Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa inakwamisha juhudi za kukabiliana na Ebola huku wagonjwa wa Ebola wakiongezeka kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwanachama wa timu ya kusafisha uchafu akiwa amevaa suti ya hatari akinyunyizia dawa jengo huko Bunia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Carmel Ndomba Mbikayi Nyumba ya mtu aliyethibitishwa kuwa na Ebola inasafishwa kwa dawa ya kuua vijidudu katika kijiji cha Brazza, Bunia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Njaa inakwamisha juhudi za kukabiliana na Ebola huku wagonjwa wa Ebola wakiongezeka kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Afya

Mlipuko wa sasa wa ebola ya virusi vya Bundibugyo uliotangazwa rasmi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwezi Mei mwaka huu unazidi kuongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida, wakati huu maambukizi ni zaidi ya watu 3,200.

Ni kauli za maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa waliyoitoa wakati wakizungumza na waandishi wa habari. Karl Skau Kaimu Mkuu wa WFP ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, na Julien Harneis Mratibu wa Ebola wa Umoja wa Mataifa wamesema huu ndio mlipuko wa Ebola unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa. 

Kwa kulinganisha, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, watu 1,000 wamefariki dunia nchini DRC ilhali katika mlipuko wa Afrika Magharibi, ilichukua miezi minane kufikia vifo 1,000. 

Kasi ya ugonjwa ni kubwa kuliko mwitikio

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani siku ya Jumatano Julai 29 kutokea Bunia jimboni Ituri, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola Julien Harneis amegusia kasi ya ugonjwa akisema.

«Katika saa 24 zilizopita watu 15 wamekufa kwa Ebola DRC na idadi ya wagonjwa inaongezeka kwa kasi, ikiwa ni maradufu katika kila siku 20. Kasi ya ongezeko ni kubwa kuliko kasi yetu ya mwitikio."

Amezungumzia pia watoa huduma wanaosaidia harakati za kudhibiti ebola akisema, "Lakini nimeshuhudia pia kazi ya kipekee ya watu kwenye jamii kama Grace na Christine wanaopika chakula cha WFP kwa ajili ya wagonjwa walioko kwenye vituo karibu na nyumbani kwao. Pia wahudumu wa kujitolea kwa Msalaba MWekundu wanaozika waliofariki dunia, vile vile wauguzi, madaktari na wakongomani kutoka bara la Afrika na kote duniani. »

Kudhibiti Ebola ni mpango mtambuka - chakula na matibabu

Upatikanaji wa chakula kwa mujibu wa WFP ni moja ya muarobaini wa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo ambao virusi vya sasa vya Bundibugyo havina chanjo wala tiba. 

Kaimu Mkuu wa WFP Carl Skau akizungumza kwenye mkutano huo yeye amesema mtu anaweza kudhania kwamba kudhibti ebola ni kutibu tu wagonjwa, “lakini  Hapana. Hii kutokana na uzoefu wetu, inahitaji mbinu mbalimbali ikiwemo chakula. Hatuwezi kuwatenga wagonjwa bila kuwapatia pia chakula. Wahudumu wa afya hawawezi kufanya kazi kutwa kucha kwenye mazingira haya hatari bila kuwapatia chakula. Na kwa kweli tuna jamii nzima ambayo imefungiwa ndani na tunatarajia wasalie ndani, na pia wanapaswa kupatiwa chakula.”

Wametamatisha mkutano wao wakisihi ufadhili zaidi kwa mashirika ya kiutu, halikadhalika usalama ili huduma dhidi ya ebola ziweze kufikia wahusika kwani kasi ya maambukizi ni kubwa kuliko.

Wananchi wazungumzia mlipuko ulivyokwamisha maisha yao

Lakini hali mashinani ikoje? Video ya WFP inatuinatupitisha Bule, kitongoji kilichoko eneo la Djugu, jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Eneo hili limetelekezwa. Makazi matupu! Maduka yamefungwa! Hakuna dalili za uhai hapa! Utauliza kulikoni? Ni kwa sababu ya mashambulizi yanayofanywa na waasi kila uchao. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema eneo hili lina rasilimali kama madini ambayo waasi wakivamia, hubeba kisha huuza kiharamu na kujipatia fedha za kuendeleza shughuli zao.

Vifurushi vya chakula WFP vyasambazwa kwa manusura wa Ebola na watu waliogusana nao huko Muchanga, Katwa, Butembo.
Picha ya UN/Martine Perret Kama sehemu ya mwitikio wa Dharura wa Ebola, WFP husaidia kudhibiti Ebola kwa kuwapa chakula manusura na watu ambao wanaweza kuwa na virusi hivyo.

