Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wakimbia makazi yao kufuatia mapigano Kivu Kusini, DRC

Mwanamke mmoja huko Sange, Wilaya ya Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anabeba sanduku la Biskuti za High Energy za WFP kichwani mwake baada ya kupokea msaada wa dharura wa chakula kwa familia za watu waliohamishwa.
© WFP/Musa Abema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. WFP inatoa chakula cha dharura kwa familia zinazokimbia vurugu huko Uvira, kuhakikisha hakuna mtu anayekufa njaa wakati wa mgogoro (MAKTABA)

Maelfu wakimbia makazi yao kufuatia mapigano Kivu Kusini, DRC

Amani na Usalama
  • Mapigano yamefurusha zaidi ya watu 48,000
  • Mapigano ni ya kuanzia katikati ya mwezi Julai
  • Huduma zimevurugika, OCHA yatoa wito kwa pande kinzani

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mapigano yanayoendelea katika maeneo ya nyanda za juu jimboni Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yanaendelea kuwalazimu maelfu ya wananchi kuyakimbia makazi yao huku yakivuruga upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

OCHA kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wake, imenukuu washirika wake wa kiutu wakisema kuwa tangu katikati ya mwezi uliopita wa Julai, mapigano katika maeneo ya Uvira, Fizi na Mwenga yamesababisha zaidi ya watu 48,000 kuyahama makazi yao.  Aidha, vifo na majeruhi miongoni mwa raia pamoja na uharibifu wa miundombinu muhimu vimeripotiwa.

Vyanzo vya habari vinaripoti kuwa mapigano hayo ni kati ya jeshi la serikali, (FARDC) na makundi yaliyojihami likiwemo M23.

Misaada ya kibinadamu yakwama

OCHA imeeleza kuwa hali ya ukosefu wa usalama, kufungwa kwa barabara, uharibifu wa miundombinu na hitilafu za mawasiliano ya simu vinaendelea kuzuia:

  • Kufikishia wahitaji misaada ya kibinadamu.
  • Uokoaji na usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.
  • Upatikanaji wa huduma za msingi kwa wananchi walioathirika.

Huduma za afya zatikisika

Sekta ya afya imeathirika vibaya kwa kiwango kikubwa kutokana na uharibifu wa vituo vya afya na kuondoka kwa wahudumu wa afya katika maeneo yaliyoathirika. Tangu mwezi Januari, zaidi ya watu 80 waliojeruhiwa kutokana na mapigano na mabaki ya vilipuzi vya kivita wameshindwa kupata matibabu wanayohitaji.

Hofu ya Ebola yaendelea

Wakati huo huo, juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola zinaendelea katika jimbo hilo.

 Maafisa wa afya wanafuatilia watu 55 waliobainika kuwa waliwasiliana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.

Kufikia tarehe 1 Agosti, mamlaka za afya za kitaifa zimeripoti jumla ya watu 3,748 waliothibitishwa kuwa na Ebola katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele na Tshopo.

Wito wa OCHA

OCHA imetoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo kuchukua hatua zifuatazo:

  • Kulinda raia dhidi ya madhara ya mapigano.
  • Kuruhusu upatikanaji salama na endelevu wa misaada ya kibinadamu.
  • Kurejesha huduma za mawasiliano ya simu ili kusaidia ulinzi wa raia, juhudi za afya ya umma na shughuli za misaada.

“Mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa bila kuboreshwa kwa hali ya usalama na upatikanaji wa huduma, maelfu ya wananchi wataendelea kukabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa mateso, magonjwa na ukosefu wa huduma muhimu,” imesema taarifa hiyo ya OCHA.