Unyonyeshaji ni msingi wa afya ya mtoto, serikali zichukue hatua
Chonde chonde, serikali chukueni hatua kuimarisha mifumo ya afya na huduma za kusaidia akina mama kunyonyesha vema watoto wao wachanga, ili kuhakikisha kila mtoto anaanza maisha akiwa na afya bora. Ni kauli kwenye ujumbe wa pamoja wa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na la Afya Duniani (WHO), ujumbe uliomo kwenye taarifa yao ya pamoja iliyotolewa New York, Marekani na Geneva, Uswisi wakati huu ambapo Wiki ya Unyonyeshaji Mtoto Maziwa ya Mama ikianza leo duniani kote.
Wakuu wa mashirika hayo Catherine Russell, wa UNICEF na Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, wamesema bado akina mama na familia nyingi duniani hawapati huduma na msaada unaohitajika ili waweze kunyonyesha watoto wao ipasavyo.
"Unyonyeshaji ni moja ya njia rahisi lakini zenye nguvu zaidi za kulinda afya ya mtoto. Kwa kuwekeza katika huduma zinazothibitishwa kufanya kazi, tunaweza kumpa kila mtoto mwanzo bora wa maisha na kuhakikisha kila mama anapata huduma na msaada anaohitaji,"imesema taarifa hiyo.
Wamesema kuimarisha unyonyeshaji ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa afya na maendeleo ya jamii.
UNICEF na WHO zimetaja mambo 9 ya kuzingatiwa na serikali:
- Kuimarisha mifumo ya afya ili itoe huduma bora za unyonyeshaji.
- Kupanua huduma za ushauri nasaha katika jamii.
- Kuimarisha programu za usaidizi wa akina mama wanaonyonyesha.
- Kutekeleza kikamilifu Kanuni za Kimataifa za Udhibiti wa Uuzaji wa Mbadala wa Maziwa ya Mama.
- Kudhibiti biashara na matangazo yanayodhoofisha unyonyeshaji.
- Kuwekeza katika likizo ya uzazi yenye malipo.
- Kuboresha sera rafiki za maeneo ya kazi kwa akina mama wanaonyonyesha.
- Kujumuisha huduma za unyonyeshaji katika huduma za ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.
- Kuendelea kutoa huduma hizo hata katika maeneo yenye migogoro na majanga.
Kwa nini unyonyeshaji ni muhimu?
- Humpatia mtoto lishe kamili katika miezi ya mwanzo ya maisha.
- Huimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.
- Hupunguza hatari ya magonjwa makubwa na vifo vya watoto.
- Huchochea ukuaji wa ubongo na uwezo wa kujifunza.
- Humlinda mama dhidi ya saratani ya titi na viungo vya uzazi, pamoja na kisukari aina ya pili.
- Hupunguza gharama za matibabu kwa familia na serikali.
- Huchangia mafanikio ya elimu na kipato cha mtoto baadaye maishani.
- Huongeza tija ya uchumi kupitia afya bora ya jamii.
- Kila dola moja inayowekezwa katika kuhamasisha unyonyeshaji inaweza kurejesha takribani dola 59 katika faida za kiuchumi.
Maendeleo yanaonekana
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiwango cha unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza kimeongezeka kutoka asilimia 37 mwaka 2012 hadi zaidi ya asilimia 47 mwaka 2026.
Aidha, unyonyeshaji hadi mtoto anapofikisha miaka miwili umeongezeka kutoka asilimia 38 hadi asilimia 50 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Hata hivyo, mashirika hayo yamesema bado kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji na utekelezaji wa sera ili kufikia malengo ya kimataifa ya afya ya watoto na akina mama.