Sasa tumulika msingi wa mada hii ambayo ni harakati za shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo duniani, WFP za usaidizi wa kibinadamu wakati huu ambapo eneo hili limegubikwa sio tu na mapigano bali pia mlipuko wa Ebola.

Katika kambi ya raia waliokimbia mashambulizi na kuishi katika makazi ya vibanda vilivyofunikwa kwa mahema, wakimbizi wengine wanaendelea kujenga vibanda vipya, huku vingine ni chakavu. Watoto wanapitapita.

Dorica Hanibaliye ni mmoja wa wakimbizi wa ndani hapa Djugu anaelezea jinsi mlipuko wa sasa wa Ebola uliotangazwa mwezi Mei mwaka huu wa 2026 umekuwa na madhara kwenye maisha yao.

"Tangu mlipuko ulipoanza, tumeshindwa kuendelea na shughuli zetu za kila siku kwa sababu tunaishi katika hofu ya kudumu ya ugonjwa huu. Chakula kilikuwa haba, na bei za bidhaa sokoni zilipanda sana."

Mgao wa chakula pamoja na kinga dhidi ya Ebola

Ni kutokana na hali hiyo, WFP iliamua kuwapatia msaada wa chakula wakimbizi wa ndani.

Wakimbizi wa ndani wanapanga foleni kupokea mgao wa chakula. Wanaume, wanawake tena wengine wamebeba watoto wao. Tangazo..

Kandoni mwa hema walimopanga foleni wakisubiri mgao, kuna ndoo yenye maji, lengo ni kuhakikisha usafi wa mikono, njia mojawapo ya kujikinga na Ebola.

Halikadhalika, mfanyakazi wa WFP amebeba kipima joto ili kila aliyepanga foleni apimwe kwanza iwapo joto la mwili haliko zaidi ya kiwango kinachotakiwa ili apatiwe huduma ya matibabu. Hii ni kwa kuwa joto la mwili likiwa juu, ni moja ya viashiria ya mhusika kuwa na ugonjwa, pengine hata Ebola.

Mgao ni mafuta ya kula, maharage na unga wa mahindi

Video inatusogezea karibu vyakula ambavyo kaya zinapatiwa na ni unga wa mahindi, maharage na mafuta ya kula.

Miongoni mwa waliopata mgao huu wa chakula kutoka WFP ni mwendesha bodaboda aitwaye Kanana. Yeye anasema sasa biashara ya bodaboda imepungua na ndio maana kafuata mgao wa chakula. Akisema motoo anamaanisha pikipiki au bodaboda.

"Siku hizi, wateja hawatumii tena bodaboda kama walivyokuwa wakifanya hapo awali kwa sababu wanaogopa kuambukizwa Ebola. Wana hofu kwamba huenda mtu mwenye Ebola alitumia pikipiki hiyo kabla yao. Hivyo, hatupati wateja wengi kama tulivyokuwa tukipata zamani."

Kituo cha afya chapatia watoto na akina mama vyakula vilivyorutubishwa

Katika kituo cha afya cha Salama, akina mama na watoto wao pamoja na akina baba wakiwa na watoto. Kinachoendelea, mhudumu wa afya anaelimisha kuhusu lishe bora, kwani uhaba wa chakula umesebabisha watu zaidi ya milioni 2.65 kwenye kanda 48 za kiafya zilizokumbwa na Ebola kuwa na uhaba mkubwa wa chakula. Muuguzi   kwenye kituo hicho kinachopata usaidizi kutoka WFP, anapatia wazazi vyakula vyenye virutubisho kwa ajili ya watoto wao.

Jean de Dieu Nduwingal ni Muugusi katika kituo hiki cha afya anasema, "Kwa sasa, Kituo cha Afya cha Salama kinashuhudia ongezeko kubwa la watoto wenye utapiamlo mkali. Mara nyingi tunaona watoto watatu au wanne wenye utapiamlo wakiletwa kwa wakati mmoja, wakiambatana na mama zao ambao nao pia wana utapiamlo."

Wafanyakazi wa WFP na watawala wanabeba masanduku ya vifaa, ikiwemo kinga za uso, kwenye kituo cha usafirishaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa mlipuko wa Ebola.
© WFP/Michael Castofas Wafanyakazi wa WFP na wasaidizi wanabeba masanduku ya vifaa vya matibabu katika kituo cha usafirishaji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati wa mlipuko wa Ebola.