Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu mpya wa UN kuingia ng’we nyingine

Jina la Katibu Mkuu kwenye dawati la mbao katika Jumba la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiwa na viti vya bluu na picha kubwa ya ukuta.
UN Photo/Loey Felipe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huzungumza mara kwa mara katika Baraza la Usalama. (pichani)

Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu mpya wa UN kuingia ng’we nyingine

Masuala ya UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakuwa na upigaji kura usio rasmi kesho Alhamisi wenye lengo la kutathmini uungwaji mkono wa wagombea saba waliojitokeza kumrithi Katibu Mkuu wa sasa Antonio Guterres anayemaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu.

Je ni nini kinafanyika? Assumpta Massoi amekuwa anafuatilia mchakato huu na nimezungumza naye angalau atupatie kwa muhtasari.

Hebu tueleze wagombea ni wangapi kwanza?

Bila shaka Anold. Wagombea hadi katikati ya wiki iliyopita walikuwa sita lakini Ijumaa ya Julai 24 idadi iliongezeka na kuwa 7 baada ya Olara Otunnu, mwanadiplomasia kutoka Uganda kuwasilisha jina lake. Wengine ni Michelle Bachelet kutoka Chile, Maria Fernanda Espinosa kutoka Ecuador, Rafael Grossi kutoka Argentina, Rebeca Grynspan kutoka Costa Rica, Carolyn Rodrigues Birkett kutoka Guyana na Macky Sall kutoka Senegal. Wagombea wote isipokuwa Otunnu, walishakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Baraza la Usalama na Baraza Kuu.

Kolagi ya picha saba za kitaalamu za wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu, ikionyesha kundi tofauti la wanawake na wanaume wakiwa wamevalia mavazi rasmi ya kibiashara.
Umoja wa Mataifa Wagombea saba walioteuliwa kuwa Katibu Mkuu UN ; Michelle Bachelet (Chile), María Fernanda Espinosa (Ecuador), Rafael Grossi (Argentina), Rebeca Grynspan (Costa Rica), Olara Otunnu (Uganda), Carolyn Rodrigues Birkett (Guyana) na Macky Sall (Senegal).
Lakini watu walidhania kuwa hii ni zamu ya ukanda wa Amerika ya Kusini, kwamba nafasi hii ni mzunguko wa mabara?

Ni kweli imezoeleka hivyo lakini ni kanuni ambayo haijaandikwa. Azimio la mwaka 1997 la  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilieleza kwamba uzingatiaji unaofaa unapaswa kutolewa kwa mzunguko wa uwakilishi wa kijiografia, lakini hilo limeendelea kuwa desturi isiyo rasmi badala ya kuwa sharti la kisheria.

Sasa hiyo kesho nini kitafanyika?

Kwanza kabla ya kueleza hilo, nikujulishe tu Anold kwamba mfumo huu wa kupiga kura utakaotumiwa kesho ulibuniwa na mmoja wa wagombea wa sasa, Olara Otunnu wakati huo Uganda ikiwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1981. Baraza kupitia kura turufu lilishindwa kusonga mbele kwenye kumpata nani asonge mbele katika kupigiwa kura na kupendekezwa kwa Baraza Kuu. Hivyo akaibuka na mfumo huo kwa lugha ya kiingereza Straw Poll.

 Sasa kitakachofanyika kesho, kwa mujibu wa Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Julai, Balozi  Zénon Mukongo Ngay, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye Umoja wa Mataifa, kwenye duru ya mwanzo ya upigaji kura, wanachama wote 15 watatumia karatasi zinazofanana za kura kila moja ikiwa na jina la mgombea ili kuonesha msimamo wa jumla kuhusu wagombea. Wataandika Kuhimiza au Kutohimiza au sina maoni.

Katika duru zinazofuata, kura za wanachama watano wa kudumu wenye kura turufu au veto, ambazo ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani zitatofautishwa kwa rangi maalumu ili kubainisha iwapo mgombea anakabiliwa na kura ya "kutokuhimiza" ambayo inaweza kusababisha matumizi ya kura ya turufu.

Ishara ya Umoja wa Mataifa kwenye sakafu ya Duka la Mkutano Mkuu.
UN Photo/Loey Felipe Picha ya Crest ya Umoja wa Mataifa katika Ukumbi wa Mkutano Mkuu.
Sasa hii ina maana gani?

Wachambuzi wanasema hii inaweza kusababisha mgombea anayepata kura ya kutohimizwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro.

Sasa baada ya hapo?

Baada ya hapo mchakato unaofuata ni Baraza kuwa na kikao cha faragha cha kuamua kuhusu mgombea, na kisha linapitisha azimio la kumpendekeza mgombea huyo kwa Baraza Kuu.

Na Baraza Kuu linafanya nini?

Baraza Kuu sasa linakutana kujadili pendekezo la Baraza la Usalama na kisha kupitisha azimio la kumteua Katibu Mkuu.

Je imewahi kutokea Baraza Kuu likakataa azimio hilo?

Katu haijawahi kutokea. Na ni kwamba Katiba ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa Katibu Mkuu atateuliwa na Baraza Kuu kufuatia mapendekezo ya Baraza la Usalama.

Shukrani sana Assumpta Massoi kwa ufafanuzi huo, macho na masikio ni kwenye Baraza la Usalama.