Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SDG 9: Wakfu wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya unavyowasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao

Mwanamume aliyevaa suti amesimama mbele ya bango la Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu katika Chuo Kikuu cha Mt. Kenya.
UN News/Anold Kayanda Profesa Peter Wanderi Mwangi ambaye amewakiwakilisha Chuo Kikuu cha Mount Kenya cha nchini Kenya chenye matawi mbalimbali katika Afrika Mashariki katika mkutano wa United Nations Academic Impact (UNAI), Mpango unaosisitiza nafasi muhimu ya taasisi za elimu ya juu katika kuhimiza maendeleo endelevu na kuunga mkono utekelezaji wake.

SDG 9: Wakfu wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya unavyowasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Chuo Kikuu cha Mount Kenya cha nchini Kenya chenye matawi mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki ni moja ya taasisi za kitaaluma duniani zilizoko katika  kile kwa lugha ya Kiingereza kinafahamika kwa jina ‘United Nations Academic Impact (UNAI)’, huu ni mpango wa Umoja wa Mataifa unaozipa nafasi muhimu taasisi za elimu ya juu kushiriki katika kuhimiza Malengo 17 ya maendeleo endelevu,SDG na kuunga mkono utekelezaji wake.

Chuo hiki cha Mount Kenya kilichagua jukumu la kutekeleza lengo namba 9 yaani SDG9 linalolenga kuendeleza viwanda, ubunifu na miundombinu.
 
Ili kufahamu ni kwa namna gani Chuo Kikuu cha Mount Kenya kinawasaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kifedha lakini wana uwezo wa kitaaluma, Anold Kayanda wa Idhaa hii amezungumza na Profesa Peter Wanderi Mwangi ambaye alikiwakilisha chuo hicho katika Kongamano la Kimataifa kuhusu Elimu ya Juu lililofanyika mwezi uliopita hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, kongamano lililoendeshwa kupitia UN Global Compact.
 
“Tuna njia mbili ama tatu lakini nitataja mbili. Kwanza chuo kikuu hapo mwanzoni kilianzisha ‘Mount Kenya University Foundation’. Wakfu huu unachangia kutafuta pesa ya kusaidia wanafunzi ambao hawana njia ya kujilipia. Kawaida wanakuja wakitarajia watapata msaada lakini kuna shida hapa na pale labda msaada haupatikani. Ama mtu akiingia katika chuo anapata shida ambapo Wakfu unakuja kumsaidia.” Anasema Profesa Wanderi.
 
Mwanazuoni huyo anasema wakati mwingine wanatafuta mashirika mengine yanayoweza kutoa mdaa kwa wanafunzi ili waweze kukamilisha masomo yao na baadaye kuingia katika jamii kusaidia kuendeleza viwanda, ubunifu na miuondombinu.

Masomo nje ya nchi

Profesa Wanderi anaeleza kwamba baadhi ya wanafunzi wanapelekwa katika nchi nyingine ili kuongeza maarifa na ujuzi, “mathalani nchini Ujerumani kwa miezi mitatu” katika Chuo Kikuu cha Munich na wanafundishwa halafu wanarudi nyumbani.
 
“Kwa hivyo hizo ndizo shughuli zile ambazo tunachangia katika kuhakikisha hii leo hili lengo namba tisa (SDG9) linaendelea hapa nchini (Kenya).” Anahitimisha Profesa Peter Wanderi Mwangi.