Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataka mwitikio wa kimataifa dhidi ya biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu

Mwanamke akiwasili Lajas Blancas, Panama, baada ya kuvuka Darien Gap.
Alejandra Silva/ UNODC Mwanamke akiwasili Lajas Blancas, Panama, baada ya kuvuka Darien Gap.

Guterres ataka mwitikio wa kimataifa dhidi ya biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu

Haki za binadamu

Biashara haramu ya usafrishaji wa binadamu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu amekumbusha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na  akatoa wito wa kuwepo kwa mwitikio wa pamoja unaoweza kubaini mitandao hiyo ya uhalifu na kukatiza vyanzo vyao vya fedha.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa Dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu inayoadhimishwa kila mwaka tarehe thelathini Julai, amesema wahalifu wanawavutia watu kwa ahadi za ajira nzuri, lakini baadaye wanawafanya mateka na kuwalazimisha kuendesha utapeli mtandaoni.

Guterres amezitaka nchi kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Uhalifu wa Mtandao uliopitishwa mwaka 2024, kushirikiana kuvunja mitandao ya uhalifu na kuwasaidia manusura kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Biashara haramu ya binadamu kwa madhumuni ya uhalifu imeongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), aina hii ya unyonyaji imeongezeka kutoka asilimia moja ya waathirika waliogunduliwa duniani mwaka 2016 hadi asilimia nane mwaka 2022.

Msichana mchanga katika vazi jeupe anasimama mbele ya ukuta uliofunikwa na maandishi, ikiwa ni pamoja na ujumbe 'NAKUPENDA' ulioandikwa kwa kijani.
© UNICEF/Ron Haviv Watu wanaouzwa na kulazimishwa kufanya kazi katika vituo vya udanganyifu wanakabiliwa na mateso, unyanyasaji wa kijinsia na hali kama za gereza.

Wengi wanaolengwa ni kutoka Afrika

Aidha, mwaka 2022, waathirika wenye uraia kutoka nchi 162 walisafirishwa kwa biashara hiyo haramu katika nchi 128. Kwa upande mwingine, takribani asilimia 70 ya watu waliochunguzwa, kushtakiwa na kutiwa hatiani kwa makosa ya biashara haramu ya binadamu walikuwa wanaume.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, waathirika kutoka Afrika ndio kundi linalolengwa zaidi na mashirika ya uhalifu, wakichangia asilimia 31 ya biashara haramu ya binadamu inayovuka mipaka.

Ajira kupitia majukwaa ya kidijitali

Biashara haramu ya usafirishaji binadamu kwa ajili ya uhalifu wa kulazimishwa hutokea pale watu wanapotumiwa na kulazimishwa kufanya uhalifu kwa manufaa ya wafanyabiashara hao haramu, mara nyingi kupitia udanganyifu, vitisho au kulazimishwa.

Mara nyingi, mchakato wa ajira huanza kwenye majukwaa ya mtandaoni. Matangazo bandia ya ajira hulenga watu wanaozungumza lugha nyingi, wenye ujuzi wa kidijitali na wanaofahamu matumizi ya mitandao ya kijamii.

Ulaghai wa mtandaoni si uhalifu pekee wanaolazimishwa kufanya waathirika hao. Pia hulazimishwa kushiriki katika shughuli mbalimbali haramu, ikiwemo wizi, biashara ya dawa za kulevya, udanganyifu wa kifedha na ulaghai wa mtandaoni.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 300,000 kwa sasa wamefungwa katika vituo vinavyodhibitiwa na mashirika hayo ya uhalifu.

Afisa wa usalama wa kike mwenye sura ya ki-Asia, amevaa kofia nyeusi na kanzu ya polo iliyo na nembo ya Umoja wa Mataifa, anazingatia kazi ya kukagua mizigo katika uwanja wa ndege.
© UNODC Wawakilishi wa UNODC wanapitia maandishi na nyaraka zingine ambazo walaghai hutumia kuwashawishi waathirika wao katika kituo cha udanganyifu kilichoshambuliwa katika mji mkuu wa Cambodia Phnom Penh. Desemba 2025.

Ulinzi wa waathirika kiini cha mwitikio

Kutokana na kuenea kwa biashara haramu ya usafrishaji watu binadamu katika maeneo mbalimbali duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limeongeza wito wake wa kuimarisha kinga, ulinzi wa waathirika, ushirikiano wa kuvuka mipaka na ubia madhubuti ili kuvunja mitandao ya biashara hiyo haramu.

Mapema mwaka huu, IOM imezindua Mkakati wake Mpya wa Kikanda wa Kukabiliana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kwa Ajili ya Uhalifu katika Asia na Pasifiki kwa kipindi cha 2026 hadi 2030.

Mpango huo unalenga kuhakikisha ulinzi wa waathirika, kuimarisha ushirikiano wa kuvuka mipaka na kuongeza nguvu za ubia katika kuvunjwa kwa mitandao ya biashara hiyo haramu.

IOM imesisitiza kuwa watu wanaolazimishwa kufanya uhalifu ndani ya vituo vinavyoendeshwa na mitandao ya biashara hiyo haramu ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu, na hivyo wanapaswa kulindwa.