumu sana.

“Kungeweza kutokea vifo kutokana na kutokwa damu nyingi,” Sa’aida amesema hayo akiongeza kuwa, “Mama angeweza kupoteza maisha yake, na mtoto pia.”

Sa’aida naye ni mkimbizi

Sa’aida mwenyewe alilazimika kuyakimbia makazi yake mwaka 2024, na sasa anafanya kazi katika kliniki  tembezi ya afya inayoungwa mkono na UNFPA, iliyowekwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Karama 3, katika mji mkuu wa jimbo hilo, Ad-Damazin.

Yeye ni mmoja wa wakunga 15 waliotumwa na kupewa vifaa kupitia mpango wa UNFPA unaolenga kuwafundisha na kuwaajiri kwa haraka wahudumu hawa muhimu wa afya katika jamii zinazowahitaji zaidi.

Shuhuda za wanufaika – Somaya ni mmojawao

“Bila yeye, ningepata mateso makubwa,” amesema Somaya, ambaye alisaidiwa na Sa’aida kambini. “Hatuna fedha, na hatujui pa kwenda wala namna ya kupata huduma za afya hapa. Bila msaada wake, nisingeweza kufika hospitalini. Kuwepo kwa Sa’aida kambini kumetupatia hisia ya usalama.”

Kukidhi mahitaji mahali yalipo

Safya pia alitumwa na UNFPA katika kambi ya Al Karama, ambapo anahifadhi kumbukumbu za wanawake wote wajawazito na maeneo wanayoishi. “Ikiwa mwanamke haji kuniona, mimi humfuata popote alipo ili kumchunguza na kujua kwa nini hakufika,” amesema.

Nchini Sudan kote, vituo vingi vya afya bado havifanyi kazi, hali inayowaacha wanawake wajawazito waliokimbia makazi yao bila huduma salama na endelevu za uzazi. Timu za UNFPA zinaendesha kliniki tembezi za huduma za uzazi pamoja na maeneo salama katika sehemu mbalimbali za nchi, lakini nyingi zimelazimika kufungwa kutokana na upungufu mkubwa wa ufadhili.

“Wanawake wengi hujifungulia hapa kambini, lakini baadhi ya wagonjwa wanahitaji kupelekwa hospitalini, hasa akina mama wenye umri mkubwa na wale ambao wamejifungua mara nyingi hapo awali,” amesema Safya akiongeza kuwa. “Siwezi kuhatarisha maisha yao. Kila ninapobaini kuwa kuna tatizo la uzazi linalohitaji huduma maalumu, huhakikisha mama huyo anapelekwa hospitalini mara moja.'

Shuhuda ya huduma ya Safya

Al Raddyia, mama wa watoto 11, alipowasili kambini akiwa katika hatua za mwisho za ujauzito, alipata huduma ya kliniki ya wajawazito kutoka kwa Safya 

"Nilianza uchungu wa kujifungua na nilipata maumivu ya uzazi kwa siku nzima. Maumivu yalipozidi, nilimpigia simu na alifika mara moja. Aliniuliza nimewahi kujifungua watoto wangapi hapo awali. Nikamwambia huyu ni mtoto wangu wa kumi na mmoja."

Safya alitambua kuwa Al Raddyia alikuwa katika hatari kubwa wakati wa kujifungua na akampeleka mara moja katika Hospitali ya Wazazi ya Ad-Damazin, ambako alijifungua salama.

"Hata baada ya kujifungua, Safya alikuwa akinitembelea kila baada ya siku mbili ili kuhakikisha mimi na mtoto tunaendelea vizuri," Al Raddyia ameiambia UNFPA.

Kwa sasa mama na mtoto wanaendelea vizuri kiafya. Hata hivyo, bila huduma ya mkunga mwenye ujuzi, matokeo yangeweza kuwa tofauti kabisa.

Wakunga: Uwekezaji wenye manufaa makubwa katika huduma za afya

Wakunga wana uwezo wa kutoa karibu huduma zote muhimu za afya ya uzazi na afya ya ngono. Huduma hizo ni pamoja na kuhamasisha uzazi wa mpango, kutambua na kuwapeleka wagonjwa wenye dharura za uzazi katika vituo vya rufaa, kuwasaidia manusura wa ukatili wa kijinsia, pamoja na kuchangia katika ufuatiliaji wa magonjwa na elimu ya afya.

"Wanawake wajawazito huja kwangu mara kwa mara kuniuliza kuhusu maendeleo ya ujauzito wao na hatua wanazopaswa kuchukua ili kubaki na afya njema," amesema Safya. "Humfuatilia kila mama kuanzia mwezi wa tatu wa ujauzito hadi atakapojifungua salama."

Uwekezaji katika taaluma ya ukunga unatambuliwa duniani kuwa mojawapo ya njia zenye gharama nafuu, zenye mafanikio makubwa na endelevu katika kuboresha afya na kuongeza nafasi ya kuishi kwa mama na mtoto mchanga.

Kuokoa maisha kupitia ujuzi na maarifa

Katika wiki tatu za kwanza tangu walipoanza kazi, wakunga wanaoungwa mkono na UNFPA walisaidia kujifungua salama kwa akina mama 140 na kutoa huduma za ufuatiliaji kwa zaidi ya wanawake wajawazito 700.

Kwa ufadhili wa Serikali ya Norway, UNFPA kwa sasa inawapa mafunzo wakunga wengine 30 katika Jimbo la White Nile na wakunga wengine 30 katika Jimbo la Kordofan Kaskazini.

 Wakunga hao watapelekwa kufanya kazi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya ya uzazi na afya ya ngono.

UNFPA pia inaendelea kutoa huduma za rufaa kwa Hospitali ya Wazazi ya Ad-Damazin kwa wanawake wanaohitaji kujifungua kwa upasuaji, pamoja na kutoa msaada wa fedha taslimu na vocha kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wanaokabiliwa na matatizo mengine wakati wa kujifungua.

Mwaka 2026, UNFPA inaomba msaada wa dola za Marekani milioni 129.2 ili kukidhi mahitaji muhimu ya huduma za afya ya uzazi, pamoja na hatua za kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini Sudan. Hadi sasa ni theluthi moja tu ya ombi hilo imepatikana.