El Nino: Tunakabiliwa na hali mpya isiyokuwa na mfano - Guterres atoa mapendekezo manne
El Nino: Tunakabiliwa na hali mpya isiyokuwa na mfano - Guterres atoa mapendekezo manne
- Kulinda maisha ya wananchi
- Kulinda wafanyakazi
- Kujenga miundombinu inayostahimili joto
- Kukabiliana na chanzo cha tatizo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema dunia inaingia katika kipindi hatari cha ongezeko la joto kali kutokana na kuimarika kwa mkondo wa mawimbi oto baharini au El Niño pamoja na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na matumizi ya nishati ya mafuta kisukuku.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani Ijumaa Julai 31 baada ya kutolewa kwa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa (WMO), Guterres amesema utabiri unaonesha kuwa kuanzia mwezi ujao wa Agosti hadi Oktoba mwaka huu karibu maeneo yote ya nchi kavu duniani yatakuwa na joto la juu kuliko kawaida, hali inayoweza kuvunja rekodi nyingi za hali ya hewa.
Guterres: Dunia iko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa
Katika hotuba hiyo alimozungumzia pia ziara yake ya hivi karibuni Mashairki ya Kati na Cyrpus, Guterres amesema dunia sasa iko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, akionya kuwa El Niño inaongeza nguvu kwenye sayari ambayo tayari imeathiriwa vibaya na ongezeko la joto duniani.
Amesema jkinachozua tafrani si mizozo pekee bali pia joto kali kupindukia na kwamba, joto kali si tishio la baadaye bali ni janga linaloendelea sasa, likisababisha vifo, kuathiri vibaya afya za watu na kuzorotesha uchumi katika maeneo mbalimbali duniani.
Madhara ya joto la kupindukia
Katibu Mkuu huyo amesema joto kali linaendelea kusababisha mambo kadhaa ikiwemo :
- Vifo vinavyoongezeka duniani, ingawa vingi havirekodiwi rasmi kama vinavyotokana na joto.
- Familia kuishi katika makazi yasiyo salama.
- Wafanyakazi kulazimika kuchagua kati ya kulinda afya zao au kupata kipato.
- Watoto kushindwa kujifunza kutokana na mazingira ya joto kupita kiasi.
- Miji mingi kushindwa kutoa huduma kwa ufanisi.
Walio hatarini zaidi
Kwa mujibu wa Guterres, makundi yanayoathirika zaidi na joto kali ni watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wafanyakazi wanaofanya kazi zao maeneo ya nje.
Nini Kifanyike?
Guterres amezitaka serikali duniani kuchukua hatua zifuatazo:
1. Kulinda maisha ya wananchi
- Kuandaa mipango ya kitaifa na mijini ya kukabiliana na joto kali.
- Kuimarisha mifumo ya utabiri na tahadhari za mapema.
- Kuhakikisha upatikanaji wa njia endelevu za kupunguza joto kwa usawa.
2. Kulinda wafanyakazi
- Kuweka viwango vya usalama mahali pa kazi wakati wa joto kali.
- Kubadili saa za kazi ili kupunguza hatari.
- Kulinda mishahara pale kazi zinaposimamishwa kutokana na joto.
3. Kujenga miundombinu inayostahimili joto
- Kuboresha miji, nyumba, shule na hospitali ili ziweze kuhimili joto kali.
- Kujumuisha hatua za kukabiliana na joto katika mipango ya maendeleo na bajeti za serikali.
4. Kukabiliana na chanzo cha tatizo
- Kupunguza matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi.
- Kusitisha uidhinishaji wa miradi mipya ya nishati za mafuta.
Wito wa haraka
Guterres amesema dunia inatumia fedha nyingi kuchochea mabadiliko ya tabianchi kupitia ruzuku za nishati ya mafuta kisukuku, badala ya kuwalinda wananchi dhidi ya athari zake.
Amesisitiza kuwa joto kali tayari limefika na linaendelea kuwa hatari zaidi kila mwaka, akionya kuwa bila hatua za haraka za kuwalinda watu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, madhara yataongezeka na kugharimu maisha na uchumi duniani.
Soma hotuba nzima hapa.